Wednesday, August 14, 2024

WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA BADEA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amefanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA), Dkt. Sidi Ould Tah jijini Harare , Zimbabwe tarehe 13 Agosti, 2024. 

Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo viongozi hao, wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikitoa misaada ya kifedha, mikopo nafuu, na ufadhili kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo barani Afrika.

Aidha, Mhe. Balozi Kombo amemueleza Dkt. Tah kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wabia wa maendeleo kwa ustawi wa watu wake na Taifa kwa ujumla, hivyo ni matarajio yake kwamba mazungumzo hayo yatafungua maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Hivyo, katika kuendelea kuimarisha Diplomasia ya Uchumi, Wizara itaendelea kusimamia taratibu za makubaliano ambazo BADEA itaingia na sekta husika ili kuhakikisha nchi yetu inanufaika vyema na fursa za ujenzi wa miundombinu ya kidigitali na upatikanaji wa mawasiliano ya kimtandao (Internet). 

Naye Dkt. Tah ameeleza kuwa Benki hiyo ina nia ya kufadhili nchini Tanzania ujenzi wa Kituo cha kwanza cha kuhifadhi taarifa zinazohusu masuala ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence & Robotics) na kwamba kukamilika kwa taratibu za uanzishwaji wa mradi kutawezesha utekelezaji kuanza kwa wakati. Mazungumzo kuhusu suala hili yanaendelea. 

Viongozi wengine walioshiriki mazungungumzo hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. IGP (RTD) Simon Sirro.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Rais wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA), Dkt. Sidi Ould Tah walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa SADC unaoendelea jijini Harare , Zimbabwe tarehe 13 Agosti, 2024.
Mazungumzo yakiendelea
Mazungumzo yakiendelea
Picha ya pamoja
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisisitiza alipokuwa kwenye mazungumzo na Rais wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA), Dkt. Sidi Ould Tah jijini Harare, Zimbabwe tarehe 13 Agosti, 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. IGP (RTD) Simon Sirro (kulia) wakifuatilia
Rais wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA), Dkt. Sidi Ould Tah akiwa kwenye mazungumzo na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo yaliyofanyika jijini Harare, Zimbabwe

Tuesday, August 13, 2024

NAIBU WAZIRI LONDO AMTEMBELEA KATIBU MKUU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Masharki (EAC) Mhe. Monica Nduva alipomtembelea Ofisini kwake jijini Arusha.

 

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb) akisaini kitabu cha wageni Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Masharki (EAC) Mhe. Monica Nduva alipomtembelea  jijini Arusha .
 

 

mazungumzo yakiendelea

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb) katika picha na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Masharki (EAC) Mhe. Monica Nduva alipomtembelea Ofisini kwake jijini Arusha.
 
 NAIBU WAZIRI LONDO AMTEMBELEA KATIBU MKUU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb) ametembelea Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Masharki (EAC) Mhe. Monica Nduva Ofisini kwake tarehe 13 Agosti 2024 jijini Arusha. 

Katika mazungumzo yao, Mhe. Londo alimuhakikishia Mhe. Nduva ushirikiano na kumuelezea kuwa Tanzania itashiriki katika masuala yote yanayohusu Jumuiya ya EAC kwa uzito unaostahili. 

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujitambulisha na kufahamiana baada ya Mhe. Londo kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mwezi Julai 2024. 

Mhe. Londo aliongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi.

DKT. MPANGO AFUNGUA MKUTANO WA KWANZA WA ELIMU WA EAC NA MAADHIMISHO YA MWAKA WA ELIMU WA UMOJA WA AFRIKA

 

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Naibu Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika jijini Arusha.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na wageni mbalimbali katika meza kuu  katika Ukumbi wa AICC wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika jijini Arusha.


Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Wageni na washiriki mbalimbali kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia ufunguzi wa  mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.

 Naibu Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo wa kwanza kushoto akiwa na mawaziri wengine kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia ufunguzi wa  mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi wa pili kushoto aliimba wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika  jijini Arusha katika ukumbi wa AICC.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo alipowasili katika Ukumbi wa AICC kufungua mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika  jijini Arusha.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi alipowasili katika Ukumbi wa AICC kufungua mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika jijini Arusha.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amefungua mkutano wa kwanza wa elimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maadhimisho ya Mwaka wa elimu wa Umoja wa Afrika.

Akifungua mkutano huo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha Mhe. Dkt. Mpango amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwekeza zaidi katika elimu na afya ili kuweza kunufaika na idadi kubwa ya watu iliyopo hususani vijana ambao watakuwa wameelimika na kuwa na afya bora na hivyo kujiletea maendeleo.
 
