Thursday, August 1, 2024

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NJE AFUNGUA MKUTANO KUJADILI ITIFAKI YA UMOJA WA AFRIKA KUHUSU UHURU WA WATU KUSAFIRI BILA VIKWAZO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kuridhia Itifaki ya Uhuru wa Watu Kusafiri bila Vikwazo ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Balozi Mussa ametoa wito huo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo Agosti 01, 2024 mjini Unguja, Zanzibar.

Amesema kuwa faida za Itifaki hiyo ni nyingi kwa watu wa Afrika ambapo mbali na kurahisisha usafiri wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, lakini pia ni muhimu katika ukuzaji rasilimali watu na kutengeneza fursa kwa vijana kama vile biashara, utalii, kuimarisha utamaduni miongoni mwa watu na kwa kiasi kikubwa itakuza uchumi wa nchi za Afrika. Itifaki hiyo pia itawawezesha raia kutoka nchi za Afrika kuishi na kujenga uchumi kwa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Amesema  mafanikio ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambao umeanza kutekelezwa na nchi wanachama tangu mwaka 2021, yatafikiwa kikamilifu pale nchi zote wanachama zitakaporidhia Itifaki hii ili kwenda sambamba na Itifaki nyingine za Uhuru wa Kuingiza  Bidhaa na Uhuru wa Kutoa Huduma.

“Ninafurahi kwamba Nchi nyingi na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi kama EAC, ECOWAS, IGAD na SADC zimefanyia kazi Itifaki hii kupitia kanda zao na lengo ni kuongeza zaidi uhuru wa watu wa Afrika kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine”, amesema Balozi Mussa.

Pia amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha kuridhiwa kwa Itifaki hiyo ambayo ilipitishwa na nchi za Afrika mwaka 2018. Hadi sasa ni nchi nne pekee zimeridhia itifaki hiyo inayohitaji nchi 15 kuiridhia ili kuanza utekelezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo  amesema kuwa Mkutano huo utajikita katika kuainisha changamoto na nini kifanyike ili kuwezesha kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika hususan katika sekta ya ukuzaji biashara, utalii na uchumi kwa ujumla. Pia amesema wajumbe watajadili, kujifunza na kubadilishana uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na nchi ambazo tayari zimeridhia  Itifaki hiyo.

Naye Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC, Mhe. Rita Amijkhobu amesema Itifaki hiyo ikianza kutumika itainganisha Afrika na kuwa kitu kimoja ambapo itawezesha watu kupita kwenye mipaka kwenda nchi nyingine bila vikwazo hatua itakayosaidia mzunguko wa biashara kukua kwa haraka.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akizungumza katika ufungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo Agosti 01, 2024 mjini Unguja, Zanzibar. 


Mhe. Rita Amijkhobu, Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC naye akizungumza kwenye Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika leo

Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Mhe. Emilio Rossetti akielezea jambo kwenye mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 

Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shiyo akizungumza na kuwakaribisha wageni waliokuja nchini kuhudhuria Mkutano wa majadiliano.

Juu na chini ni sehemu ya wajumbe walio hudhuria  Mkutano kwenye mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 




Sehemu ya wajumbe kutoka Zimbabwe na Uganda wakifuatalia kwa makini ufunguzi rasmi wa mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo. 

Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo ukiendelea. 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.