Monday, August 19, 2024

RAIS MNANGAGWA AKABIDHI ENEO LA UJENZI WA MAKUMBUSHO YA UKOMBOZI WA AFRIKA


Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa amezindua ujenzi wa Makumbusho ya Urithi wa Afrika na kukabidhi eneo la hekta moja (1) kwa ajili ya uhifadhi wa historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika linalotambulika kama Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC au “SADC Liberation Square” 


Mhe. Mnangagwa alikabidhi Kituo hicho rasmi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, ambapo kilipokelewa kwa niaba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi na kueleza kuwa Kituo hiko kitachangia juhudi za Kanda za kuenzi michango ya Wapigania uhuru katika harakati za ukombozi na pia ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kuenzi Waanzilishi wa SADC.


Kwa upande wake, Mhe. Mnangagwa alikiri kuwa Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC kitachangia uhifadhi wa historia muhimu za ukombozi ambazo zinaendelea kuandaliwa chini ya mpango wa kujenga Makumbusho ya SADC jijini Gaborone na ule wa kujenga Makumbusho ya Urithi wa Afrika nchini Tanzania. Hali kadhalika, Mhe. Mnangagwa alizialika nchi wanachama za SADC kuchangia katika kuboresha Kituo hicho kwa kuwasilisha zana za Sanaa kutoka nchini mwao zinazoelezea historia ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.


Makabidhiano ya eneo hilo yameenda sambamba na ziara ya kutembelea eneo la mradi pamoja na zoezi la kupanda mti ambao ulipandwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Magosi na kushuhudiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki ziara hiyo akiwemo, Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mtukufu Mswati III, Mfalme wa Eswatini, Mhe. Andry Rajoelina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar, na Mhe. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Jamhuri ya Botswana.


Ziara hiyo ilikuwa ni muendelezo wa ratiba ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 Agosti 2024. Akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuwaenzi wanaharakati wa kweli na wana wa Afrika waliojitoa muhanga katika kupigania ukombozi wa nchi zao. Hivyo, ni heshima kubwa kwa mataifa yetu kutambua mchango wao na kuona fahari kuienzi historia yetu.


Aidha, Wakuu hao wa nchi na Serikali walitembelea pia Kituo cha uchakataji taka cha Geo Pomona cha jijini Harare ambacho awali kilikuwa dampo na baadae  kuanza kuchakata taka kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme sambamba na kutoa ajira mbalimbali kupitia shughuli za kituo hicho.


Mradi huo una uwezo wa kukusanya taka ngumu zenye uzito wa tani 1000 na kuzaliwa kiasi cha Megawati 16 hadi 22 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya Taifa kwa matumizi ya umma wa Zimbabwe.


Akihutubia katika uzinduzi huo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa eneo hilo awali lilikuwa limekithiri kwa uchafu na wingi wa taka na hivyo kupatikana kwa teknolojia bora na ya kisasa ya kuchakata taka imesaidia kutunza mazingira kwa kuteketeza taka hatarishi pasipo kuleta madhara ya kiafya kwa bianadamu, mimea, wanyama na mazingira kwa ujumla.


“Zimbabwe imeweka ahadi ya kukiendeleza na kukisimamia kituo hiki ili kiwe cha mfano katika kuitengeneza kanda ya kijani kwa kutunza mazingira na kuzalisha umeme” alisema Mhe. Mnangagwa.


Aidha, alieleza kuwa miradi kama hii ni sehemu ya jitihada za ubunifu unaohitajika ili kuiletea Jumuiya ya SADC maendeleo na akasisitiza ni vyema kuendelea kuwa wabunifu katika kila sekta kwa kuwa ni wazi kuwa kila nchi itajengwa na wenye nchi na sio kinyume chake.

====================================

Habari katika picha; Matukio yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa eneo la Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika

Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walioshiriki katika ziara ya kutembelea eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika na Kituo cha kuchakata taka vilivyopo Harare, Zimbabwe tarehe 8 Agosti, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa akihutubia katika ziara ya ujumbe wa SADC kwenye kituo cha kuchakata taka tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe

Mhe. Mnangagwa akimkabidhi Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi eneo la ujenzi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika ambaye alipokea kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Mhe. Magosi akipanda mti katika eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika.


Mratibu wa Masuala ya SADC kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akimwagilia mti uliopandwa katika eneo hilo la mradi unaoashirikia "umoja na mshikamano katika kanda" wakati wa hafla ya uzinduzi wa eneo hilo.


Matukio mengine yaliyojiri katika kituo cha kuchakata taka






No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.