Mhe. Dkt. Mpango amesema ongezeko la watu katika mataifa ya Afrika Mashariki linatoa ishara ya ulazima wa kuongeza uwekezaji wa rasilimali zaidi za kifedha, kiafya na kielimu ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa elimu bora na afya bora kwa watu wake.
 
“Mwenendo wa idadi ya watu Afrika Mashariki unaweza kuwa baraka kubwa kama ukitumiwa vizuri kwani kuendelea kuwa na vijana wengi wenye ujuzi na umahiri wa kujenga uchumi  imara hali ambayo itafikiwa ikiwa rasilimali watu hiyo itatumika kikamilifu”, alisisitiza Dkt. Mpango.
 
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuhakikisha mabadiliko ya dhati ya elimu yanafikiwa na hivyo kutoa matokeo chanya kwa vijana wengi ndani ya Jumuiya.

Amesema takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Bara la Afrika limekua likipata matokeo yenye faida katika elimu ukilinganisha na mabara mengine na kuongeza kuwa   ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara bado unakabiliwa ufadhili mdogo zaidi uliowekezwa katika sekta ya elimu ambao ukipatikana kwa kiwango kinachostahili utaleta tija na manufaa makubwa kwa nchi hizo.

Ametoa wito kwa hatua zaidi kuchukuliwa na juhudi zaidi kutumika ili kutambua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu barani Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na uwekezaji mdogo unaofanywa katika sekta hiyo na kusababisha utoaji wa elimu bora yenye ujuzi unaohitajika kuawa mgumu na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto tatu zinazoikabili dunia kwa sasa ambazo ni ongezeko la idadi ya watu, utandawazi na  maendeleo ya teknolojia.
 
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo ameeleza kuwa imefanya elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi miaka kumi ifikapo mwaka 2027/2028. Aidha amesema Serikali imefanya mabadiliko ya mtaala wa elimu nchini ambayo yanalenga kuongeza ubora wa elimu pamoja na kuandaa rasilimali watu itakayoendana na mahitaji ya dunia kwa sasa ya aendeleo ya dijitali, teknolojia pamoja na kutumia vema fursa mbalimbali zilizopo.
 
Ametaja pia hatua za uboreshaji wa miundombinu ya elimu kama vile kujenga madarasa ya kufundishia, nyumba za walimu, kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha na nyenzo za kufundishia kama vile kompyuta na vitabu ili kutimiza lengo la kuongeza ubora wa elimu, kuongeza upatikanaji wake na kuhakikisha elimu inayotolewa inatosheleza mahitaji ya ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya teknolojia.
 
Makamu wa Rais amewashukuru washirika wa Kimataifa wanaoiunga mkono Tanzania katika mageuzi ya sekta ya elimu na kuukaribisha mpango mpya wa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (PEERS) ambao utasaidia uratibu wa mifumo ya elimu katika kanda.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo amesema Elimu ni jiwe la msingi ambalo tunajengea sio tu maendeleo ya kitaaluma na kijamii na kwa mtu mtu binafsi bali pia ni uwezeshaji wa kiuchumi ambao husaidia kupunguza umaskini na kuleta maendeleo kwa jamii.

Ameongeza kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimepiga hatua kubwa hususan katika viwango vya usajili wa Watoto shuleni hali ambayo imetokana na juhudi za serikali kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kimataifa ya Elimu kwa Wote kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 26 cha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.

WAZIRI WA MAMLAKA YA FORODHA WA CHINA AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KIKAZI.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi. Said Shaibu Mussa akimpokea Waziri wa Mamlaka ya Forodha ya China, Mhe. Yu Jianhua mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

============

Waziri wa Mamlaka ya Forodha ya China, Mhe. Yu Jianhua amewasili nchini leo Agosti 13, 2024 kwa ziara ya kikazi ya Siku tatu.

Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipokelewa na Naibu Katibu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa.

Ziara ya Waziri Yu Jianhua inalenga kukamilisha makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini China mwezi Novemba 2022.

Mhe. Waziri Yu Jianhua ndiye anahusika na kutoa vibali vya kufungua masoko ya bidhaa mbalimbali kuingia nchini China.

Akiwa nchini Tanzania, Mhe. Yu Jianhua atakutana na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii; Wizara ya Kilimo; Wizara ya Uvuvi na Mifugo; Kamishna wa TRA; na atatembelea Bandari ya Dar es Salaam.

