Friday, November 2, 2018

Dkt. Ndumbaro ashiriki Mkutano wa nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiwa kwenye Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) unaofanyika Durban, Afrika Kusini  kuanzia tarehe 2 Novemba,  2018. Mhe. Dkt. Ndumbaro anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo ambao pamoja na mambo mengine nchi hizo zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyo chini ya maeneo tisa vipaumbele kwa IORA ambayo ni usalama na ulinzi wa bahari; biashara na uwekezaji; usafiri wa bahari; uvuvi; menejimenti ya udhibiti wa majanga; taaluma, sayansi na teknolojia; utalii na utamaduni; uchumi bahari; na uwezeshaji wanawake. Mwingine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi
Mkutano ukiendelea
Picha ya pamoja ya Mawaziri
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan M. Mwinyi (kushoto) akijadiliana jambo na mmoja wa wajumbe wakati wa Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA). Balozi Mwinyi aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha 20 cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kilichofanyika tarehe 31 Oktoba na tarehe 01 Novemba, 2018.

===================================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi unaofanyika Durban, Afrika Kusini leo tarehe 2 Novemba,  2018
Mkutano huu umetanguliwa na Kikao cha 20 cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba, 2018 ambapo ujumbe huo uliongozwa na Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Jumuiya ya nchi za mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association – IORA) ilianzishwa mwaka 1997 awali, ikijulikana kama Indian Ocean Rim Association for Regional Cooperation IORA-AC kabla ya kubadilishwa kuwa IORA mwaka 2013. Jumuiya hii inaundwa na nchi wanachama 21 ambazo ni Afrika Kusini, Australia, Bangladesh, Comoro, India, Indonesia, Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Malaysia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Singapore, Somalia, Sri Lanka, Sultani ya Oman, Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Yemen. Tanzania ni moja kati ya nchi waanzilishi wa Jumuiya hii.
Katika muundo wake, IORA pia ina washirika wa mazungumzo (Dialogue Partners) saba (7) ambao ni Jamhuri ya Watu wa China, Japan, Marekani, Misri, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambao hushiriki katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Jumuiya.
Katika uongozi, Afrika Kusini ndie Mwenyekiti wa sasa wa IORA akisaidiana na Umoja wa Falme za Kiarabu kama Makamu Mwenyekiti. Hivyo, Mheshimiwa Lindiwe Sisulu (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Kusini aliongoza mkutano huu.
Lengo kuu la IORA ni kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi. Ikumbukwe kwamba Bahari ya Hindi ni eneo muhimu sana kiuchumi, kirasilimali, kiusalama pamoja na maendeleo kwa ujumla.
Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2001 inaelekeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ishirikiane na nchi jirani, za mbali na zenye malengo mema katika sura za kikanda, kimataifa na pande mbili kwa manufaa yetu. Huu ndio msingi wa Tanzania kuendelea kushiriki katika IORA kwani inatusaidia kujenga mahusiano yanayolenga kukuza uchumi; tunapata fursa ya kutangaza na kuvutia uwekezaji katika uchumi bahari (blue economy); na tunashiriki katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya kikanda ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Vilevile, kupitia IORA tunashiriki katika mfumo wa kupeana taarifa za kibiashara (IORA Trade Repository); kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukuza biashara ndogo na za kati (SMEs); pamoja na kushirikiana kwenye kulinda usalama katika Bahari ya Hindi.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huu wa 18 wa Mawaziri umeridhia  maombi ya nchi za Maldives na Myanmar kujiunga uanachama wa IORA.  Vilevile, Mawaziri wamekubali maombi ya nchi za Uturuki na Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) kuwa Washirika wa Mazungumzo
Aidha, nchi mbalimbali wanachama ikiwemo Tanzania wameahidi kuendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyo chini ya maeneo tisa vipaumbele kwa IORA ambayo ni usalama na ulinzi wa bahari; biashara na uwekezaji; usafiri wa bahari; uvuvi; menejimenti ya udhibiti wa majanga; taaluma, sayansi na teknolojia; utalii na utamaduni; uchumi bahari; na uwezeshaji wanawake.
Jumuiya hii ni fursa nyingine muhimu sana kwa Tanzania kwa kuwa ina malengo mazuri yenye maslahi kwa nchi na Ukanda kwa ujumla. 
 Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikiDodoma.
02 Novemba, 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.