Thursday, November 29, 2018

Dkt. Mahiga akutana na Viongozi kutoka Norway, Denmark, Venezuela na China

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wa pili kutoka kushoto ukiwa katika mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam leo. Viongozi hao walijadili namna ya kukuza na kuimarisha ushirikiano hususan wa kibiashara ikiwemo mchakato wa kampuni ya Equinor wa kuzalisha gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kusafirisha nje ya nchi.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup wa pili kutoka kulia akisisitiza jambo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wa pili kutoka kushoto akiongea wakati wa mkutano wake na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup. Wengine katika picha kutoka kulia ni Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Magabilo Murobi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas Nyamanga na Afisa Dawati, Bi. Tunsume Mwangolombe


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiagana na mgeni wake, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup baada ya kufanya mazunguzmo ambayo yalikuwa ya mafanikio makubwa katika mustakabali wa Tanzania na Norway.


Picha ya pamoja.

Mazungumzo na Mhe. Zhui Yuxiao, Balozi anayesimamia masuala ya Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC)



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amekutana na Balozi Zhui Yuxiao, Mwakilishi kutoka China anayesimamia masuala ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Wawili hao walijadili utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC uliofanyika Beijing mwezi Agosti 2018.  Wamekubaliana kuundwa kwa kamati ya utekelezaji ambayo itaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ambapo Wizara imetakiwa pia kuteua mtumishi mmoja mwandamizi awe mratibu wa masuala ya FOCAC.
Balozi Zhui Yuxiao, Mwakilishi kutoka China anayesimamia masuala ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga. Mwingine ni Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wang Ke.
Picha ya pamoja.

Mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga katikati akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura hayupo pichani. Wengine ni Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Magabilo Murobi na Afisa Dawati, Bi. Lillian Kimaro.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura katikati akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga. Mhe. Naibu Waziri pamoja na mambo mengine ameleta ujumbe kuwa Venezuela inataka kufungua ofisi ya ubalozi nchini jambo ambalo Mhe. Mahiga amelikaribisha kwa mikono miwili na kueleza kuwa endapo Venezuela itafungua ubalozi itakuwa nchi ya nne kutoka Latin Amerika kuwa na ofisi ya Ubalozi Tanzania.
Ujumbe wa Venezuela wa kuomba kufungua ubalozi nchini.
Picha ya pamoja 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiagana na mgeni wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wa pili kutoka kushoto ukiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen. Katibu Mkuu alikuja kupata ufafanuzi kuhusu masuala ya haki za binadamu na kuihakikishia Tanzania kuwa haijasitisha msaada wake kwa Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea wakati wa mkutano wake na Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen. Wengine katika picha kutoka kulia ni Katibu wa Mhe. Waziri, Bw. Magabilo Murobi na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas Nyamanga.
Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen wa kwanza kulia akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiagana na mgeni wake, Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen 
Mkutano na Waandishi wa Habari

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga baada ya kumaliza mazungumzo na wageni wake aliongea na waandishi wa habari ili kupitia kwao wananchi waweze kujua masuala yaliyojadiliwa kwa ajili ya manufaa ya nchi yao.
Baadhi ya wanahabari waliohudhuria mkutano na Mhe. Waziri.
Sehemu nyingine ya wanahabari.
Mkutano unaendelea

Wednesday, November 28, 2018

Matukio mbalimbali ya ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Bw. Jestas Nyamanga (kushoto) akizungumza na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ziara ya kikazi ya siku nne. 
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup amekutana na Kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) katika ofisi za Wizara hiyo leo. Mazungumzo yao yalihusu kukuza na kuimarisha ushirikiano hususan katika programu za kuboresha mifumo ya ukusanyaji fomu kodi Tanzania.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup  katikati akiendelea na mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji hayupo pichani. kushoto ni Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Elisabeth Jacobsen
Watumishi walioshiriki mazungumzo hayo, kushoto ni Bi. Tunsume Mwangolombe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa zinajadiliwa katika mazungumzo hayo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas Nyamanga.

