Serikali ya Tanzania na Cuba
zimesisitiza kukuza ushirikiano wa kimkakati ili kuendelea kuimarisha
ushirikiano wa kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo
mawili Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati, Fidel Castor Ruz wa Cuba.
Msisitizo huo umetolewa wakati
wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba uliofanyika
kwa njia ya mtandao tarehe 30 Oktoba 2024 katika Kikao cha Ngazi ya Wataalamu
ambapo ujumbe wa Tanzania ulishiriki kikao hicho katika Ofisi Ndogo za Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ufunguzi wa
mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Naomi Mpemba kwa
niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameeleza kuwa na imani na wajumbe wa mkutano huo
na kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana kwa dhati na Cuba kwa ajili ya
maendeleo endelevu na ustawi wa nchi hizo mbili.
Aidha, ameeleza kuwa kufanyika
kwa mkutano huo ni matokeo ya ziara ya Makamu wa Rias wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador
Valdés Mesa nchini mwezi Januari, 2024 ambapo alikubaliana masuala
mbalimbali ya ushirikiano na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na kuelekeza kufanyika kwa
Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.
‘’Mkutano huu ni ushahidi
tosha wa nia thabiti waliyonayo viongozi wetu na sisi wataalamu katika kukuza
ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa kuweka mfumo rasmi wa ufuatiliaji
wa masuala mbalimbali ya utekelezaji na kujitathmini mara kwa mara’’ alieleza
Bi. Mpemba.
Ushirikiano kati ya Tanzania
na Cuba licha ya kuwa imara kisiasa na kidiplomasia, pia umekuwa ngao muhimu ya
kufungua fursa mbalimbali katika sekta muhimu kama vile: afya, elimu, utalii,
biashara, uwekezaji na utafiti. Kadhalika ushirikiano huu umerasimishwa kwa Mikataba
na Hati za Makubaliano ya Ushirikiano zenye taratibu za kisheria zilizopelekea
kupatikana kwa fursa za ufadhili wa masomo, teknolojia mpya, mafunzo ya
udaktari na kushirikishana pamoja utaalamu katika maeneo tofauti.
Hata hivyo, ameleeza kuwa bado
kuna fursa mbalimbali katika ushirikiano wa Tanzania na cuba zinazohitaji
kuwekewa mikakati ya kuzikuza na kuziimarisha kwa kuongeza maeneo mapya ya
ushirikiano.
Naye Kiongozi wa Ujumbe wa
Kikao cha Wataalam na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Cuba, Balozi Carlos Hernandez ameeleza
kuwa na matumaini na kikao hicho kuwa cha mafanikio kwa ustawi wa pande zote
mbili na kusisitiza umuhimu wa kufanyika majadiliano ya kina na ya mafanikio
katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati.
‘’ Kwa kile kidogo tulicho
nacho tupo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kujenga uwezo na
kutoa ujuzi hususan katika masuala ya teknolojia kwa maendeleo na ustawi wa
pande zote mbili’’ alisema Balozi Hernandez.
Kikao hiki pamoja na masuala
mengine kimejadili kukuza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kati ya
Tanzania na Cuba ikiwemo ushirikiano katika sekta ya afya, kilimo na uzalishaji
wa chakula, elimu na masuala ya utamaduni na michezo. Aidha, kikao hicho cha
watalaamu ni maandalizi ya Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Tanzania na Cuba
utakaofanyika tarehe 4 Novemba, 2024 jijini Havana, Cuba.
Kikao cha Ngazi ya Wataalamu
pia kimehudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba,
Mhe. Humprey Polepole na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis
Despaigne Vera.
Tanzania na Cuba
zilianzisha ushirikiano wa kidiploamsia mwaka 1962 mara baada ya uhuru wa
Tanzania na mwaka 1986 zilisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano ya
kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika uchumi, sayansi na ushirikiano
katika masuala ya kitaalamu.
|
Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Naomi Mpemba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, akifungua kikao cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kilichafanyika kwa njia ya mtandao tarehe 30 Oktoba, 2024 katika ngazi ya wataalamu. Pembeni yake ni Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi. |
|
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kikao |