Sunday, September 1, 2024

RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA INDONESIA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia na sehemu nyingine duniani kuja kuwekeza nchini katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hususan kwenye maeneo ya Utalii, Bandari, Uvuvi na Kilimo cha Baharini, Uchukuzi na uchimbaji wa Mafuta na Gesi.

 

Mhe. Rais Mwinyi ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali, Indonesia leo tarehe 1 Septemba, 2024.

 

Mhe. Rais Mwinyi ambaye yupo nchini hapa kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa la Pili la Ushirikiano wa Indonesia na Afrika amesema, Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kwenye sekta ya uchumi wa buluu duniani na kwamba Tanzania imejipanga kunufaika kupitia sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wawekezaji kutoka Indonesia na kwingine duniani.

 

 “Tunaamini kwamba uzoefu uliowawezesha Indonesia kupiga hatua kubwa kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu utatuwezesha na sisi kujifunza na kufanikiwa. Hivyo tumekuja kuwaonesha na kujifunza  kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua kwenye maeneo niliyozungumzia ikiwemo Uvuvi, kilimo cha mwani, uchukuzi, utalii na uchimbaji wa mafuta na gesi” amesema Mhe. Rais Mwinyi.

 

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury amesema Sera ya Mambo ya Nje ya Indonesia na ile ya Tanzania zinafanana kwa kiasi kikubwa ambapo zote zinasisitiza katika kuchochea maendeleo kupitia diplomasia ya uchumi. Hivyo, Kongamano hilo ni njia mojawapo ya kutekeleza sera hizo katika kuhamasisha uwekezaji na biashara ili kuinua uchumi wa nchi hizi mbili.

 

Pia alimshukuru Mhe. Rais Mwinyi na ujumbe wake kwa kushiriki Kongamano hilo ambalo linalenga kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Indonesia katika sekta ya uchumi wa buluu kwa manufaa ya pande mbili.

 

Wakati wa Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), mada mbalimbali kuhusu uwekezaji ziliwasilishwa na Taasisi za Tanzania ikiwemo ZIPA na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 

Ujumbe wa Mhe. Rais Mwinyi ulioshiriki Jukwaa hilo unamjumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Amina Khamis Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Indonesia.

 

Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika utafanyika jijini Bali, kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia lililofanyika jijini Bali tarehe 1 Septemba 2024 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika litakalofanyika nchini hapa kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2024. Mhe. Rais Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Jukwaa hilo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Mhe. Pahala Mansury akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (kulia) akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi naye akishiriki Kongamano hilo. 
Mhe. Rais Dkt. Mwinyi akiwa ameongozana na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele mara baada ya kuwasili kwa ajilio ya kushiriki Kongamano la  Biashara kati ya Zanzibara na Indonesia lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji akishiriki Kongamano la Biashara kati ya Zanzibar na Indonesia
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bw. John Kambona akiwa na Afisa Dawati kutoka Idara hiyo, Bw. Suleiman Magoma wakishiriki Kongamano la Biashara
Sehemu ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Indonesia wakishiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Zanzibar na Indonesia
Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Indonesia, Bw. Suleiman Saleh akishiriki Kongamano hilo
Picha ya pamoja
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.