Sunday, August 25, 2024

Ujumbe wa Tanzania washiriki Mazoezi ya ‘Walk the Talk’


Brazzaville, Congo 

25 Agosti 2024

 

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wameungana na mgombea wa Tanzania kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Faustine Ndugulile (MB), katika mazoezi ya ‘Walk the Talk’.

 

Tukio hili la mazoezi ya ‘Walk the Talk’ lililofanyika Jijini Brazzaville, na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali waliowasili; lina lenga kuimarisha afya pamoja na kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza. 

 

Wakiwa kwenye mazoezi hayo, Waziri Mhagama na Waziri Kombo walipata fursa ya kusalimiana na mawaziri wenzao  na kuwaomba kuunga mkono mgombea wa Tanzania Dkt. Ndugulile katika juhudi zake za kuwania nafasi hii muhimu, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwa na maisha yenye afya na kufuata mifumo bora ya kuzuia magonjwa.

 

Wakati wa tukio hilo, viongozi hawa wa Tanzania walikuwa sehemu ya ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioandamana na Dkt. Ndugulile kwa ajili ya kumnadi na kumpigia kura katika uchaguzi wa Mkutano wa 74 wa WHO Kanda ya Afrika.

 

Ushiriki wa Tanzania kwenye mazoezi haya ni sehemu ya maandalizi na mkakati wa kuhakikisha kuwa Dkt. Ndugulile anapata uungwaji mkono kutoka kwenye nchi wanachama wa WHO, na pia kuonesha dhamira ya Tanzania katika kukuza afya ya jamii. 

 

Pamoja na Mawaziri hawa wawili, ujumbe wa Tanzania kwenye mazoezi hayo umejumuisha pia wabunge mahiri kwenye masuala ya chaguzi za kimataifa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni  Mwenyekiti wa Bunge Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Elibariki Emmanuel Kingu. Wengine ni Mhe. Neema Kichiki Lugangira, Mhe. Shamsia Azizi Mtamba, na Mhe. George Ranwell Mwenisongole.

 

Kauli Mbiu ya Dkt. Ndugulile kwenye kinyang’anyiro hiki ni “Pamoja, Tujenge Afya Bora Barani Afrika” yaani “Building a Healthier Africa Together” 



 


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.