Sunday, October 6, 2024

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI AONGOZA KIKAO CHA WAKUU WA MISHENI ZA UANGALIZI ZA KIMATAIFA ZILIZOPO MSUMBIJI

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume tarehe 06 Oktoba 2024 ameongoza kikao kazi cha Wakuu wa Misheni za  Kimataifa za Uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024.

 

Mkutano huo ulihudhuriwa na Wakuu wa Misheni za Uangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU-EOM), Umoja wa Ulaya (EU-EOM), Jumuiya ya Madola na Jukwaa la Uchaguzi la Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (ECF-SADC).

 

Misheni ya uangalizi ya Umoja wa Afrika inaongozwa na Makamu wa Rais Mstaafu wa Angola, Mhe. Bornito de Sousa Baltazar Diogo huku Misheni ya Jumuiya ya Madola ikiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Saint Lucia, Mhe. Kenny Anthony.

 

Aidha, Misheni ya Umoja wa Ulaya inaongozwa na Mbunge katika Bunge la Ulaya, Mhe. Laura Ballarin Cereza na Misheni ya ECF-SADC inaongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Angola, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva.

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akiongoza kikao kazi cha Wakuu wa Misheni za Kimataifa za Uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024. Kikao hicho kilifanyika tarehe 06 Oktoba, 2024 jijini Maputo na kuhudhuriwa na Wakuu wa Misheni za Uangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU-EOM), Mhe. Bornito de Sousa Baltazar Diogo, Makamu wa Rais Mstaafu wa Angola, Umoja wa Ulaya (EU-EOM), Jumuiya ya Madola, Mhe. Kenny Anthony, Waziri Mkuu Mstaafu wa Saint Lucia na Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva wa Jukwaa la Uchaguzi la Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (ECF-SADC).

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Msumbiji kutoka Umoja wa Afrika (AU-EOM), Mhe. Bornito de Sousa Baltazar Diogo, Makamu wa Rais Mstaafu wa Angola akishiriki kikao cha Wakuu wa Misheni za Ungalizi za Kimataifa kilichoongozwa na Mhe. Dkt. Karume

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji kutoka Jukwaa la Uchaguzi la Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (ECF-SADC), Mhe. Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva akishiriki kikao cha Wakuu wa Misheni za Ungalizi za Kimataifa kilichoongozwa na Mhe. Dkt. Karume
Mhe. Dkt. Karume akisalimiana na Mhe. Kenny Anthony, Waziri Mkuu Mstaafu wa Saint Lucia ambaye pia ni Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji kutoka Jumuiya ya Madola

Mhe. Dkt. Karume akiteta jambo na Mhe. Kenny Anthony, Waziri Mkuu Mstaafu wa Saint Lucia ambaye pia ni Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji kutoka Jumuiya ya Madola
Mhe. Dkt. Karume akizungumza na Mwakilishi wa Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya Umoja wa Ulaya. Kushoto ni Mjumbe wa Troika kutoka Tanzania ambaye pia ni Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa
Balozi Mussa akisalimiana na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Msumbiji kutoka Umoja wa Afrika (AU-EOM) na Makamu wa Rais Mstaafu wa Angola, Mhe. Bornito de Sousa Baltazar Diogo

Picha ya pamoja ya Waku wa Misheni za Uangalizi za Kimataifa
Picha ya pamoja ya Wakuu wa Misheni za Kimataifa za Uangalizi  wa Uchaguzi nchini Msumbiji wakiwa na Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania ambao ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ay Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mussa (kushoto) na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema (kulia) 

Picha ya pamoja










































 

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI VYA NCHINI MSUMBIJI


Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume  tarehe 06 Oktoba, 2024 jijini Maputo amefanya mazungumzo na viongozi na wawakilishi  kadhaa wa vyama vya upinzani vya Msumbiji ikiwa ni mwendelezo wa jukumu lake la kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024.

 

Katika mazungumzo yake na viongozi hao kutoka vyama vya MPD, PEMO, UDM, RD, PDM, Ecologists na PPD, Mhe. Dkt. Karume pamoja na mambo mengine aliwaeleza lengo la Misheni anayoiongoza kuwa ni kuangalia uchaguzi kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya uchaguzi ya SADC iliyorekebishwa mwaka 2021 inayozingatia misingi ya haki, usawa na demokrasia. Pia alitumia fursa hiyo kuwatakia wananchi wa Msumbiji uchaguzi wa amani na utulivu.

 

Ujumbe wa Mhe. Dkt. Karume  kwenye mkutano huo uliwajumuisha Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania, Zambia na Malawi, Sekretarieti ya SADC akiwemo Mkurugenzi wa Organ , Prof. Kula Ishmael Theletsane na  Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC). Wajumbe  wa Troika kutoka Tanzania walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na  Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema.

