Thursday, August 15, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AFUNGUA KONGAMANO LA KISWAHILI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amefungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo. 

Kongamano hilo linaloongozwa na mada kuu isemayo "Lugha ya Kiswahili kwa Maendeleo Barani Afrika" linajumuisha Wataalam, Watafiti na wadau wa Kiswahili kutoka Nchi za Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali duniani. 

Akifungua Kongamano hilo Waziri Chumi ameeleza kuwa kiswahili kimekuwa miongoni mwa lugha inayotuunganisha Waafrika hususan waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, na hasa kutokana na mchango wake wakati wa harakati za kupigania uhuru. 

Akizungumzia nafasi ya Wizara katika kueneza lugha ya Kiswahili ulimwenguni Mhe. Chumi ameeleza Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje Nchi ilitoa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika kutambuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). 

Vilevile ameongeza kusema kuwa licha ya mchango huo, Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kukipa kipaumbele cha kipekee Kiswahili kupitia Sera Mpya ya Mambo ya Nje inayofanyiwa mapitio, hatua ambayo itachangia kubidhaisha lugha hiyo adhimu duniani hivyo kuongeza matumizi ya Kiswahili nje ya mipaka yetu. 

"Kwa sasa Wizara yetu ipo kwenye hatua za mwisho za mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Taifa letu. Kutokana na tathmini tuliyoifanya kwenye mapitio hayo, tumekubaliana kuongeza mawanda ya Diplomasia ya Uchumi kwa kujumuisha maeneo ambayo siyo ya jadi (traditional) ikiwemo masuala ya kubidhaisha Kiswahili" Alieleza Mhe. Chumi.

Aliongeza kusema kuwa Wizara kwa siku za usoni inatarajia kuongeza wigo wa upatikanaji wa fursa kwa waalimu wa Kiswahili na wakalimani sehemu mbalimbali duniani pamoja na uuzaji wa vitabu vya kiswahili.

Kwa upande wake, mratibu wa kongamano hilo Dkt. Zainabu Idd ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuenzi na kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi. 

Aidha, Dkt. Zainabu pamoja na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kutoa msukumo wa matumizi ya Kiswahili katika majukwaa na matukio mbalimbali ya kimataifa ikiwemo katika matamasha makubwa ya michezo kama vile AFCON, ili kukiongezea thamani na kuwavutia watu wengi zaidi duniani kutumia lugha hiyo adhimu.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikisha kuongeza wigo wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili hususan katika Jumuiya za Kikanda ambapo tayari Jumuiya za SADC, EAC na AU zinatumia lugha hiyo katika kuendesha vikao mbalimbali. 

Vilevile Wizara inaendelea na mikakati ya kukuza na kubidhaisha Kiswahili ikiwemo kufungua madarasa ya kufundishia Kiswahili katika Balozi za Tanzania zilizopo sehemu mbalimbali duniani. 

CHAKAMA ni chama kinachoundwa na wahadhiri wanaofundisha Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki kikilenga kuunganisha wadau wa Kiswahili Kikanda na Kimataifa kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo utafiti na kufanya mijadala fikirishi kuhusu lugha ya Kiswahili
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akitia saini kwenye kitabu cha wageni muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akisalimiana na Prof. Albino John Tenge Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, alipowasili katika Chuo Kikuu cha Dodoma kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akikabidhiwa cheti cha kutambua mchango wa Wizara katika kufanikisha kufanyika kwa Kongamano hilo na kukuza lugha Kiswahili.
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akifuatilia  hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodom
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea
Mkuu wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii Prof. Albino John Tenge akizungumza kwenye ufunguzi Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa CHAKAMA linalofanyika jijini Dodoma
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki likiendelea

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.