Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana Harare, Zimbabwe kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya husika utakaofanyika tarehe 17-18 Agosti,
2024.
Mkutano huo unatarajia kujadili masuala mbalimbali ikiwemo, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, usalama wa chakula na lishe kwenye kanda na Utekelezaji wa Mpango wa Manunuzi ya Pamoja ya Huduma za Afya ya SADC unaoratibiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ya Tanzania.
Aidha, hafla ya
ufunguzi wa mkutano huo imewezesha makabidhiano ya nafasi ya unyekekiti katika
ngazi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Nazaré José Salvador amekabidhi nafasi hiyo
kwa mwenyekiti mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya
Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbambwe, Balozi Albert Ranganai Chimbindi
akisisitiza kumpa ushirikiano katika nafasi hiyo.
Naye Balozi Chimbindi amemshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda
wake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Pia ameahidi kuzingatia ushauri
aliokuwa akiutoa kwa Sekretariet ya SADC na kufanya kazi pamoja ili kuyafikia
malengo ya jumuiya hiyo kwa maslahi jumuishi.
“Tumepiga hatua lakini bado tuna kila sababu ya kuweka bidii
kwenye ujenzi wa miundombinu, usafiri na hatimaye tuweze kuifikia SADC
tunayoitaka. Niwahakikishie kuwa Zimbabwe ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi
kwa kufuata malengo, kanuni na mikataba ya SADC'', Balozi Chimbindi.
Mkutano wa Wakuu wa
Nchi na Serikali SADC utatanguliwa na
mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ambayo ni: Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi
ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics,
Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao
utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa
kipindi cha Agosti 2023 hadi Agosti 2024. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za
SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa
Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu
Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ
aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).
Mikutano mingine ni:
Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2024 pamoja;
na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika
utakaofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024.
===================================
Kushoto ni Afisa Sheria Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Felister Lero na Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule wakifatilia mkutano. |
Picha ya pamoja:
Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) baada ya
ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika
tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.