Thursday, July 25, 2024

DKT. TULIA AMUAPISHA BALOZI MAHMOUD THABIT KOMBO KUWA MBUNGE

 




 







 

 

 

 




Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Akson amemuapisha Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla ndogo iliyofanyika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam tarehe 25 Julai,2024.

Hafla hiyo ya uapisho imehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Naibu Waziri Mteule wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Lazaro Londo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Naibu Katibu Mkuu Balozi Said Shaib Mussa na watendaji wengine wa Ofisi ya Bunge.

Tarehe 21 Julai, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alimteua Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Mhe. Rais pia aliwateua Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb) kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mhe. Cosato David Chumi (Mb) kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje. Waziri.

 Mhe. Balozi Kombo na Manaibu Waziri wateule wataapishwa tarehe 26 Julai, 2024 Ikulu jijini Dar es salaam.

Wednesday, July 24, 2024

TANZANIA-COMORO ZASAINI HATI NNE ZA MAKUBALIANO


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae wakionesha moja ya Hati za Makubaliano.

Tanzania na Visiwa vya Comoro zimesaini Hati nne za Makubaliano kwenye kilele cha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 jijini Dar es Salaam. 

Hati zilizosainiwa katika kikao hicho zinazojumuisha nyanja za; Ushirikiano wa Kidiplomasia, Afya, Biashara na Viwanda na Teknolojia ya Habari. Utiaji saini hati hizo umeshuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kihistoria, Waziri Tax ameelezea umuhimu wa kusainiwa kwa hati hizo kuwa itawezesha pande hizo mbili kuwa na ushirikiano ulio katika mpangilio mzuri katika nyanja husika na hivyo kuleta tija zaidi.

"Pamoja na kutia saini Hati za Makubaliano pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo mengine mengi ikiwemo miondombinu, nishati, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, utalii, utamaduni, sanaa na michezo na Maendeleo ya vijana". Ameeleza Dkt. Tax


Naye Mhe. Mbae ameeleza kufurahishwa kwake na kufanyika kwa mkutano huo wa JPC na kuongeza kuwa mkutano huo ni kiungo muhimu katika kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano na kati ya Tanzania na Comoro.

Ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo na hivyo kuonesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kuendelea kushirikiana na Comoro.

Mbali na kusainiwa kwa Hati hizo Mawaziri hao wameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Jumla wa Ushirikinao mwaka 2009. 

Vilevile mkutano huo umejadili na kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kukuza biashara baina ya pande hizo mbili. Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine italenga kuwahimiza sekta binafsi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo na zile zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Eneo Huria la Biashara la SADC.

Akizungumzi kuhusu mkutano huo Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu ameeleza kuwa, Comoro ni mshirika muhimu wa Tanzania katika biashara, ambapo kwa mwaka 2023 Tanzania iliuza nchini humo bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 148. 

Ameongeza kusema kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo sio tu yataongeza ushirikiano wa kidiplomasia bali yanatarajiwa kuongeza kiasi cha bidhaa ambazo Tanzania inaingiza nchini humo. 

Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania umejumuisha wataalamu na watendaji kutoka sekta mbalimbali na umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ambaye pia aliongoza mkutano huo kwa kushirikiana na mwenyekiti mwenza Waziri Mbae wa Comoro. 
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa hutoba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa hutoba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 jijini Dar es Salaam
Washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro wakifurahia jambo

Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae wakitia saini Hati za Makubaliano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae akizungumza kwenye Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu Mussa akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro uliofanyika jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu na Mhe. Balozi Fatima Alfeine wa Comoro wakifuatilia zoezi la utiaji saini wa Hati za Makubaliano kwenye mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam

DKT. TAX AKUTANA NA KAIMU NAIBU WAZIRI WA MAREKANI

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), akisalimiana na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass alipokutana naye kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Michael Batle  alipomsindikiza Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaamm, kulia ni Katibu Mkuu Balozi Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Marekani Mhe. Michael Batle 
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), akizungumza na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


