Monday, September 9, 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amwakalisha Rais Samia kwenye ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.


Dkt. Biteko ametoa agizo hilo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika  Septemba 9, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) cha jijini Arusha.


Mhe.Dkt. Biteko amesema Serikali inatambua kuwa fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti yake kila mwaka zimekuwa zikitumika kwenye ununuzi wa umma na kuongeza kuwa Serikali imekuwa makini kuhakikisha fedha hizo zinapata usimamizi makini.


“Naomba Wizara ya Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji kwani bila ya maadili wananchi hawawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo tarajiwa na hivyo  umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.


Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na hivyo kuleta tija na kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika.


Hafla ya ufunguzi wa Jukwaa  hilo la 16 la Ununuzi wa Umma kwa Nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), umehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia maswala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Shaibu Mussa.


 Jukwaa hilo la  Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) linafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC, jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.