Monday, November 26, 2018

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway kutua Tanzania


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

VIONGOZI WA NCHI MARAFIKI WAENDELEA KUTEMBELEA TANZANIA WAKIONGOZWA NA WAZIRI WA MAENDELEO YA KIMATAIFA WA NORWAY

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 27 hadi 30 Novemba 2018.

Wakati wa ziara yake nchini, Waziri huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ratiba ya Waziri huyo itahusisha pia mikutano na viongozi wengine wa Serikali wakiwemo Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Phillip Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango na Bw. Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mikutano hiyo itajadili namna ya kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Norway hususani kwenye maeneo ya ukusanyaji wa mapato, mazingira, nishati na kilimo.
Mheshimiwa Waziri Astrup pia atatembelea Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme inayofadhiliwa na Serikali ya Norway ikiwemo iliyoanzishwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mtambo wa kuzalisha umeme wa maji uliojengwa na Norway, Sweden na Finland kwenye miaka ya 1990 na kukarabatiwa hivi karibuni na Serikali ya Norway. Kwenye ziara mkoani Tanga, Waziri huyo ataambatana na Mhe. Subira Mgalu (Mb), Naibu Waziri wa Nishati.
Vilevile, Waziri huyo pamoja na Mhe. Omary Mgumba (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo watatembelea maghala na mtambo wa kuhifadhi mbolea uliopo karibu na Bandari ya Dar es Salaam, unaomilikiwa na kampuni ya Yara kutoka Norway ambapo Waziri kutoka Norway atasaini makubaliano na uongozi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambapo Norway itasaidia Programu inayoitwa Farm to Market Alliance (FtMA) iliyo chini ya WFP.
Ratiba ya Waziri huyo itahusisha pia hafla itakayojumuisha watanzania waliowahi kusoma na kufanya kazi nchini Norway. Akiwa ni mmoja wa viongozi waliosoma nchini Norway, Mhe. Job Y. Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Tanzania atakuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo inayotegemewa kuhusisha washiriki wapatao 400.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kufanya ziara nchini kati ya tarehe 27 na 30 Novemba 2018 ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Gorge Arreaza tarehe 29 Novemba 2018, Katibu Mkuu anayesimamia maendeleo na ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Dernmark, Bw. Trine Rask tarehe 28 hadi 30 Novemba 2018 na Mkurugenzi anayesimamia nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugon- Moulin tarehe 27 hadi 29 Novemba 2018. Ziara hizi zinalenga kuongeza wigo wa ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo rafiki.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 26 Novemba 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.