Wednesday, September 18, 2024

Balozi Shelukindo aongoza Kikao na Sekretarieti ya SADC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameiongoza timu ya Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-ORGAN)  katika siku ya pili ya kikao na Sekretarieti ya SADC.

Kikao hicho kilichoratibiwa na Bw. Terry Rose, Afisa Mkuu Kamati ya Siasa na Diplomasia ya SADC kimejikita katika kujadili masuala mbalimbali yahusuyo muundo wa kamati hiyo na majukumu yake ndani ya kanda ikiwemo uangalizi wa uchaguzi kwa nchi zinazotarajia kufanya uchaguzi. Nchi hizo ni pamoja na Jamhuri ya Msumbiji, Botswana, Namibia na Mauritius chini ya  Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOMs) na Baraza la masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC).

Aidha, Kikao hicho kimejadili masuala mengine ikiwemo utekelezaji wa maamuzi  yanayohusu siasa na diplomasia katika Kanda, sera na mikakati ya siasa na diplomasia pamoja na mifumo ya usuluhishi na kuzuia migogoro ili kuimarisha demokrasia na ushirikiano kati ya Nchi Wanachama  kupitia Baraza la Usuluhishi (MRG) na Jopo la Wazee (PoE).


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.