Ziara katika Shirika la Reli Tanzania

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup akiwa katika Shirika la Reli Tanzania. Mhe. Waziri alienda katika Shirika hilo kutembelea wahandisi wa kike wanaofadhiliwa na Serikali ya Norway. Katika programu hiyo Serikali ya Norway ishafadhili wahandisi wa kike 506 kwa gharama ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 4.2 kwa kipindi cha miaka 8. Ufadhili huo umepunguza uwiano wa wahindisi wa kiume na wakike kutoka 1:27 kabla ya programu kuanza na kufikia 1:10 kwa sasa. 

Wahandisi wa kike ambao wapo katika mafunzo ya vitendo wakitoa maelezo ya shughuli wanazofanya katika Shirika la Reli Tanzania.



Ziara katika Viwanja vya Gymkhanas

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup akipiga mpira akiwa katika viwanja vya Gymkhanas. Mhe. Waziri alienda katika viwanja hivyo kujumuika na kuongea na watoto wa kike walioshindwa kumaliza masomo kwa sababu mbalimbali na kwa sasa Serikali ya Norway inatoa msaada wa fedha kwa ajili ya kuwafundisha watoto hao stadi za maisha. 

Baadhi ya watoto waliopo katika programu inayofadhiliwa na Norway ya kuwapatia stadi za maisha ijulikanayo Bonga Programu inayoendeshwa na Mfuko wa OCODE.






Tuesday, November 27, 2018

Dkt. Ndumbaro atembelea Chuo cha Diplomasia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (kulia) akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Bernard Archiula mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika chuo hicho. Mhe. Naibu Waziri aliweza kutembelea maeneo mbalimbali ya chuoni hapo pamoja na kufanya mkutano na Uongozi wa chuo na Wakufunzi. Katika mkutano huo, uongozi wa chuo pamoja na Wakufunzi walitumia fursa hiyo kumwelezea Dkt. Ndumbaro changamoto wanazokabiliana nazo chuoni hapo ikiwa ni pamoja na ufinyu wa majengo kulingana na mahitaji ya chuo na uchache na uchakavu wa miundombinu ya kufundishia.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri alitumia ziara hiyo kujua mikakati mbalimbali waliyojiwekea chuoni hapo ikiwa ni pamoja na dhamira ya kujenga majengo mapya ambayo ramani ya mchoro wa majengo hayo iliwasilishwa kwa Mhe. Naibu Waziri.

Kwa Upande wa Dkt. Ndumbaro alitumia fursa hiyo kuupongeza Uongozi pamoja na Wakufunzi wa chuo cha Diplomasia kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na changamoto wanazokumbana nazo. Aidha, alitoa rai kwa Uongozi wa Chuo pamoja na Wakufunzi wawe wabunifu zaidi. 
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Archiula akimwelezea jambo Dkt. Ndumbaro huku Naibu Mkurugenzi wa Masomo Prof. Kitojo Wetengere akisikiliza kwa makini.
Balozi Charles Sanga akisalimiana na Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro akisalimiana na mmoja wa wahasibu wa Chuo cha Diplomasia, Bw. Daniel Kaguo. 
Dkt. Ndumbaro akizungumza kwenye mkutanao na Uongozi pamoja na Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia hawapo pichani.
Sehemu ya watumishi wa Chuo cha Diplomasia wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro hayupo pichani alipokuwa akizungumza nao.
Sehemu ya Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia, wa kwanza kulia ni Katibu wa Naibu Waziri, Bw. Charles Faini
Mkutano ukiendelea
Dkt. Ndumbaro akionyeshwa na kuelezewa ramani yenye mchoro wa majengo ya kisasa yatakayo jengwa katika eneo la Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam  









Dkt. Ndumbaro akutana na Mwakilishi wa Aga Khan

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbarom (kulia) akimsikiliza Mwakilishi wa Mfuko wa Aga Khan nchini, Bw. Amin Kurji walipokutana katika Ofisi ndogo ya Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Novemba 2018.

