Thursday, June 25, 2020

MKUTANO WA MAWAZIRI WA KAMATI YA SADC YA ASASI YA USHIRIKIANO WA SIASA, ULINZI NA USALAMA KWA NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM


Mkutano wa Mawaziri wa Kamati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama kwa ngazi ya Makatibu Wakuu/ Maafisa Waandamizi umefanyika Jijini Dar es Salaam kwa njia ya Mtandao (Video Conferencing).

Mhimili wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC unaongozwa na mfumo wa Utatu (Troika) ambapo kwa sasa Mwenyekiti ni Zimbabwe, mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu unaofanyika leo ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 26 Juni 2020 chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Sibusiso Busi Moyo na utakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mambo ya Ndani, Ulinzi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka nchi wanachama wa SADC.

Pamoja na mambo mengine mkutano umepokea na kujadili agenda zinazohusu masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Ukanda wa SADC.
Mkutano wa leo umehudhuriwa na nchi wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, DRC,  Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Zambia, Zimbabwe na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ni moja ya mihimili ya SADC inayosimamia masuala ya Usirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Kanda. Mhimili huu unatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Mkataba wa uanzishwaji wa SADC wa mwaka 1992 na Itifaki ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ya mwaka 2001.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (katikati), kushoto kwake ni Katibu  Mkuu Wizara ya Ulinzi, Dkt. Faraji Mnyepe , mwisho kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Christopher Kadio wakifuatilia mkutano  huo kwa njia ya video conference, Jijini Dar es salaam




Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na baadhi ya Maafisa waandamizi kutoka Tanzania wakifuatilia mkutano huo kwa njia ya Video Conference, jijini Dar es Salaam

                                  Mkutano ukiendelea

NAIBU WAZIRI DKT. NDUMBARO AFANYA ZIARA KATIKA MIPAKA YA NCHI ILIYOPO MKOANI RUVUMA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) anaendelea na ziara ya siku sita (6) katika maeneo ya mipaka iliyopo mkoani Ruvuma. Mpaka sasa Dkt. Ndumbaro amefanya  ziara katika mpaka wa Wenje uliopo Wilayani Tunduru, Chiwindi uliopo Wilayani Nyasa na mpaka wa Magazini uliopo Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. Mipaka hii inaiunganisha Tanzania na Nchi jirani ya Msumbuji. 


Ziara hii ambayo inatokana na utekelezaji wa majukumu  ya Wizara, ikiwemo utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ,kujenga, kulinda na kudumisha uhusiano wa kimataifa, inalenga kuwahimiza watendaji na Mamlaka mbalimbali za Mkoa na Wilaya za Mipakani kuhusu umuhimu wa wakudumisha, kulinda, na kuendeleza uhusiano mzuri baina ya Taifa letu na nchi tunazo pakana nazo ili kustawisha biashara baina yetu na nchi tunazopakana nazo. Kadhalika, ziara hii inalenga kuhimiza umuhimu wa kulinda mipaka ya nchi na kubaini changamoto zinazowakabili wakazi wa mipakani. 

Aidha, kwa upande wake Dkt. Ndumbaro amewataka watendaji na Wakuu wa Wilaya hizo, kuendelea kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, vilele kutengeneza na kuanzisha masoko ya bidhaa mbalimbali maeneo ya karibu na mipakani kwa lengo la kuchagiza biashara, ajira na kuongeza mapato ya Serikali. "Wizara tumejipanga kutekeleza mkakati wa kuhakikisha kuwa tunashiriana kwa ukaribu na wadau wanaosaidia kutekeleza majukumu ya Wizara zikiwemo Mamlaka za Mikoa na Wilaya ambazo zipo mipakani" alisema Dkt. Ndumbaro

Wakati huo huo katika ziara hii Dkt. Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na kamati za ulinzi na usalama  katika Wilaya ya Namtumbo ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Sophia Mfaume, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tunduru ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Julius Mtatiro na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nayasa ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Isabela Chilumba. Wakuu wa Wilaya zote tatu pamoja Wakuu vya Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hizo kwa nyakati tofauti waliambatana na Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro kuzuru maeneo ya Mipakani.

Wananchi wa Tunduru kwa upande wao wameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki  kupitia Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zinazowakabili. Baadhi ya changamoto walizozitaja ni pamoja na kutokuwepo kwa huduma ya kivuko cha uhakika, barabara (kiwango cha lami) ukosefu wa huduma ya  maji safi na salama ya uhakika na umeme. Hata hivyo Dkt. Ndumbaro ameeleza  hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali  katika kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatuliwa.