Ujumbe wa Waziri huyo pia utatembelea Stesheni ya TAZARA ikiwa ni sehemu muhimu ya uhusiano kati ya Tanzania na China.

Itakumbukwa kwamba tayari Wizara imewezesha kupatikana soko la mihogo, soya, ufuta, kahawa, mbegu za pamba, karafuu kutoka Tanzania kuuzwa nchini China.

WAZIRI KOMBO ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUTEKELEZA MIKAKATI YA KIKANDA – SADC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameahidi kushirikiana na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukuza uchumi wa kanda.

Hayo yamejiri wakati akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC unaofanyika nchini Zimbabwe kuanzia tarehe 13 hadi 16 Agosti, 2024 ambapo, Mhe. Kombo anashiriki mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

‘’Naahidi kushirikiana nanyi katika kutekeleza mikakati ya kikanda kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030’’ alisema Waziri Kombo.

Aidha, Waziri Kombo ameeleza kwamba Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ikiwa ni pamoja na ulipaji wa michango yake ili kuyafikia malengo ya kanda hiyo.

Mkutano wa Mawaziri wa SADC pia umefanya makabidhiano ya nafasi ya mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. Balozi Tete António amekabidhi nafasi hiyo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Balozi Dkt. Fredrick Shava.

Wakati wa makabidhiano hayo Mhe, Tete António amempongeza Mhe. Shava kwa kupokea majukumu hayo na pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Zimbabwe, ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake Mhe. Shava ameshukuru kwa kuaminiwa kukabidhiwa jukumu hilo na ameeleza kuwa Zimbabwe ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama kufikia malengo na vipaumbele vya jumuiya hiyo. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuhimiza ulipaji wa michango ili kuiwezesha jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

WAZIRI KOMBO ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUTEKELEZA MIKAKATI YA KIKANDA – SADC

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameahidi kushirikiana na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kukuza uchumi wa kanda.

 

Hayo yamejiri wakati akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC unaofanyika nchini Zimbabwe kuanzia tarehe 13 hadi 16 Agosti, 2024 ambapo, Mhe. Kombo anashiriki mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

 

‘’Naahidi kushirikiana nanyi katika kutekeleza mikakati ya kikanda kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030’’ alisema Waziri Kombo.

 

Aidha, Waziri Kombo ameeleza kwamba Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ikiwa ni pamoja na ulipaji wa michango yake ili kuyafikia malengo ya kanda hiyo.

 

Mkutano wa Mawaziri wa SADC pia umefanya makabidhiano ya nafasi ya mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. Balozi Tete António amekabidhi nafasi hiyo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Balozi Dkt. Fredrick Shava.

 

Wakati wa makabidhiano hayo Mhe, Tete António amempongeza Mhe. Shava kwa kupokea majukumu hayo na pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Zimbabwe, ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo.

 

Kwa upande wake Mhe. Shava ameshukuru kwa kuaminiwa kukabidhiwa jukumu hilo na ameeleza kuwa Zimbabwe ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama kufikia malengo na vipaumbele vya jumuiya hiyo. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuhimiza ulipaji wa michango ili kuiwezesha jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

=====================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 16 Harare, Zimbabwe.

   Kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifatilia Mkutano wa Mawaziri wa SADC unaoendeleo Harare, Zimbabwe.


Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah wakifuatilia mkutano huo

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akijadili jambo na Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Mratibu wa Masuala ya SADC Kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri (kulia)


Meza kuu ikiongoza mkutano

Picha ya pamoja.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC aliyemaliza muda wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. Balozi Tete António akikabidhi mamlaka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Balozi Dkt. Fredrick Shava.

Monday, August 12, 2024

WAZIRI KOMBO KUSHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA SADC, HARARE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili Harare, Zimbabwe kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 13 na 14 Agosti, 2024


Mkutano huo wa Mawaziri  ni sehemu ya mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 nchini Zimbabwe.


Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC kilichofanyika tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024 nchini humo ambacho kilijadili na kufanya maandalizi ya nyaraka mbalimbali zitakazo pokelewa na kujadiliwa na mkutano huo wa Mawaziri. 


Baada ya kuwasili nchini Zimbabwe, Mhe. Kombo amepokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Balozi IGP (RTD) Simon Sirro na kufanya kikao na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika mikutano ya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.


Mawaziri wengine watakaoshiriki mkutano huo ni pamoja na; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW).

===============================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe ambapo alifanya kikao cha ndani cha maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa SADC kitakachofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 16 Agosti, 2024

Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Balozi IGP (RTD) Simon Sirro wakifuatilia kikao hicho.

