|
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akichangia mada kwenye Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Afya wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mei 3, 2024. |
Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Afya katika Nchi Wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki wameweka mikakati na kukubaliana kuongeza ushirikiano zaidi katika kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hiyo.
Azma hiyo imefikiwa leo tarehe 3 Mei 2024 kwenye Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Afya wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Dar es Salaam.
Mawaziri hao wamekutana kupitia na maboresho ya mikakati itakayosaidia kutatua changamoto zinazo changia kuzorota kwa ustawi wa sekta ya afya katika Jumuiya.
Sambamba na kufikia azma hiyo Mawaziri hao wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha mifumo na miundombinu ya utoaji wa huduma za afya ikiwemo uimarishaji wa maabara, maboresho ya programu mbalimbali za afya, maboresho ya mafunzo kwa wataalam wa afya, maboresha ya sera za afya, utafiti na ufuatiliaji.
Vilevile wamejadili na kuweka mikakati mahsusi ya kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwashauri na kuwahamasisha wananchi uzingatiaji wa mlo kamili, kufanya mazoezi na kuacha au kupunguza matumizi ya pombe.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Afya nchini Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na utekelezaji wa mikakati hiyo, ambapo amebainisha kuwa katika suala la uhamasishaji wa ufanyaji mazoezi Serikali imechukua hatua ya kufunga daraja la Tanzanite la jijini Dar es Salaam kwa kila Jumamosi ili kuruhusu wananchi kufanya mazoezi katika daraja hilo.
Mbali na hayo Mawaziri hao wamejadili kuhusu namna ya kukabliana na changamoto mbalimbali zinazochangia kuzorota kwa sekta hiyo katika Jumuiya. Wametaja changamoto hizo kuwa ni Mabaliko ya Tabia Nchi, uhaba wa fedha za kuendesha programu na miradi mbalimbali ya afya, milipuko ya magonjwa, kuzuka kwa vita na mapigano kwenye baadhi ya maeneo katika Jumuiya, uhaba wa wataalam na miundombinu isiyotosheleza mahitaji ikiwemo vituo vya afya na vifaa tiba.
Katika kukabiliana na changamoto hizo wamepitisha mikakati ya kukabiliana nazo ikiwemo kuimarisha mfumo wa ununuzi wa dawa kwa pamoja, kupitisha mpango mkakati wa pamoja wa masuala ya afya wa Jumuiya kwa mwaka 2024/2030, kuimarisha ufuatiliaji na utambuzi wa wagonjwa, kukamilisha na kuwasilisha andiko la kuomba fedha za kukabiliana na majanga, kuimarisha afua za kinga ili kutokomeza malaria katika Jumuiya na kuendelea kusimamia Vyuo Vikuu vya Afya ili viendelee kutoa elimu bora ndani ya Jumuiya.
Mkutano huo uliofanyika kwa siku tano kuanzia terehe 29 Aprili hadi tarehe 3 Mei 2024 uliaanza katika Ngazi ya Wataalam ambapo pamoja na masuala mengine walikufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 23 wa Baraza hilo. Tarehe 2 Aprili 2024 uliendelea katika Ngazi ya Makatibu Wakuu na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 3 Mei 2024.
|
Mawaziri na Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta ya Afya katika nchi Wanachama wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja |
|
Makatibu Wakuu wanaosimamia Sekta ya Afya na Elimu katika nchi Wanachama wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja |
|
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Afya wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mei 3, 2024. |
|
Bi. Judith Ngoda Afisa Uchumi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Afya la Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam, Mei 3, 2024. |
|
Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Afya wa Afrika Mashariki ukiendelea
|