 

 Mhe. Dkt. Karume kwa nafasi yake ya Mkuu wa Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC ameendelea kukutana na viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambapo hadi sasa amekutana na Mwenyekiti wa  Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Kamishna Msidizi wa Jeshi la Polisi la Msumbiji na Mgombea urais wa Chama Tawala cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo na Viongozi wa dini.

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza  na viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani vya Msumbiji ikiwa ni mwendelezo wa jukumu lake la kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024. Mkutano huo umefanyika tarehe 06 Oktoba 2024 jijini Maputo na kuwahusisha viongozi kutoka vyama vya MPD, PEMO, UDM, RD, PDM na PPD
Mjumbe wa Troika kutoka Tanzania ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akijitambulisha wakati wa kikao kati ya Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya SADC, Mhe. Dkt. Karume na viongozi wa vyama vya upinzani vya nchini Msumbiji
Mjumbe wa Troika kutoka Tanzania ambaye pia ni Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema akijitambulisha wakati wa kikao kati ya Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya SADC, Mhe. Dkt. Karume na viongozi wa vyama vya upinzani vya nchini Msumbiji
Sehemu ya viongozi hao wa vyama vya upinzani vya Msumbiji wakizungumza wakati wa kikao kati yao na Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini humo, Mhe. Dkt. Karume
Kiongozi wa Chama cha Ecologists akizungumza 
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea
Mjumbe kutoka Baraza la SADC la Ushauri kuhusu masuala ya Uchaguzi akizungumza 
Mjumbe wa Troika kutoka Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akizungumza
Mhe. Dkt. Karume akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi wa vyama vya upinzani aliokutana nao
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Picha ya pamoja





 

MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA SADC NCHINI MSUMBIJI AENDELEA KUKUTANA NA WADAU WA UCHAGUZI NCHINI MSUMBIJI

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume ameendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024.

 

Mhe. Dkt. Karume  kwa nyakati tofauti leo tarehe 05 Oktoba 2024 jijini Maputo, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msumbiji, Mchungaji Augusto Pedro na Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Binadamu (CDD), Prof. Adriano Nuvunga.

 

Katika mazungumzo yake na viongozi hao, Mhe. Dkt. Karume pamoja na mambo mengine aliwaeleza lengo la Misheni hiyo ya SADC kuwa ni kuangalia uchaguzi kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya uchaguzi ya SADC iliyorekebishwa mwaka 2021 inayozingatia misingi ya haki, usawa na demokrasia.

 

Ujumbe wa Mhe. Dkt. Karume  kwenye mikutano hiyo uliwajumuisha Wajumbe wa Troika kutoka Tanzania, Zambia na Malawi, Sekretarieti ya SADC akiwemo Mkurugenzi wa Organ , Prof. Kula Ishmael Theletsane na  Wajumbe wa Baraza la Ushauri wa masuala ya Uchaguzi la SADC (SEAC). Wajumbe  wa Troika kutoka Tanzania walioshiriki ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa na  Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema.

 

Vilevile, Mhe. Dkt. Karume amepokea taarifa kutoka kwenye Kamati ya Uandishi ya Misheni hiyo kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa kutoka kwa waangalizi wa SADC ambao walisambazwa kwenye majimbo 11 ya uchaguzi nchini humo tangu tarehe 03 Oktoba 2024.

 

Mhe. Dkt. Karume kwa nafasi yake ya Mkuu wa Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC ameendelea kukutana na viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa uchaguzi ambapo hadi sasa amekutana na Mwenyekiti wa  Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Msumbiji, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Kamishna Msidizi wa Jeshi la Polisi la Msumbiji na Mgombea urais wa Chama Tawala cha FRELIMO, Mhe. Daniel Francisco Chapo.

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC –SEOM) nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume akizungumza na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msumbiji, Mchungaji Augusto Pedro (hayupo pichani) ikiwa ni mwendelezo wa Mkuu huyo wa Misheni ya SADC wa kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi mkuu wa Msumbiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 Oktoba 2024. Mazungumzo yao yalifanyika jijini Maputo tarehe 5 Oktoba 2024
Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msumbiji, Mchungaji Augusto Pedro akizungumza na Mkuu wa Misheni ya SADC ya uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Karume (hayupo pichani)
Mazungumzo yakiendelea kati ya Mhe. Dkt. Karume (kulia) na Mchungaji Pedro (kushoto)