Kutoka kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mratibu wa Masuala ya SADC Kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri wakifuatilia kikao.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW)  akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe tarehe 12 Agosti, 2024.


Kikao kikiendelea


Saturday, August 10, 2024

TANZANIA YASISITIZA ULIPAJI MICHANGO SADC


Tanzania imeahidi kukamilisha mchango wake wa mwaka katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzisisitiza nchi nyingine wanachama kufanya hivyo ili kuiwezesha Jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 

Hayo yamejiri wakati wa Kikao cha Kamati ya Fedha cha Jumuiya ya SADC kilichofanyika tarehe 10 Agosti 2024, Harare, Zimbabwe. 

Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba ambaye ameambatana na Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya SADC kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina. 

Akichangia katika mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba amesema kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa majukumu yanayotekelezwa na Jumuiya kwa ustawi wa kanda hivyo, itaendelea kuwa mwanachama hai na kukamilisha michango yake mapema ili kuwezesha Jumuiya ya SADC kutekeleza vyema shughuli zake, ambazo Tanzania ni mnufaika. 

‘’Tanzania inaahidi kukamilisha michango yake ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jumuiya zenye maslahi kwa nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, hivyo napenda kusisitiza kwamba nchi yetu itatimiza ahadi hiyo siku chache zijazo’’ alisema Dkt. Mwamba. 

Aidha, mapendekezo ya kikao hicho yatawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri la SADC kwa ajili ya kufanyiwa kazi katika mkutano wake utakaofanyika tarehe 13-14 Agosti, 2024. 

Pamoja na masuala mengine kikao hicho kimejadili masuala yafuatayo:- Hali ya Michango kwa Nchi Wanachama; Hali ya Michango kwa Washirika wa Maendeleo; Taarifa ya utekelezaji wa Taarifa ya Fedha kwa mwaka 2023/24 na Utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Kikanda. 

Masuala mengine yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho yanahusiana na Bajeti ya Nyongeza na Uhamisho wa Vifungu vya Bajeti, Taarifa za athari za kibajeti za rasilimaliwatu; Mpango wa Kati wa Mapato na Matumizi wa mwaka 2023/24-2026/27 na Taarifa ya Kamati ya Ukaguzi ya SADC.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kamati ya Fedha ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika tarehe 10 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.


Kulia ni Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya SADC kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha, Bw. James Msina wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
Sehemu ya ujumbe wa kikao cha Kamati ya Fedha ya SADC ukifuatilia mkutano.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa kikao cha Kamati ya Fedha ya SADC ukifuatilia mkutano

Friday, August 9, 2024

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA OACPS

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, akichangia mjadala kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean, na Pacific (OACPS) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 9 Agosti 2024

Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean, na Pacific (OACPS) umefanyika leo tarehe 9 Agosti 2024, kwa njia ya mtandao, ukiwashirikisha mawaziri kutoka nchi 79 wanachama wa Jumuiya hiyo.

Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).

Mkutano huo, ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. TÉTE António, uliangazia masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Jumuiya, ikiwa ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita, maendeleo ya programu na miradi mbalimbali, hali ya kifedha ya Jumuiya, na maandalizi ya mkutano ujao wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa OACPS.

Katika hotuba ya ufunguzi, Mhe. António alisisitiza umuhimu wa mkutano huo katika kutatua changamoto mbalimbali, hususan za kifedha na kiutendaji, ili kuimarisha ufanisi wa Jumuiya.

Balozi Mbundi, akichangia katika mjadala, alisisitiza umuhimu wa matumizi bora ya rasilimali fedha na kuhimiza Sekretariati ya OACPS kuzingatia miongozo ya matumizi sahihi ya fedha ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa bajeti. Pia aliungana na wajumbe wengine kuhimiza nchi wanachama kumalizia michango yao kwa Sekretariati na kupunguza matumizi yasiyo ya maendeleo kama njia ya kukabiliana na upungufu wa fedha.

Balozi Mbundi alieleza kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha imani ya nchi wanachama na wadau wa maendeleo ambao wanachangia kwenye bajeti ya miradi na programu mbalimbali za Jumuiya hiyo.

Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ulijumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Makamu wa Rais, ukiongozwa na Balozi Stephen Mbundi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America (DEA) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia Mkutano wa OACPS uliokuwa ukiendelea kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. TÉTE António akiongoza Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 9 Agosti 2024
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, muda mfupi kabla ya kuanza kwa OACPS uliofanyika kwa njia ya mtandao