Tuesday, August 20, 2024

WAZIRI KOMBO APOKEA MWALIKO WA RAIS SAMIA KUSHIRIKI JUKWAA LA FOCAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushiriki Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping utakaofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing nchini China. 


Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, pia umeainisha  nafasi ya kipekee kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na kuzungumza Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa.


Akipokea mwaliko huo kwa niaba ya Mhe. Rais, Mhe. Balozi Kombo ameelezea kuwa nafasi ya Mhe. Rais kushiriki na kuzungumza katika Jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla,  hali ambayo itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kupigiwa mfano kwenye Jumuiya hiyo kongwe Afrika.


Aidha Balozi Kombo amemhakikishia Balozi Chen ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC ambapo Tamko la FOCAC na Mpango Kazi wa FOCAC itakuwa ni moja ya Matokeo ya Mkutano huo. 


Naye Balozi wa China Mhe. Chen ameelezea kufurahishwa kwa China kutokana na kupokelewa kwa mwaliko wa kuhudhuria Mkutano na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China.


Amesema China inaona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kuahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania. 


Jukwaa la Focac lilianzishwa kwa lengo la kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika ili kuchagiza maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 


FOCAC limekuwa jukwaa linalotoa fursa sawa kwa pande zote mbili kujadili masuala muhimu ya kimaendeleo na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo amani na usalama na mabadiliko ya tabia nchi.





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.