Mhe. Dkt. Karume akizungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Binadamu (CDD), Prof. Adriano Nuvunga katika mkutano uliofanyika jijini Maputo tarehe 5 Oktoba 2024
Mjumbe wa Troika na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Sahibu Mussa akichangia jambo wakati wa mkutano kati ya Mhe. Dkt. Karume na Prof. Nuvunga hawapo pichani.
Mjumbe wa Troika na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Sofia Mjema akichangia hoja wakati wa Mkutano kati ya Mhe. Dkt. Karume na Mkurugenzi wa CDD, Prof. Nuvunga hawapo pichani
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la SADC la masuala ya Uchaguzi naye akichangia jambo
Mjumbe wa Troika ambaye pia ni Balozi wa Malawi nchini Msumbiji, Mhe. Wezi Moyo akichangia jambo. Kushoto ni Mjumbe wa Troika kutoka Zambia, Bw. Lubasi
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri naye akichangia jambo
Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Taarifa ya Misheni ya SADC, Bi. Shazma Msuya akitoa taarifa kwa Mkuu wa Misheni ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi nchini Msumbiji, Mhe. Dkt. Karume (hayupo pichani)
Bi. Msuya akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Misheni, Mhe. Dkt. Karume
Uwasiishaji taarifa ya Misheni ukiendelea
Mhe. Dkt. Karume akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msumbiji baada ya kukamilisha mazungumzo yao
Mhe. Dkt. Karume akiagana na Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Msumbiji mara baada ya mazungumzo yao
Mhe. Dkt. Karume akiagana na Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Binadamu (CDD), Prof. Adriano Nuvunga baada ya mazungumzo yao
Picha ya pamoja 
















 






Saturday, October 5, 2024

WAZIRI KOMBO AWATAKA WATAFITI WA AFRIKA KUZINGATIA UZALENDO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akichangia mada kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewataka Wanazuoni, Asasi za Kiraia na Taasisi zinazofanya tafiti kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Bara la Afrika kutanguliza uzalendo na maslahi ya Afrika ili matokeo ya tafiti hizo yaweze kuwa na tija kwa Afrika.

Waziri Kombo ameyaeleza hayo alipokuwa akichangia mada kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika (APSD) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaoendelea jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini. Mada hiyo ilihitaji ufafanuzi kuhusu, namna Serikali za Afrika zinatumia na kuzingatia matokeo ya tafiti katika kufanya maamuzi ya masuala mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro. 

Akizungumza kuhusu mada hiyo Waziri Kombo licha ya kueleza kuhusu umuhimu wa utafiti na mchango wake kwa Serikali katika kufanya maamuzi yenye tija kwa wanchini, alisema kuwa Watafiti wengi wa Waafrika wamekuwa wakitanguliza maslahi ya wanaowafadhili na hivyo kupotosha uhalisia wa masuala husika ambapo huondoa uhalali na ushawishi wa kutumiwa na Serikali za Afrika katika kufanya maamuzi mbalimbali.

“Sote tunatambua kuwa, kufanya tafiti kunahitaji rasilimali, fedha nyingi na muda wakutosha, hivyo Serikali nyingi za Afrika zimekosa uwezo wa kutafati masuala mengi kwa wakati. Nitoe wito kwa wanazuoni na taasisi mbalimbali inapotokea fursa za kufanya tafiti lazima kutanguliza uzalendo na maslahi ya Afrika kwanza ili matokeo ya tafiti husika yawe na mchango kwa Serikali na watu wake”. Alieleza Waziri Kombo 

Waziri Kombo katika mchango wake ambao uliwavutia wengi katika mdahalo huo, aliongeza kusema kuwa yapo masuala mengi muhimu yanayohusu Waafrika ambayo tulipaswa kuyafahamu, mathalani kiwango na aina za rasilimali tulizonazo katika mataifa yetu, lakini tafiti nyingi hazijielekezi katika kutafuta majawabu ya masuala kama hayo badala yake yanajielekeza kutafiti masuala yenye maslahi kwa wafadhili wao. 

Mbali na kusisitiza suala la uzalendo Waziri Kombo aliwataka Watafiti kuzingatia ubora na weledi wa tafiti zao. Alieleza kuwa wakati mwingine watafiti wamekuwa wakitoa matokeo yenye taarifa zisizokuwa na uhalisia hasa takwimu hivyo kuadhiri utekelezaji wa mipango na mikakati inayotegemea taarifa za tafiti hizo.

Katika mdahalo huo uliohudhuriwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki, Waziri Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbambwe Mhe. Federick Shava walishirikiana katika kujadili na kuchangia mada hiyo wakiongozwa na Prof. Antoni van Nieuwkerk kutoka Chuo Kikuu cha Wits cha jijini Johannesburg.

Mdahalo huo wa siku tatu unalenga kujadili masuala ya Amani na Ulinzi pamoja na kutafuta namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro inayoendelea Barani Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifuatilia jambo kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifafanua jambo kwenye Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbambwe Mhe. Federick Shava na Prof. Antoni van Nieuwkerk (katikati) akiongoza mdahalo huo
 Mdahalo ukiendelea
 Mdahalo ukiendelea
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Bertha Makilagi akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Emmanuel Shayo akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki akifuatilia Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki unaondelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Rais wa zamani wa Zibwabwe Mhe. Johaquim Chissano akihutubia kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa kwanza wa Amani na Usalama Afrika uliofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa njia ya mtandao.