Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) leo tarehe 17 Agosti, 2024 umekabidhi
jukumu la Unyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Organ on Politics, Defence and Security)
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Asasi hiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama
katika kanda ya SADC na ina mamlaka ya kuongoza na kutoa ushauri kwa nchi
wanachama katika masuala yanayohatarisha amani, usalama na utulivu katika kanda
hiyo. Majukumu hayo huratibiwa katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Asasi hiyo.
Nafasi za uongozi kwa
upande wa SADC Organ hufuata mzunguko kama ilivyo katika
nafasi ya uongozi wa SADC lakini sio nchi zote zinaweza kuwa Mwenyekiti
isipokuwa kwa kigezo cha uwepo wa hali ya ulinzi na usalama katika nchi
mwanachama. Tanzania imeshawahi kuwa Mwenyekiti mara tatu katika vipindi
tofauti: 2006/2007, 2012/2013 na 2016/2017 na sasa itaongoza kwa kipindi cha
2024/2025 ambapo itakuwa mwenyeji wa vikao vya Asasi hiyo kwa kipindi husika.
Kufuatia utaratibu
huo, Troika
ya SADC kwa mwaka 2024/2025 inaundwa na Zambia (Mwenyekiti aliyemaliza muda)
Tanzania (Mwenyekiti wa sasa) na Malawi (Makamu Mwenyekiti).
Jukumu
kubwa linalomkabili Mhe. Rais Samia katika asasi hiyo ni pamoja na kusimamia
amani Mashariki mwa DRC hivyo, ataendeleza jitihada zake pale ambapo uongozi
uliopita uliishia.
Mkutano huo pia,
umemthibitisha Mwenyekiti wa SADC ambapo, Mhe. Emerson Bambudzo Mnangagwa Rais
wa Jamhuri ya Zimbabwe amepokea jukumu hilo na nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa
SADC imeenda kwa Mhe. Andry Rajoelina Rais wa Jamhuri ya Madagascar ambapo nchi
hizo zitaongoza katika kipindi cha 2024/2025.
Akihutubia mkutano huo
Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Mnangangwa amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea
jukumu la uenyekiti wa SADC na amemuhakikishia ushirikiano katika kufanikisha
majukumu hayo waliyokabidhiwa kwa ustawi wa kanda na wananchi wake.
Pia, ameeleza kuwa
jumuiya hiyo inaendelea kufungua fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo
endelevu ya kikanda kupitia agenda yake ya kipaumbele ya maendeleo ya viwanda.
Jitihada hizo zitakuza ubunifu na kuongeza thamani ya bidhaa katika masoko ya
kikanda na kimataifa.
Kuhusu shughuli nyingine
zilizofanyika sambamba na mkutano huo Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa kulikuwa na
Kongamano la Uwekezaji lililoandaliwa na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya
Kiuchumi Afrika (BADEA) na Wiki ya Viwanda ambazo zilitumika kuonesha bidhaa na
huduma mbalimbali kutoka nchi wanachama pamoja na kutoa fursa kwa
wafanyabishara kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa biashara.
Shughuli nyingine
iliyofanyika ni pamoja na mhadhara wa umma ambao unasaidia katika kujenga
uelewa wa masuala ya msingi ambayo husaidia katika ubunifu na kuendelea
kuimarisha hatua za mtangamano. Hivyo ni muhimu kwa vyuo vikuu na vyuo vingine
vinavyofanana navyo kutafakari namna bora ya kuwekeza katika ubunifu ili
kuwezesha mikakati ya kikanda kupata matokeo ya kimaendeleo kwa mafanikio.
Pamoja na hayo
amesisitiza umuhimu wa kukuza sekta ya nishati, kilimo, biashara, uwekezaji na
usafirishaji na kuhimiza umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto
zake na kuiwezesha jumuiya hiyo kuinuka kiuchumi.
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali pia umemalizika kwa nchi wanachana kusainiwa Itifaki na matamko mbalimbali ya kikanda, kwa upande wa Tanzania imesaini Itifaki ya Ajira na Kazi, Tamko la
Kuwalinda Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi na Tamko la Kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi
kama Janga la Kiafya kwa Jamii ya Ukanda wa SADC ifikapo 2030.
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mkutano wao Kawaida wa 44 uliofanyika tarehe 17 Agosti, 2024Harare, Zimbabwe. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.