Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho
kutoka kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani, Balozi
Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Balozi Mteule wa Rwanda nchini,
Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.
Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amewapongeza mabalozi hao
kwa uteuzi waliuopata na pia amewaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa
majukumu yao kwa kipindi watakachokuwa nchini kuziwakilisha nchi zao.
Aidha, ameeleza Mabalozi hao Wateule wanatarajiwa kuwasilisha
Hati za Utambulisho kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania tarehe 12 na 13 Agosti, 2024.
Akiongea na Balozi Mteule wa Zimbambwe nchini, Mhe. Ndingani,
Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na ushirikiano wa
kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati, Mwl.
Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati, Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Vilevile, akamkaribisha Mhe. Ndingani kutembelea Maktaba ya Hayati Mwl. Nyerere iliyopo Butiama, mkoani Mara ambayo imesheheni historia yake.
Balozi Kombo pia, akaeleza umuhimu wa kuwekeza na kurithisha
historia ya ukombozi kwa vijana ili waweze kufahamu kwa kina namna waasisi hao
walivyojitoa kupigania uhuru wa Bara la Afrika hususan harakati za ukombozi wa nchi
za Kusini mwa Afrika.
Viongozi hao pia wamejadili juu ya umuhimu wa kufanyika kwa Mkutano
wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Zimbabwe ambapo
ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Tanzania na
Zimbabwe zinashirikiana katika masuala ya biashara, uwekezaji, usafirishaji,
usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi, elimu, Sanaa na utamaduni, na
sekta nyingine za kisiasa.
Akizungumza na Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Coppola, Mhe. Waziri Kombo amesisitiza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kupitia mpango wa ushirikiano wa Italia na Afrika unaofahamika kama “Mattei Plan”. Tanzania na Italia zinashirikiana katika sekta za utalii, elimu, Maji, biashara na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na ngozi ili kukuza biashara yake kimataifa.
Tanzania na Italia zinatarajia kuwa na Kongamano la biashara
litakalofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba, 2024 kwa lengo la kukuza
sekta ya biashara na za kiuchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili amabapo,
pembezoni mwa kongamano hilo kutafanyika mashauriano ya kisiasa.
Vilevile, katika mazungumzo yake na Balozi wa Rwanda, Mhe. Jenerali,
Patrick Nyamvumba, Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa Tanzania itaendelea
kushirikiana na Rwanda kupitia ujirani wa nchi hizo mbili sambamba na kusimamia
makubaliano mbalimbali yaliyokubaliwa katika nyakati tofauti na majukwaa mbalimbali
ambayo nchi hizo mbili zimekubaliana kuyatekeleza.
Tanzania na Rwanda zinashirikiana katika sekta za mawasiliano, biashara na uwekezaji, usafirishaji, elimu, utamaduni na michezo, miundombinu, kilimo na mifugo.
Jukumu hili la kupokea Nakala za Hati za Utambulisho
limefanywa na Mhe. Waziri Kombo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi
ya Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
=======================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Zimbabwe nchini, Mhe. Helen Bawange Ndingani (Kushoto).
Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.
=======================================
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Italia nchini, Mhe. Giuseppe Sean Coppola (Kushoto).
Mapokezi hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 6 Agosti, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mahmoud Thatib Kombo (Mb.) amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka
kwa Balozi Mteule wa Rwanda nchini, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba
(kushoto). Mapokezi hayo yamefanyka katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es
Salaaam tarehe 5 Agosti, 2024.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.