Tuesday, June 23, 2020

SADC YAPITISHA MWONGOZO WA KIKANDA WA URAZINISHAJI (HARMONIZATION) NA UWEZESHAJI WA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI


Waziri wa Mamb ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari (hawaako pichani), kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge baada ya kumaliza kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano  (JNICC) jijini Dar es Salaam





Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya video umepitisha kwa kauli moja Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya SADC wakati huu wa janga la Corona.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine umepitia na kujadili masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la Corona ili kunusuru uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.
Mkutano huo pia umekubaliana kuwa na mpango wa pamoja wa kununua dawa, vifaa tiba na kinga kutoka nchini India na kuwa na hatua za pamoja za kukabiliana na ugonjwa wa COVID 19.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa  na Kikao cha Makatibu Wakuu ambao waliandaa nyaraka ambazo zilitumiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri na kufikia makubaliano hayo.
Mkutano huo umekutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.