Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amefanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi Afrika (BADEA), Dkt. Sidi Ould Tah jijini Harare , Zimbabwe tarehe 13 Agosti, 2024.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo viongozi hao, wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikitoa misaada ya kifedha, mikopo nafuu, na ufadhili kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo barani Afrika.
Aidha, Mhe. Balozi Kombo amemueleza Dkt. Tah kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wabia wa maendeleo kwa ustawi wa watu wake na Taifa kwa ujumla, hivyo ni matarajio yake kwamba mazungumzo hayo yatafungua maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.
Hivyo, katika kuendelea kuimarisha Diplomasia ya Uchumi, Wizara itaendelea kusimamia taratibu za makubaliano ambazo BADEA itaingia na sekta husika ili kuhakikisha nchi yetu inanufaika vyema na fursa za ujenzi wa miundombinu ya kidigitali na upatikanaji wa mawasiliano ya kimtandao (Internet).
Naye Dkt. Tah ameeleza kuwa Benki hiyo ina nia ya kufadhili nchini Tanzania ujenzi wa Kituo cha kwanza cha kuhifadhi taarifa zinazohusu masuala ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence & Robotics) na kwamba kukamilika kwa taratibu za uanzishwaji wa mradi kutawezesha utekelezaji kuanza kwa wakati. Mazungumzo kuhusu suala hili yanaendelea.
Viongozi wengine walioshiriki mazungungumzo hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. IGP (RTD) Simon Sirro.
Mazungumzo yakiendelea |
Mazungumzo yakiendelea |
Picha ya pamoja |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. IGP (RTD) Simon Sirro (kulia) wakifuatilia |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.