Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha amani na usalama katika kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Balozi Kombo ametoa Msisitizo huo wakati wa Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO) wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.
Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 15 Agosti, 2024 ambapo, mikutano hii miwili ni mikutano ya awali ya maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika leo tarehe 16 Agosti, 2024.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo kujadili ajenda zilizojikita katika kutafuta amani na usalama wa Jumuiya hiyo na umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kufanikisha jitihada za suala hilo.
Agenda zilizojadiliwa na mkutano huu ni pamoja na Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda, Uimarishwaji wa Demokrasia katika Kanda, Mfumo wa Kuwaenzi Viongozi Waasisi wa SADC na Wagombea wa Nafasi mbalimbali wa Kanda katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.
Akichangia katika mkutano huo Waziri Kombo amesema kuwa Tanzania inalipa kipaumbele suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika kanda na katika kufanikisha hili Tanzania inashiriki kikamilifu katika juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake.
“Tuna nia ya dhati ya kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika masuala ya amani na usalama. Tunaamini uzoefu wetu utatuwezesha kuchangia kwa ufanisi katika jukumu la Baraza la Usalama” alisema waziri Kombo.
Aidha, Waziri Kombo amewasilisha ombi la kuendelea kuungwa mkono na nchi za SADC katika nafasi mbalimbali zinazowaniwa na Watanzania ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Afrika inayowaniwa na Dkt. Faustine Ndugulile.
Pia, ameomba kuungwa mkono katika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2026 – 2028 na Ujumbe usio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029 na 2030.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.
=======================================
Kulia ni Mhe. Dkt. Ndugulia anayewania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika. |
Ujumbe wa Tanzania ukiwa umesisiamam wakati wimbo wa SADC uliokuwa ukiimbwa kabla ya kuanza kwa mkutano. |
Ujumbe wa Zambia |
Sehemu nyingine ya Ujumbe wa Tanzania |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.