Friday, August 9, 2024

WAZIRI KOMBO AJITAMBULISHA KWA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiwa katika picha na Viongozi na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), pamoja na Manaibu Waziri Mhe. Cosato Chumi (Mb.) na Mhe. Denis Lazaro Londo (Mb.); wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman kwalengo la kujitambulisha kufuatia mabadiliko madogo ya hivi karibuni ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akitoa salamu zake kwenye mkutano huo uliofanyika tarehe 9 Agosti, 2024 Mheshimiwa Othman amesema ni vyema kwa Taifa kutumia fursa zilizopo katika Mtangamano wa Afrika Mashariki, ili kujiimarisha kiuchumi, kwani Afrika Mashariki ni zaidi ya jumuiya; ni ni shirikisho la kufungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vyema, zitaleta tija kwa Taifa.

Aidha amewaelekeza viongozi hao ambao wamepewa dhamana ya kuisimamia Wizara hii ya muungano, kuzitumia fursa zilizopo katika Taasisi za Kimataifa ili kuendana na kasi ya maendeleo ulimwenguni.

"Zipo taasisi kama WIPO, zinazobeba fursa nyingi ndani yake, ambazo mataifa ya Asia na Ulaya wanazitumia vilivyo kujinufaisha, ila kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla bado tupo nyuma sana; tukizingatia hili ni jambo adhimu kwa mustakbali wa maendeleo ya Nchi yetu".

Aidha Mheshimiwa Othman amewahimiza watendaji hao kutoa elimu, kwa jamii za wazawa na hata wageni, juu ya mambo ya msingi yanayoihusu Serikali ya Muungano, na yepi ya Zanzibar, ili kuondoa mkanganyiko sambamba na kuwajengea uelewa mpana wananchi kuhusu haki zao na pia maeneo sahihi ya kupata huduma kwa wakati.

Akielezea kuhusu suala la tija kupitia sekta za utalii, hususan kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Mhe. Othman amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa kumbi za mikutano zenye hadhi ya kimatifa, ili kurahisisha harakati za kuvutia mataifa ya kigeni kuja kutalii Tanzania na hatimaye kunufaisha taifa kupitia mapato ya utalii. Hivyo, Mheshimiwa Othman ameridhishwa na hatua ya ujumbe huo kujitambulisha na kubadilishana mawazo, huku akiahidi mashirikiano mema, kwa maslahi mapana ya Taifa.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi za Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Migombani, Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja, Mhe. Balozi Kombo, kwa niaba ya Wizara ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na viongozi wakuu wote, pamoja na waliopo Zanzibar; ili kuleta ufanisi, na kufikia malengo, kwa ajili ya kuitangaza zaidi nchi katika jamii ya kimataifa.

Aidha, Mhe. Balozi Mahmoud, ambaye ameteuliwa kwenye wadhifa huo hivi karibuni akitokea Italia, kama Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ameahidi kuitendea kazi miongozo na mashauri yote aliyopewa, kwa maslahi makubwa ya Tanzania.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ndg. Ilyasa Juma Pakacha na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Chiku Kiguhe.
 Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Chiku Kiguhe akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman                          `
Kutoka kulia; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) pamoja na Manaibu Waziri Mhe. Cosato Chumi (Mb.) na Mhe. Denis Lazaro Londo (Mb.)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb.), akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akisisitiza jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipokwenda Ofisini kwake kujitambulisha
Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Yusuf Mndolwa akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman
Naibu Katinu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa akijitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.