Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasili jijini Bali,Indonesia leo tarehe 31 Agosti 2024 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Pili la Indonesia na Afrika unaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.
Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Mariam Mwinyi pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali alipokelewa na Naibu Waziri wa Biashara wa Indonesia Mhe, Jerry Sambuaga.
Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika ambao utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Bandung Spirit for Africa's Agenda 2063,” unalenga kuangazia kanuni za pamoja ambazo zimeweka msingi imara wa kuwa na uhusiano jumuishi, usawa na endelevu kati ya Indonesia na Afrika.
Maeneo muhimu ya ushirikiano yanayotarajiwa kujadiliwa katika Jukwaa hilo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, nishati, uchumi wa buluu, madini, afya na ushirikiano wa maendeleo.
Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mhe. Rais Mwinyi atafanya ziara ya kikazi nchini Indonesia kuanzia tarehe 04 hadi 06 Septemba 2024.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.