|
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Bi. Dana Hyde, Mtendaji Mkuu wa MCC mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Marriot Jijini New York. |
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE
HOUSE,
1
BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Sasa
ni Rasmi: Tanzania kupata mabilioni mengine ya MCC
· Yafaulu mtihani wa kupata bilioni 992.8
za kuboresha sekta ya umeme
· Yafanikiwa baada ya kutimiza masharti
yote likiwemo la kupambana na rushwa
· Zitaanza kutolewa mwakani baada ya
kupigiwa kura na Bodi ya MCC
Tanzania
imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka
Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium
Challenge Corporation (MCC) la Marekani na itaanza kupata na kunufaika na
mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya
kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Habari
hizo njema zimetangazwa Jumamosi, Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu wa
MCC, Bi. Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot
Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo
Bwana Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC. Rais Kikwete yuko New
York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Hongera
Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya
kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa
MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Bi. Hyde
amemwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi
za Fedha wa Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.
Bi. Hyde
amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17,
mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,
Bwana John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika
masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na
rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.
MCC
imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha
kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya
kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa
kukabiliana na rushwa.
Tofauti
na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC
hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa
uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na
fedha hizo.
Miongoni
mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani
ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani
duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani
(USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi Lenhardt,
Mtendaji Mkuu
wa MCC Bi. Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI)
Balozi Mark Green.
Mabalozi
Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa
majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1.
Bi
Hyde amesema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa
kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa
MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania ikiwa ni
pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi nchini. Kiasi cha asilimia
46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na
sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1.
Chini
ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani
milioni 472.8 (sawa na sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola
milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1 basi
Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo
kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2
zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi
kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi
ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium
Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo
itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha
zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga,
Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha,
fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya
Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa
10 ya Tanzania Bara.
Fedha
hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya
Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga
barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa
kiwango cha lami.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
27
Septemba, 2015