Rais wa Jamhuri ya
Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema ameihakikishia ushirikiano Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wakati huu inapotarajia kukabidhiwa jukumu la uenyekiti wa Asasi ya
Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics,
Defence and Security) na kuahidi kutimiza majukumu yake kama Mwenyekiti anayemaliza
muda wake kwa kipindi cha 2023/2024.
Kadhalika, ameshukuru kwa ushirikiano
alioupata wakati wa uongozi wake na pia ameonesha kuwa na imani na Tanzania
katika kupokea jukumu la unyekiti wa Asasi ya SADC Organ Troika.
“Nipende kumhakikishia ushirikiano dada yangu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi
wake, pia nina imani utaiongoza Organ na kuifikisha katika hatua ya juu ya
mafanikio kama ambavyo umekuwa ukifanya katika majukumu mengine uliyoaminiwa” Mhe.
Hichilema.
Hayo yamejiri wakati
wa Mkutano wa Wakuu wa
Nchi na Serikali wa Asasi hiyo ya SADC Organ Troika uliofanyika tarehe 16
Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe na kuhudhuria na Mhe. Hichilema Rais wa Jamhuri ya
Zambia na Mwenyekiti wa sasa ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao.
Mbali
na Mhe. Hichilema Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mhe. Nangolo Mbumba Rais wa
Namibia na Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wake na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti ajaye wa
Asasi hivyo, kukamilisha safu ya nchi zinazounda Utatu huo.
Aidha,
katika hotuba wakati wa kufungua na kufunga mkutano Mhe. Hichilema amewashukuru
wajumbe wa mkutano huo kwa kutumia muda wao na rasilimali zao kuhudhuria na
kushiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali yenye maslahi ya kanda.
“Ni
matumaini yangu kuwa agenda zilizowasilishwa mbele yetu zitajadiliwa kwa tija
na kwa maslahi ya pande zote kwa ajili ya ustawi wa Jumuiya na watu wetu”
alisema Mhe. Hichilema.
Hivyo,
ni muhimu kuwa tayari kuonesha umoja na nia ya kufanikiwa kwa pamoja katika
kuijenga jumuiya yenye amani na usalama hali ambayo itachangia kukuza uchumi
kupitia shughuli za biashara na uwekezaji kwenye kanda.
Pia,
alitoa shukrani za kipekee kwa Jamhuri ya Namibia kwa kipindi ambacho imeongoza
kupitia Hayati Rais Hage Geingob na Rais wa sasa Mhe. Dkt. Nangolo Mbumba,
sambamba na Sekretarieti ya SADC kwa usikivu, uvumilivu na uongozi wa mfano wa
Bw. Elias Magosi ambaye pamoja na timu yake wamekuwa wakifanya kazi bila
kuchoka kuratibu kufanyika kwa mikutano hiyo.
Vilevile
akaeleza kuwa utatu wa asasi hiyo ni utaratibu mzuri wa kuendesha taasisi
yoyote yenye lengo la kufikia mafanikio kwakuwa, inaruhusu muendelezo wa
utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kikanda na kuhifadhi kumbukumbu ya masuala
mbalimbali ili hurahisisha ufuatiliaji na maamuzi.
Tanzania
inatarajia kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika
masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence
and Security) katika Mkutano wa Kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali
utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe.
Pamoja na masuala mengine mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Organ Troika umepitia na kujadili hali ya ulinzi na usalama katika kanda, hali ya ulinzi na usalama katika Falme za Eswatini na Lesotho, hali ya ulinzi na usalama katika jimbo la Cabo Del Gado na hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Habari katika picha, wakati Rais Samia aliposhiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Organ Troika
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.