Mazungumzo kati ya Dkt. Ndumbaro na Bw. Kurji yalijikita katika kujadili masuala ya ushirikiano na shughuli za maendeleo ambazo zimekuwa Mfuko wa Aga Khan nchini katika kuhudumia wananchi hususan katika sekta ya Afya na Elimu.

Mazungumzo yakiendelea

Dkt. Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Kurji 
Dkt. Ndumbaro akiagana na Bw. Kurji mara baada ya kumaliza mazungumzo.


Watanzania wahimizwa kuchangamkia ajira za UN



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania wahimizwa kuchangamkia ajira za UN

Tanzania licha ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kuchangia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, lakini ajira za raia wake kwenye Sekretarieti ya Umoja huo ni ndogo mno.  Kauli hiyo ilitolewa leo na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Bi. Huda Hanina ambaye yupo nchini kwa ajili ya kutoa semina kwa Watanzania itakayowawezesha kuwa na ujuzi na mbinu za kuomba ajira katika Umoja wa Mataifa.

Semina hiyo inahusisha washiriki kutoka Vyuo Vikuu, vyombo vya ulinzi na usalama, Wizara na mashirika ya umma inafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam tarehe 26 hadi 28 Novemba 2018.

“Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani duniani na utendaji wa vikosi hivyo unajulikana na kila mtu, hivyo, Sekretarieti inapenda kuona raia wa kawaida wanaajiriwa ndani ya Umoja wa Mataifa ili watoe mchango kama unaotolewa na vyombo vya usalama”, Alisema  

Alieleza kuwa Umoja wa Mataifa una wanachama 193 kati ya hao, nchi ambazo raia wake wameajiriwa na Umoja huo ni 168 pekee ikiwemo Tanzania yenye watumishi 91 ambao ni chini ya nusu asilimia ya watumishi wote wa Umoja huo.

Bi. Hanina aliwasihi washiriki wa semina hiyo na Watanzania kwa ujumla kuingia katika Tovuti ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, https://careers.un.org ili kufuatilia ajira zinazotangazwa na kuangalia inayofaa kulingana na ujuzi mtu alio nao na kutuma maombi.

Alisisitiza umhimu wa kuandaa wasifu kulingana na sifa zilizoainishwa na nafasi husika. Alisema tatizo kubwa linalowakabili watu wengi wakiwemo Watanzania ni kuandaa wasifu unaokidhi viwango kulingana na kazi iliyotangazwa.  “Watu wengi wanaandaa historia badala ya wasifu, kitu ambacho sio sahihi. Kinachotakiwa ni kuandaa wasifu ambao unaainisha ujuzi na sifa zinazotakiwa katika kazi iliyotangazwa”. Alisema.

Washiriki wa semina hiyo wamehimizwa ujuzi waliopata wawafundishe Watanzania wengine ili katika kipindi kifupi kijacho Watanzania wengi waweze kuomba ajira na hatimaye kuajiriwa kwenye Umoja wa Mataifa.

Semina hiyo imekuja kufuatia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ofisi yake ya Uwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa jijini New York kufanya maombi maalum kwenye Umoja huo ya kuwapatia Watanzania mafunzo na mbinu za kupata ajira katika chombo hicho kikubwa duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
Tarehe 27 Novemba 2018

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu akitoa neno la ukaribisho  katika semina ya kuwajengea uwezo  Watanzania wakuwa na mbinu na ujuzi wa kuomba na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa.
Mwakilishi kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Bi. Huda Hanina akitoa somo kwa washiriki wa semina kuhusu ujuzi na mbinu za kuomba na kupata ajira katika Umoja wa Mataifa.
Sehemu ya washiriki wa semina kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wizara, wahitimu wa vyuo vikuu, Wizara na mashirikia ya umma wakisikiliza kwa makini somo lililokuwa linatolewa.
Semina inaendelea
Bi. Hanina akiendelea kutoa somo kwa Watanzania ili waweze kuwa na mbinu na ujuzi za kufanya maombi na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa.