Friday, November 30, 2018

Wadau wa maendeleo wana imani na Tanzania, Dkt. Mahiga

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wadau wa maendeleo wana imani na Tanzania, Dkt. Mahiga

Ziara zinazofanywa nchini na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi ni ishara ya wazi kuwa nchi rafiki na wadau wengine wa maendeleo wana imani kubwa na Tanzania.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi nne kutoka Ulaya na Amerika Kusini kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere tarehe 29 Novemba 2018.

Viongozi hao ni Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Yuri Pimentel Moura; Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo na Ushirikiano kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, Bi. Trine Rask Thygesen; Mjumbe kutoka China, Balozi Zhui Yuxiao, anayesimamia masuala ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na Mkurugenzi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugou-Moulin ambaye alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.

Wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Dkt. Mahiga alieleza kuwa, licha ya Tanzania na Norway kuwa na uhusiano mzuri na imara wa kidiplomasia, kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya nchi zote mbili. Dkt. Mahiga alitoa wito kwa Serikali ya Norway kushawishi sekta binafsi ya nchi hiyo kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Alisema kuna kampuni 33 za kutoka Norway nchini Tanzania ikiwemo kampuni ya Equinor ambayo ipo katika mchakato wa kuwekeza katika gesi asilia mkoani Lindi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kusafirisha nje. “Uwekezaji huu ni mkubwa na unahitaji ardhi kubwa ambayo ishapatikana na utakapokamilika utatoa ajira za maelfu kwa vijana wa Kitanzania”. Balozi Mahiga alisema.

Balozi Mahiga aliishukuru Norway kwa misaada ya kimaendeleo inayoipatia Tanzania ikiwemo ya kusaidia kufanya mabadiliko ya kimfumo katika masuala ya ukusanyaji kodi, miundombinu, nishati ya umeme na mbolea.
Aidha, Norway inafadhili mafunzo ya vitendo kwa wahandisi wa kike ili waweze kuwa na sifa ya kusajiliwa na Bodi ya Usajili ya Wahandisi. Kutokana na ufadhili huo ambao kwa miaka minane iliyopita umegharimu Shilingi bilioni 4.2 na kuwezesha wahandisi wa kike 504 kusajiliwa na kupunguza pengo kubwa la uwiano la wahandisi wa kike na kiume ambapo uwiano wao kabla ya ufadhili huo ulikuwa ni 1:27 na sasa ni 1:10.

Waziri huyo kutoka Norway alimdokeza Dkt. Mahiga kuwa Mfalme wa Norway ana panga kufanya ziara nchini Tanzania mwaka 2019.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, wawili hao walisisitiza umuhimu wa Tanzania na Venezuela kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi ambapo Venezuela imepiga hatua na sekta ya madini ambapo Venezuela ingependa kujifunza zaidi kutoka Tanzania. Ili kurahisisha utekelezaji wa mazaungumzo yao, Mhe. Naibu Waziri amewasilisha barua rasmi ya maombi ya nchi yake ya kufungua ofisi ya ubalozi nchini jambo ambalo Balozi Mahiga aliahidi litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Dernmark, Waziri Mahiga alijulisha kuwa Kiongozi huyo alitaka kupata ufafanuzi wa hali ya mambo yanavyoendelea nchini badala ya kutegemea taarifa za vyombo vya habari ambazo wakati mwingine zinakuwa sio sahihi. 

Baada ya ufafanuzi ambao ulimridhisha na hivyo kuihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa Denmark haijasitisha misaada kwa Tanzania. Ilielezwa kuwa misaada ambayo inakwenda moja kwa moja katika sekta ambayo ina thamani ya Dola za Marekani milioni 550 inaendelea kutolewa. Msaada unaokwenda kwenye bajeti ya Serikali moja kwa moja wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10 ambao mchakato wake umekamilika,  lakini kwa kawaida huwa unatolewa kwa pamoja na wadau wengine (Umoja wa Ulaya na Sweden) wanasubiriwa wakamilishe michakato yao ya ndani ili uweze kutolewa. Msaada huo kwa upande wa Sweden ni Dola milioni 9 na Umoja wa Ulaya ni Dola milioni 37.

Kuhusu mazungumzo na Balozi Zhui Yuxiao ambayo yalihusu mikakati ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC uliofanyika Beijing mwei Agosti 2018. Balozi Zhui alishauri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iteue mtumishi mmoja mwandamizi ili awe mratibu wa masuala ya FOCAC pamoja na kuteua kamati ya utekelezaji yenye wajumbe wa sekta mbali mbali lakini iratibiwe na Wizara ya Mambo ya Nje.

Kwa upande wa mazungumzo kati ya Dkt. Ndumbaro na Katibu Mkuu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugou-Moulin, wawili hao waliridhika na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zao ambao umedumu kwa miaka 98 tokea mwaka 1920.
Dkt. Ndumbaro alihimiza wawekezaji wengi zaidi kutoka Uswisi waje nchini kuwekeza kwa kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa kwa kiasi kikubwa. Alisema hakuna mabadiliko ya sheria za uwekezaji isipokuwa mabadiliko ambayo yamelenga kuboresha zaidi yamefanyika katika sheria ya madini. Hivyo, aliwataka wawekezaji wasiwe na hofu yeyote kuhusu Tanzania.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
Tarehe 30 Novemba 2018


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.