Aidha, Wananchi wa Chiwindi, Wilayani Nyasa  wamemwomba Dkt. Ndumbaro kufikisha salaam na shukrani zao kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kuleta maendeleo nchini, na hasa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wa kipato cha chini. 

Dkt. Ndumbaro amezipongeza Mamlaka zilipo katika maeneo ya mipaka hiyo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kulinda mipaka, kudumisha mahusiano na nchi jirani na kwa kutekeleza kwa ufasaha dhana ya Diplomasia ya Uchumi licha ya changamoto zinazowakabili. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Sophia Mfaume, alipowasili Walayani hapo kwa lengo la kutembelea mpaka wa Magazini. Mpaka huu uliopo Wilayani humo unaiunganisha Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisalimiana na Katibu Tawala Bw. Adeni Nchimbi alipowasili katika Ofisi ya Wilaya hiyo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisaini kitabu cha wageni alipowalisi Ofisi za Makao Makuu ya Wilaya ya Namtumbo.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Sophia Mfaume akifungua Kikao kati ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb)
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Namtumbo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mamlaka mbalimbali wa Wilaya ya Namtumbo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akipolewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tunduru alipowasili katika Ofisi za Makao Makuu ya Wilaya hiyo. Akiwa Wilayani Tunduru Dkt. Ndumbaro ametembelea mpaka wa Wenje unaoiunganisha Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro akifungua Kikao kati ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb). 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akifafanua jambo alipokuwa akiongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tunduru.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tunduru. Mpaka wa Wenje uliopo Wilayani humo unaiunganisha Tanzania na Nchi jirani ya Msumbiji.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisikiliza risala kutoka kwa mwakilishi wa Wakazi wa Kijiji cha Wenje alipotembelea kijiji hicho kinachopakana na nchi jirani ya Msumbiji.  
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Wenje kilichopo Wilayani Tunduru, Ruvuma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Namtumbo. Mpaka wa Magazini uliopo Namtumbo unaiunganisha Tanzania na Nchi jirani ya Msumbiji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akinawa mikono kufuata kanuni na taratibu za kiafya, muhimu katika kujinga na maambukizi ya COVID-19 alipotembelea mpaka wa Wenje,Wilayani Tundu kama inavyoshauriwa na Wataalam wa Afya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe. Isabela Chilumba alipotembelea Wilaya hiyo. Akiwa Wilayani Nyasa  Dkt. Ndumbaro ametembelea Mpaka wa Chiwindi unaoiunganisha Tanzania na jirani ya Msumbiji. 
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe. Isabela Chiluba akifungua kikao kati ya Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Serikali ya Kijiji, Polisi wa upande wa Msumbiji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) kilifanyika mpakani Chiwindi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akivuka Mto unaoitenganisha Tanzania na Nchi jirani ya Msumbiji  
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyasa, wawakilishi wa Serikali ya Kijiji na Polisi wa upande wa Msumbiji katika kikao kilichofanyika mpaka wa Chiwindi, Nyasa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyasa, wawakilishi wa Serikali ya Kijiji na Polisi wa upande wa Msumbiji walropo mpakani hapo.

Wednesday, June 24, 2020

TANZANIA YAENDELEA KUZIOMBA TAASISI ZA FEDHA ZA KIMATAIFA KUSAMEHE MADENI NCHI ZINAZOENDELEA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akifuatilia mkutano wa Marais, Mawaziri Wakuu pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference) leo katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuziomba taasisi za fedha za kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya madola kufikiria kufuta kabisa madeni yaliyokopeshwa kwa nchi zinazoendelea ili fedha hizo ziweze kutumika kupambana na athari zilizotokana na Covid 19.

Ombi hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano wa Marais, Mawaziri Wakuu pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference) leo katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Prof. Kabudi amesema kuwa  Tanzania imesisitiza tena umuhimu wa mashirika ya fedha ya Kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya Madola zilizoikopesha Tanzania mbali na kutoa msamaha wa madeni waweze kufikiria kufuta kabisa madeni hayo ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kuwa na fedha za kuboresha mifumo ya afya, pamoja na kupambana na athari zilizotokana na janga la covid 19.

Katika mkutano huo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi za Jumuiya ya Madola na nchi zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na umoja na mshikamano katika kupambana na janga la Covid 19.

"Mkutano huu umekuwa ni mkutano muhimu sana katika jumuiya yetu ya madola na tumesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kushirikiana na kuwa na misaada na mipango madhubuti ya mashirika ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea katika jitihada zake za kuboresha na kujenga viwanda vyake hasa vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili inapotokea majanga kama haya ya covid 19 ziweze kuwa na dawa na vifaa tiba kwa wananchi wake," Amesema Prof. Kabudi

Ameongeza kuwa, nchi nyingi mara baada ya janga la covid 19 zilizuia utoaji wa dawa na vifaa tiba kwenda nje ya nchi kwa sababu dawa hizo walizihitaji kwa ajili ya matumizi yao wenyewe ndani ya nchi, na ndiyo maana nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (Sadc) tumeiomba India kwa upendeleo kutupatia dawa na vifaa tiba vya kukabiliana na janga la Corona.

