Tuesday, November 27, 2018

Watanzania wahimizwa kuchangamkia ajira za UN



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania wahimizwa kuchangamkia ajira za UN

Tanzania licha ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kuchangia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, lakini ajira za raia wake kwenye Sekretarieti ya Umoja huo ni ndogo mno.  Kauli hiyo ilitolewa leo na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Bi. Huda Hanina ambaye yupo nchini kwa ajili ya kutoa semina kwa Watanzania itakayowawezesha kuwa na ujuzi na mbinu za kuomba ajira katika Umoja wa Mataifa.

Semina hiyo inahusisha washiriki kutoka Vyuo Vikuu, vyombo vya ulinzi na usalama, Wizara na mashirika ya umma inafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam tarehe 26 hadi 28 Novemba 2018.

“Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani duniani na utendaji wa vikosi hivyo unajulikana na kila mtu, hivyo, Sekretarieti inapenda kuona raia wa kawaida wanaajiriwa ndani ya Umoja wa Mataifa ili watoe mchango kama unaotolewa na vyombo vya usalama”, Alisema  

Alieleza kuwa Umoja wa Mataifa una wanachama 193 kati ya hao, nchi ambazo raia wake wameajiriwa na Umoja huo ni 168 pekee ikiwemo Tanzania yenye watumishi 91 ambao ni chini ya nusu asilimia ya watumishi wote wa Umoja huo.

Bi. Hanina aliwasihi washiriki wa semina hiyo na Watanzania kwa ujumla kuingia katika Tovuti ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, https://careers.un.org ili kufuatilia ajira zinazotangazwa na kuangalia inayofaa kulingana na ujuzi mtu alio nao na kutuma maombi.

Alisisitiza umhimu wa kuandaa wasifu kulingana na sifa zilizoainishwa na nafasi husika. Alisema tatizo kubwa linalowakabili watu wengi wakiwemo Watanzania ni kuandaa wasifu unaokidhi viwango kulingana na kazi iliyotangazwa.  “Watu wengi wanaandaa historia badala ya wasifu, kitu ambacho sio sahihi. Kinachotakiwa ni kuandaa wasifu ambao unaainisha ujuzi na sifa zinazotakiwa katika kazi iliyotangazwa”. Alisema.

Washiriki wa semina hiyo wamehimizwa ujuzi waliopata wawafundishe Watanzania wengine ili katika kipindi kifupi kijacho Watanzania wengi waweze kuomba ajira na hatimaye kuajiriwa kwenye Umoja wa Mataifa.

Semina hiyo imekuja kufuatia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ofisi yake ya Uwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa jijini New York kufanya maombi maalum kwenye Umoja huo ya kuwapatia Watanzania mafunzo na mbinu za kupata ajira katika chombo hicho kikubwa duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
Tarehe 27 Novemba 2018

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu akitoa neno la ukaribisho  katika semina ya kuwajengea uwezo  Watanzania wakuwa na mbinu na ujuzi wa kuomba na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa.
Mwakilishi kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Bi. Huda Hanina akitoa somo kwa washiriki wa semina kuhusu ujuzi na mbinu za kuomba na kupata ajira katika Umoja wa Mataifa.
Sehemu ya washiriki wa semina kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wizara, wahitimu wa vyuo vikuu, Wizara na mashirikia ya umma wakisikiliza kwa makini somo lililokuwa linatolewa.
Semina inaendelea
Bi. Hanina akiendelea kutoa somo kwa Watanzania ili waweze kuwa na mbinu na ujuzi za kufanya maombi na kupata ajira kwenye Umoja wa Mataifa.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.