 Katibu Mkuu Balozi Samwel Shelukindo (kushoto) akiwa na watumishi wa wizara katika kikao kati ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb)  Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass alipofika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Balozi wa Marekani nchini Mhe. Michael Batle (kulia) akiwa na ujumbe wake  katika kikao kati ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb)  Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass alipofika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb)  akiwa na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass alipofika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb)  akiwa na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass  pamoja na Katibu Mkuu Balozi Samwel Shelukindo na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Michael Batle (kulia) alipofika  katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass katika picha ya pmoja baada ya kumaliza mazungumzo yao  katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam







Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb), amekutana kwa mazungumzo na Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Siasa wa Marekani Mhe. John Bass katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho Dkt. Tax amemuhakikishia Mhe. Bass kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Marekani katika masuala yenye manufaa kwa nchi hizi mbili na wananchi wake.

Amesema ziara ya Mhe. Bass nchini ni ushahidi wa  uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili huku ikonesha umuhimu mkubwa katika kuendelea kudumisha na kuimarisha maelewano, ushirikiano na urafiki kati ya Tanzania na Marekani na kuongeza kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na majadiliano ya wazi kwa ajili ya kujenga na kuweka misingi ya ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na Marekani.

“Nina Imani kuwa kupitia ushirikiano na uhusiano wetu sio kwamba tutakabiliana na changamoto zinazotukabili kwa pamoja bali pia tutanufaika na fursa zilizopo mbele yetu ili kuchochea ukuaji na ustawi wa pamoja, alisema Dkt. Tax.

Naye Mhe. Bass akizungumza katika kikao hicho amesema ziara yake nchini ina lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania na kuahidi kuwa Marekani inaiona Tanzania kama mdau wa kimkakati katika ushirikiano wa maendeleo.

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na Serikali ya Marekani na kuongeza kuwa ni matarajio yake kuwa kupitia majadiliano mbalimbali ambayo yemekuwa yakifanyika yatasaidia nchi yake kuibua kwa undani maeneo muhimu ambayo Serikali ya Tanzania inahitaji kuendelea ushirikiana na Marekani. 

Tanzania na Marekani zimekuwa zikishirikina katika nyanja za afya kupitia miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Shirika la Misaada la USAID, elimu, kilimo, biashara na uwekezaji, ulinzi na usalama.

Tuesday, July 23, 2024

MKUTANO WA 117 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PASIFIKI (OACPS) WAANZA JIJINI BRUSSELS

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa 117 ulioanza tarehe 23 Julai 2024, kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Bw. Msafiri Mbibo akifuatilia mkutano huo. 


Maafisa waandamizi wa Serikali wakifuatilia Mkutano huo 

Maafisa waandamizi wa Serikali wakifuatilia Mkutano huo 

Maafisa waandamizi wa Serikali wakifuatilia Mkutano huo 


Mkutano ukiendelea 

Mkutano ukiendelea  kutokea jijini Brussels


Mkutano ukiendelea  kutokea jijini Brussels



Mkutano wa 117 wa Baraza la Mawaziri la nchi za nchi za Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) Unachofanyika kwa mfumo wa mseto kuanzia tarehe 23 hadi 26 Julai 2024 umeanza jijini Brussels, Ubelgiji. 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede , anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa 117 ulioanza tarehe 23 Julai 2024. 

Mkutano huo pia unafuatiliwa kwa njia ya mtandao na Balozi wa Tanzania Brussels Mhe. Jestas Nyamanga na Maafisa waandamizi kutoka Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha, Viwanda na Biashara, Uvuvi, Mifugo, Madini, na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mkutano huo wa kwanza kwa mwaka huu unajadili maendeleo muhimu ya ushirikiano kati ya wanachama katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kuwa jukwaa la kuboresha mikakati ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi za OACPS. 

Mkutano huo pia utatoa fursa ya kuimarisha uhusiano na Umoja wa Ulaya kupitia majadiliano ya Mkataba wa Ushirikiano wa Samoa ambao unalenga kuboresha biashara uwekezaji na ushirikiano wa kisiasa kati ya nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya.

Mkutano huo unatarajiwa kujadili na kupitisha bajeti ya OACPS kwa mwaka 2024, kupitia na kujadili taarifa za fedha za OACPS ikiwemo taarifa ya uchaguzi wa hesabu za Jumuiya, kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Ubia  kati ya OACPS na Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba wa Samoa, kujadili taarifa ya ununuzi wa jengo jipya la Ofisi za OACPS na kujadili taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Madini na Nchi za OACPS uliofanyika Cameroun kuhusu uendelezaji wa madini ya kimkakati kwenye nchi wanachama.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili na kuamua kuhusu masuala mbalimbali ya jumuiya ni jukwaa muhimu kwa Mawaziri wa nchi hizo kubadilishana mawazo na kufanya maamuzi kuhusu matukio na maendeleo muhimu yaliyotokea katika kipindi cha kuanzia Juni 2023 hadi Juni 2024 ambako masuala na fursa muhimu zinazohitaji uelewa wa pamoja na mwelekeo wa kimkakati wa Mawaziri wa OACPS yalitokea.

Wajumbe wa sasa wa Baraza hilo la Mawaziri linaundwa na nchi za Jamaica- Rais, Liberia- Rais anayeondoka, Jamhuri ya Kongo, Rais ajaye, Sudan- Inawakilisha Afrika Mashariki, Angola Inawakilisha Kusini mwa Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-Inawakilisha Afrika ya Kati, Burkina Faso, Inawakilisha Afrika Magharibi,Haiti Inawakilisha nchi za Karibiani na Vanuatu Inawakilisha nchi za Pasifiki.

Monday, July 22, 2024

BALOZI SHELUKINDO AFUNGUA JPC YA KWANZA KATI YA TANZANIA NA COMORO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akifungua mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 22 – 24 Julai, 2024

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amefungua Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro katika Ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22-24 Julai 2024.

Akizungumza katika mkutano huo wa kihistoria, Balozi Shelukindo ameelezea kuridhishwa kwake na ukuaji wa mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ambao umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

“Mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka mitatu iliyopita kutoka Dola za Marekani milioni 6.75 mwaka 2021 hadi Dola milioni 54.67 mwaka 2023”. Alisema Balozi Shelukindo.

Balozi Shelukindo amesema ukuaji huo wa biashara ni mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa bado kuna haja kwa nchi hizo mbili kuongeza uwigo wa ushirikiano wa kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kwa tija ya pande zote mbili.

Amesema mikutano hiyo ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano inatoa fursa kwa nchi hizo mbili kupanua na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kupitia nyanja mbalimbali.

Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina nia ya dhati ya kupanua ushirikiano na Visiwa vya Comoro kupitia sekta mbalimbali, zikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, masuala ya kisheria, fedha, biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, miundombinu, TEHAMA, afya, elimu, michezo, sanaa na utamaduni.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Visiwa vya Comoro Mhe. Balozi Fatima Alfeine akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo ameeleza kuwa mkutano huo hautalenga kujadili namna ya kutatua changamo pekee bali kwa pamoja kuibua maneo mapya ya ushirikiano yatakayo chochea zaidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.

“Kutokana na uhimu wa mkutano huu wa kihistoria, ujumbe wetu umejumuisha wataalam kutoka sekta zote muhimu, kwa sababu tuna dhamira ya dhati sio tu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na undugu wa kihistoria uliopo kati yetu bali kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunaweka mazingira wezeshi na rafiki zaidi kwa wananchi wa pande zote mbili kunufaika zaidi kiuchumi kupitia fursa lukuki zilizopo”. Ameeleza Balozi Fatima Alfeine 

Mkutano huo wa siku tatu unashirikisha wadau kutoka Sekta za Diplomasia, Sheria, Ulinzi, Biashara, Kilimo, Biashara, Uwekezaji, Uchumi wa Buluu, ICT na Nishati


Kiongozi wa Ujumbe wa Visiwa vya Comoro Mhe. Balozi Fatima Alfeine akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam

Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam
Meza Kuu wakifuatilia Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ali Bujiku na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Sheria Dkt. Gift Kweka wakifuatilia mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi wa Tanzania Visiwa vya Comoro Mhe. Saidi Yakubu akichangia jambo kwenye mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu Mussa akichangia jambo kwenye mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Viziwa vya Comoro Nchini Tanzania Mhe. Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed akifuatilia mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro unaofanyika jijini Dar es Salaam 
Picha ya pamoja
Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro ukiendelea jijini Dar es Salaam. 

Friday, July 19, 2024

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO UINGEREZA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi ya Wizara  amekagua miradi ya maendeleo iliyopo jijini London, Uingereza kuanzia tarehe 14 hadi 18 Julai, 2024.


Katika ziara hiyo Kamati imekagua jengo la ofisi, makazi na kiwanja cha serikali. Vilevile, imefanya kikao cha mashauriano na ubalozi na wataalam wa ujenzi na uwekezaji nchini humo juu ya namna bora ya kuendeleza milki hizo za Serikali.


Katika ziara hiyo Kamati pia imekabidhi nyumba moja kwa mtumishi wa Ubalozi ambayo ukarabati wake umekamilika kwa asilimia 100 na hivyo kupunguza gharama za kulipia kodi ya pango kwa Serikali ambayo imekuwa ikilipwa kabla ya kukamilika kwake. 


Ziara hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango mahsusi wa Wizara wa kuendeleza viwanja na milki zake zilizopo nje ya nchi, ambao ulielezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) wakati alipowasilisha Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma mwezi Mei, 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa (wa pili kulia) akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki (wa kwanza kulia) katika ofisi za ubalozi huo jijini London, Uingereza wakati alipofanya ziara nchini humo kuanzia tarehe 14 hadi 18 Julai, 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akikabidhi nyumba ya makazi iliyokamilika ukarabati kwa mtumishi wa Ubalozi jijini London, Uingereza.

Balozi Said Shaib Mussa akiongoza kikao cha mashauriano kati ya Kamati ya miradi, watumishi wa ubalozi na wataalam wa ujenzi na uwekezaji kilichofanyika jijini London, Uingereza wakati wa ziara hiyo.

Ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiendelea.

Picha ya pamoja.

Kamati ikikagua miradi.

Wednesday, July 17, 2024

TANZANIA NA OMAN ZAJIPANGA KUKUZA BIASHARA


Ubalozi wa Tanzania nchini Oman umeandaa Kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika nchini Oman kuanzia tarehe 26 – 28 Septemba 2024.  

Hayo yameelezwa wakati wa kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf kilichofanyika Julai 15, 2024.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuanzisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Ghuba (GCC) na Jumuiya za kikanda ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Balozi Fatma alisisitiza pia umuhimu wa Oman kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, maarufu Sabasaba yanayofanyika kila mwaka mwezi Julai.

Kwa upande wake, Waziri Qais aliafiki mapendekezo ya Oman kushiriki maonesho ya sabasaba ambapo aliahidi kuwa atatembelea Tanzania na wafanyabiashara wakubwa ili kujionea fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini. 

Alitoa mwaliko kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuzuru Oman kwa lengo la kujionea maendeleo ya viwanda, hasa eneo la viwanda la Sohar na kujadili namna ya kuanzisha makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (MoU) baina ya pande mbili. Alipendekeza ziara hiyo kufanyika katikati ya mwezi wa Septemba au Oktoba 2024.

Viongozi hao walihimiza umuhimu wa usafiri wa moja kwa moja wa ndege ya mizigo kati ya Tanzania na Oman ili kurahisisha biashara. Kufuatia umuhimu huo, Balozi Fatma alieleza kuhusu kusainiwa kwa Mkataba mpya wa Ushirikiano wa Anga (BASA) baina ta Tanzania na Oman Julai 16, 2024 utakaoiwezesha Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kufanya safari zake nchini Oman.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa viongozi hao kuhimiza umuhimu wa kusaini Mkataba wa Kuepuka utozaji wa Kodi mara mbili ili kutimiza azma ya kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili. 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mhe. Qais bin Mohamed Al Yousuf wakikabidhiana zawadi baada ya mazungumzo yao.