Tanzania imesisitiza kuendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa lilanoshughulikia Wahamiaji (IOM) kuwawezesha vijana kiuchumi ili kutengeneza ajira zitakazojenga ustawi wao na kuleta maendeleo kwa taifa.
Msisitizo huo umetolewa leo tarehe 15 Agosti, 2024 wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alipokutana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER jijini Harare, Zimbabwe.
Aidha, katika mazungungumzo hayo Waziri Kombo ameeleza changamoto ya uhamiaji huwaathiri zaidi vijana wanaotoka katika mataifa yanayoendelea hususan mataifa ya Afrika ambapo wamekuwa wakihama kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yao na familia zao.
"Binafsi ningependa tatizo la uhamiaji lipate suluhisho kwa kufanyia kazi chanzo cha tatizo badala ya kufanyia kazi matokeo au matatizo yanayotokea baada ya watu kuhama na kupata changamoto wakiwa katika harakati za kuvuka mipaka" alisema Waziri Kombo.
Pia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto hiyo imetafuta suluhisho la ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia mradi wa kilimo ujulikanao kama “Building Better Tomorrow (BBT)’’ ambao, utawawezesha vijana kujiajiri na kuwaajiri wengine, pamoja na kufanya kilimo biashara kwa lengo la kukuza kipato.
Kwa upande wa Bw. ABDIKER ameipongeza Tanzania kwa kuwahudumia wahamiaji ambao sehemu kubwa ni wakimbizi na wale wanaopita kutoka Pembe ya Afrika kuelekea kusini mwa Afrika kutafuta maisha bora na kwamba IOM inaendelea kutoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Pia amepongeza kwa uwepo wa chuo cha uhamiaji nchini ambacho kimekuwa kikitoa elimu ya uhamiaji kwa watanzania na kwa mataifa mengine na pia amesema kuwa IOM ina mpango wa kuanzisha chuo kikubwa cha uhamiaji kitakachochukua wanafunzi ulimwenguni kote, hivyo uwepo wa chuo hicho utaongeza ushirikiano na kujenga uwezo wa kitaaluma katika masuala ya uhamiaji.
Vilevile, viongozi hao wamejadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wahamiaji ikiwemo, mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha ajali kwenye safari za majini na kupelekea watu kupoteza maisha wakati wa kuhama sambamba na ajira zisizo na staha wanazozipata baada ya kufika uhamishoni pasipo kupata taratibu rasmi za kuhama.
Hivyo, IOM ina matumaini ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania hasa wakati huu ambapo inaenda kukabidhiwa nafasi ya Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security).
================================
Habari katika picha za mazungumzo ya Mhe. Waziri Kombo na Bw. Mohammed ABDIKER
Mazungumzo yakiendelea. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.