Aidha, mkutano umejadili pia umuhimu wa teknolojia katika kupambana na Covid 19 na kuboresha mifumo ya afya na kwamba wakati umefika sasa teknolojia hiyo mahali popote ilipo ndani ya Jumiya ya Madola iweze kutolewa kwa nchi zote kwa gharama nafuu ili kuziwezesha nchi mbalimbali kutumia mifumo mipya ya kiteknolojia katika mifumo yake ya afya na kuziwezesha pia kupambana na Covid 19.

"Ni vizuri tuwe na mipango madhubuti na mikakati ya kupambana na aina hii ya majanga ambayo yanaweza kujitokeza siku za usoni na kufanya hivyo ni kuanza kujiandaa sasa kwa kuimaraisha huduma za afya katika nchi zetu," Amesema Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi ameongeza kuwa Tanzania imeanza jitihada hizo kwa kujenga hospitali nyingi za wilaya, mikoa pamoja na vituo mbalimbali vya afya na zahanati.

Mkutano umejadili, masuala mbalimbali ikiwemo, covid19, biashara, uchumi, viwanda, uwekezaji pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Mwezi April, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli aliiomba Benki ya Dunia pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa kuzisamehe madeni nchi zinazoendelea ili nchi hizo ziweze kutumia fedha hizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19).


Tuesday, June 23, 2020

SADC YAPITISHA MWONGOZO WA KIKANDA WA URAZINISHAJI (HARMONIZATION) NA UWEZESHAJI WA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI


Waziri wa Mamb ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari (hawaako pichani), kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge baada ya kumaliza kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano  (JNICC) jijini Dar es Salaam





Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya video umepitisha kwa kauli moja Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya SADC wakati huu wa janga la Corona.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine umepitia na kujadili masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la Corona ili kunusuru uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.
Mkutano huo pia umekubaliana kuwa na mpango wa pamoja wa kununua dawa, vifaa tiba na kinga kutoka nchini India na kuwa na hatua za pamoja za kukabiliana na ugonjwa wa COVID 19.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa  na Kikao cha Makatibu Wakuu ambao waliandaa nyaraka ambazo zilitumiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri na kufikia makubaliano hayo.
Mkutano huo umekutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


PROF. KABUDI AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI LA SADC



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Mollel (wa kwanza kushoto) Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Ijinia Isack Kamwelwe (katikati) wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC  unaofanyika kwa njia ya video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Wajumbe wa  Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kutoka Tanzania wakifuatilia mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Wajumbe wa  Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kutoka Tanzania wakifuatilia mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amefungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC na kuzitaka nchi wanachama kushirikiana na kuchukua hatua zinazotekelezeka katika kukabiliana na madhara yatokanayo na mlipuko wa janga la Virusi vya Corona.
 
Amesema changamoto zitokanazo na ugonjwa wa COVID 19 zipo wazi na zinazikabili nchi zote hivyo hazina budi kuungana na kutafuta suluhisho la pamoja ili  kunusuru uchumi na athari nyingine za kijamii.


Prof. Kabudi amesema ili kupata suluhisho la kudumu dhidi ya janga hilo Nchi za SADC  ni vyema zikashirikiana na Jumuiya nyingine za kikanda kama EAC na COMESA ili kuwa na miongozo na viwango vya pamoja katika kuendesha shughuli za usafirishaji wa binadamu, bidhaa na huduma huku hatua za kujikinga zikuichukuliwa. 


Amesema ni muhimu kwa nchi za SADC  kuzingatia miongozo ya wataalamu wa afya wakati zikiendesha biashara na usafirishaji wa bidhaa na huduma ili kulinda uchumi na kuondoa umasikini huku zikikabiliana na ueneaji wa janga la Corona.


Mkutano wa Baraza la Mawaziri umejadili utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Mawaziri dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa COVID 19, kupokea taarifa ya Mkutano wa Kamati ya Wataalamu ya SADC ya kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC uliofanyika tarehe 05 Juni 2020 na upendeleo utakaotolewa na India kwa nchi za SADC zitakaponunua dawa, vifaa kinga na vifaa tiba kwa ajili ya COVID 19.


Mkutano pia umepitia na kujadili Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya SADC pamoja na masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la CORONA ili kunusuru uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.


Mkutano huo umekutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.