Sehemu ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakinukuu taarifa kutoka kwa Mhe. Dkt. Ndumbaro (hayupo pichani) |
Sehemu nyingine ya wanahabari wakiwajibika |
Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa kuhusu ziara ya ujumbe wa Makampuni ya uwekezaji kutoka Uturuki iliyokuwa ikitolewa na Mhe. Dkt. Ndumbaro (hayupo pichani) |
Mkutano ukiendelea |
Mhe. Naibu Waziri Dkt. Ndumbaro pamoja na Mhe. Balozi Davutoglu na wajumbe wengine akiwemo Bw. Nyamanga wakimsikiliza Bw. Mwamweta (hayupo pichani) akitoa utaratibu wa mkitano kabla ya mkutano kuanza |
Kabla ya kushiriki mkutano na waandishi wa habari Mhe. Dkt. Ndumbaro alikutana na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Davutoglu |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizungumza na Mhe. Balozi Davutoglu |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akimweleza jambo Mhe. Balozi Davutoglu huku mara baada ya kumaliza mkutano kati yake na waandishi wa Habari. Pembeni ni Bw. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika |
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiagana na Mhe. Balozi Davutoglu |
Mhe. Balozi Davutoglu akibadilishana mawazo na Bw. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika pamoja na Bw. Mwamweta mara baada ya mkutano kati ya Dkt. Ndumbaro na waandishi wa habari kumalizika ======================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU ZIARA YA UJUMBE WA MAKAMPUNI
MAKUBWA YA UWEKEZAJI KUTOKA UTURUKI HAPA NCHINI
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas
Ndumbaro ameipongeza Serikali ya Uturuki kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano
na Serikali ya Tanzania hususan katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii.
Mhe.
Dkt. Ndumbaro ametoa pongezi hizo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika kwenye
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es
Salaam tarehe 18 Novemba 2018 kuhusu ziara ya ujumbe wa Makampuni 7 makubwa ya
uwekezaji kutoka Uturuki.
Mhe.
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa, ziara ya ujumbe huo nchini ambayo itafanyika
kuanzia tarehe 18 hadi 24 Novemba 2018 ni mwendelezo wa jitihada za Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania
nchini Uturuki na wadau mbalimbali katika kutekeleza diplomasia ya uchumi
ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kwenye kutafuta na kuleta wawekezaji
wenye nia ili wawekeze katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kukuza
uchumi na kuinua kipato cha wananchi.
Akielezea
ziara hiyo, Dkt. Ndumbaro alieleza kuwa, ujumbe wa wawekezaji kutoka Makampuni
hayo ya Uturuki hapa nchini utatembelea mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na
Simiyu. Alisisitiza kwamba ujumbe huo umechagua mikoa hiyo kwa malengo mahsusi ya kuwekeza katika sekta ya viwanda
ikiwemo Kiwanda cha nguo, kiwanda cha sukari, kiwanda cha saruji, kiwanda cha vifaa
vya ujenzi, kiwanda cha kuongeza thamani bidhaa na uwekezaji kwenye sekta ya
nishati kwa mkoa wa Simiyu.
Aidha,
kwa mkoa wa Dodoma ujumbe huo una nia ya kuwekeza katika ujenzi wa maduka
makubwa (shopping malls), ujenzi wa majengo mbalimbali (real estate) na ujenzi
wa hoteli zenye hadhi ya kimataifa.
“Tunaishukuru
kwa dhati kabisa Uturuki kwani imekuwa nchi ya kwanza kutekeleza azma ya
Serikali ya kuhamia Dodoma kwa kuonesha nia thabiti ya kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali mkoani humo ikiwemo maduka makubwa ya biashara (shopping malls) na
hoteli za kimaifa zenye hadhi ya nyota tano” alisema Dkt. Ndumbaro.
Mhe.
Dkt. Ndumbaro aliongeza kusema kuwa, ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki
umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na jitihada zinazofanywa na
Serikali ikiwemo kusainiwa kwa mikataba mbalimbali ya ushirikiano, kuboreshwa
kwa mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini na ufunguzi wa Balozi. Alieleza
kuwa, kutokana na jitihada hizo Kampuni nyingi za Uturuki zimeonesha nia na
shauku ya kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini.
“Takwimu
zinaonesha kwamba kutoka mwaka 1990 hadi mwezi Septemba mwaka 2018 jumla ya
Kampuni 48 za Uturuki zimewekeza Tanzania. Uwekezaji huo unathamani ya Dola za
Kimarekani milioni 324.46 na umezalisha ajira 3,455 kwa Watanzania katika
maeneo mbalimbali” alisema Dkt. Ndumbaro.
Akizungumzia
biashara kati ya Tanzania na Uturuki, Mhe. Dkt. Ndumbaro alieleza kuwa imeimarika
kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na miaka kadhaa
iliyopita.
Mhe.
Dkt. Ndumbaro alieleza kuwa awali Tanzania ilikuwa ikiingiza zaidi bidhaa
kutoka Uturuki kama zana za kilimo, bidhaa za ujenzi, nguo na bidhaa mbalimbali
za plastiki. Hata hivyo, mwaka 2017 kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa Tanzania
kuuza zaidi bidhaa zake Uturuki kama pamba, mbegu za mafuta, korosho na tumbaku
kuliko Uturuki ilivyouza bidhaa zake Tanzania.
“Kwa
mfano wakati bidhaa zilizouzwa Tanzania kutoka Uturuki zikiwa na thamani ya
shilingi bilioni 6.091 tu, Tanzania iliuza bidhaa Uturuki zenye thamani ya
Shilingi bilioni 154.749. Mabadiliko haya chanya yamechochewa na sababu
mbalimbali ikiwemo juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki na
Sekta Binafsi ya Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko
zinazojitokeza Uturuki” aliongeza Dkt. Ndumbaro.
Mhe.
Naibu Waziri alisema kuwa ujumbe wa Makampuni hayo makubwa kutoka Uturuki ni
fursa muhimu kwa Tanzania hususan kwenye mikoa ambayo yameonesha nia ya
kuwekeza. Aliongeza kuwa uwekezaji utakaofanywa na Makampuni hayo utatoa fursa
kubwa kwa Watanzania ambapo inakadiriwa takribani ajira 1,400 zitatolewa na
Makampuni hayo.
Kabla
ya kuelekea Dodoma na Simiyu kwa ajili ya kuendelea na ziara, wawekezaji hao,
watafanya mkutano na wadau muhimu wa masuala ya uwekezaji jijini Dar es Salaam ambao ni; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara, wenye
Viwanda na Wakulima (TCCIA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya
Ukanda Maalum wa Uwekezaji Tanzania (EPZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mkutano
kati ya Dkt. Ndumbaro na Waandishi wa Habari ulihudhuriwa pia na Balozi wa
Uturuki hapa nchini, Mhe. Ali Davutoglu ambaye nae alisisitiza nchi yake kuendelea
kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji, utalii na
biashara ili kuzililetea maendeleo nchi hizi mbili.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam.
18 Novemba 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.