Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kimeelezwa kuwa ni moja ya muhimili muhimu katika kufanikisha agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 31, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo alipokutana na uongozi wa kituo hicho chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Christine Mwakatobe.
Mhe. Londo alisema kuwa Rais Samia amelipa umuhimu mkubwa suala la utalii ndiyo maana amecheza filamu ya Tanzania: The Royal Tour, na manufaa yake yameaanza kupatikana kwa kuongezeka kwa watalii na fedha za kigeni nchini.
"Utalii una maeneo mengi na moja kati ya hayo maeneo ni utalii wa mikutano. Hivyo, kwa Tanzania hakuna taasisi nyingine inayotegemewa na Serikali kulitekeleza kwa ufanisi eneo hili na kulitolea miongozo isipokuwa AICC pekee", Waziri Londo alisema.
Mhe. Londo aliongeza kuwa AICC ndiyo sura na kioo cha nchi na ni moja ya kituvu cha diplomasia ya Tanzania, hivyo, endapo watumishi wa kituo hicho watajituma kwa kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa, basi watakuwa wamelitangaza vyema jina la Tanzania.
"Mnapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi, wanaokuja kushiriki mikutano. Wageni hawa, wengi wao huwa hawapati fursa ya kwenda sehemu yoyote zaidi ya AICC kutokana na ratiba za mikutano, maana yake wakiridhika na huduma zenu, mtakuwa mmelitangaza jina la Tanzania na kinyume chake mtakuwa mnalibomoa jina la Tanzania" Mhe. Londo alitahadharisha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Mwakatobe ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, amesema kuwa malengo yake ni kukifanya kituo hicho kuwa taasisi namba moja nchini, Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau ili aweze kufanikisha lengo hilo.
Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho kama vile uchakavu wa miundombinu, kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi, ameanza kuchukua hatua ya kufanya maboresho ya majengo na ununuzi wa vifaa vya kisasa kama vile vifaa vya ukalimani, vyoo na vipoza joto.
Aidha, amesema kwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao, Kituo kimeanza kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili shughuli zote ziweze kufanyika kidigitali kwa lengo la kuongeza mapato na kuleta ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja.
Amemalizia kwa kusema kuwa mapato ya kituo hicho yameongezeka kwa kupata faida ghafi ya bilioni 6.5 mwaka 2023/2024 ukilinganisha na faida ya bilioni 1.7 mwaka 2022/2023.
Mhe. Naibu Waziri Londo kabla ya kufanya kikao na menejimenti ya AICC alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na kituo hicho. Maeneo hayo ni pamoja na Kijenge site D 1 lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 21, Kijenge site E lenye nyumba za makazi na ukubwa wa ekari 48 na Soweto ambapo pia kuna makazi na ukubwa wa ekari zaidi ya 50.
Mhe. Naibu Waziri baada ya kuona maeneo hayo ambayo yote yapo katikati ya jiji la Arusha, amesema kuwa AICC ina uwezo wa kulibadilisha jiji hilo endapo rasilimali hizo zitatumiwa ipasavyo.