Wednesday, August 21, 2024

WAZIRI KOMBO AAGANA NA BALOZI WA UFARANSA NA USWIS HAPA NCHINI.

Waziri wa Mambo ya Nje ma Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameagana na aliyekuwa Balozi wa Ufaransa Mhe. Nabil Hajlaoui na Balozi wa Uswisi Mhe. Didier Chassot ambao wamemaliza muda wao wa uwakilishi hapa nchini.


Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwa nyakati tofauti katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam Mhe. Balozi Kombo amempongeza Mhe. Nabil Hajlaoui kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.


“Mhe. Balozi Hajlaoui nakupongeza sana kwa kazi kubwa, nzuri na ya mfano, uliyoifanya hapa nchini, hasa katika eneo la kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa, kwakweli hongera sana na nikutakile kila la heri huko uendako,” alisema Balozi.


Naye Mhe. Balozi Hajlaoui ameshukuru kwa ushirikiano alioupata wakati wote alipokuwa nchini na hivyo kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi bila ya kikwazo chochote na kuahidi kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania huko aendako.


Katika tukio lingine akiagana na Balozi wa Uswisi anayemaliza muda wake nchini Mhe. Didier Chassot Balozi Kombo amemshukuru na kumpongeza kwa kushiriki kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi katika kipindi chake cha uwakilishi.


Amemuahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano kwa ajaye na kuendelea na kukamilisha masuala mbalimbali ya ushirikiano aliyoyaanzisha.


Naye Mhe. Chassot ameishukuru Wizara kwa ushirikiano mzuri iliyompatia wakati wote wa uwakilishi wake hapa nchini na kuahidi kuwa atayaendelea mazuri yote alyojifunza alipokuwepo hapa nchini.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.