Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. January Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano
wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala
ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO)
unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati
ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024, pamoja na mambo mengine
umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya
Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa
SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika
Kanda.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye
pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia,
Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo
ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika
nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya
kudumu inapatikana kwenye maeneo ya changamoto.
Aidha, akizungumzia hali ya amani
na usalama kwenye maeneo yenye
changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Mhe. Haimbe amesema hali sasa
inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na
mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo
endelevu ya kiuchumi katika kanda.
Kadhalika amezipongeza misheni za
ulinzi wa amani za SADC iliyopo DRC na ile iliyopo Kaskazini mwa Msumbiji kwa
kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha amani na usalama kwenye maeneo hayo
vinarejea mbali na changamoto kadhaa wanazopitia.
Kuhusu misheni ya ulinzi wa amani
ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambayo inamaliza muda wake wa operesheni mwezi
Julai 2024, Mhe. Haimbe ameipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kupambana na
vitendo vya ugaidi na kurejesha hali ya amani kwa wananchi wa Jimbo la Cabo
Delgado lililopo Kaskazini mwa Msumbiji.
“Napongeza misheni ya SAMIM kwa
kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Japo wanamaliza operesheni huko Kaskazini mwa
Msumbiji, bado mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka katika
Nchi zote wanachama wa SADC yataendelea. Hivyo naziomba nchi zote wanachana
kuendelea kushirikiana na kuandaa mikakati ya pamoja kukabiliana na vitisho
hivi” alisisitiza Mhe. Haimbe.
Awali akizungumza, Katibu
Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC
itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na
kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Pia aliongeza kusema bado
jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali
zilizopo katika kanda ikiwemo ugaidi, vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka na
rushwa. Kadhalika, Mhe. Makosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa
Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Haimbe kwa kazi nzuri aliyofanya
katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya
ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa
Tanzania, Mhe. January Makamba.
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama
ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika
kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka
mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.
Mbali na Mhe. Makamba, ujumbe wa
Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu
Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.
Samwel Shelukindo, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob
Mkunda, Balozi wa Tanzania nchini
Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa
Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi.
Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024. |
|
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano
katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11
na 12 Julai 2024. |
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) kwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob
Mkunda (katikati) na Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Mnyepe (kulia) wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano
katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11
na 12 Julai 2024. |
|
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano
katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) ambaye pia ni Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt.
Mulambo Haimbe akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi Mkutano huo iliyofanyika tarehe 11 Julai 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mulungushi uliopo jijini Lusaka, Zambia
|
|
Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri
|
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shelukindo akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha
Waziri |
|
Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jenerali Mathew Mkingule akishiriki Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa SADC
|
|
Meza kuu
|
|
Mkutano ukiendelea
|
|
Mhe. Waziri Makamba akizungumza na viongozi mbalimbali kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
|
|
Picha ya pamoja
|