Thursday, June 25, 2020

PROF. KABUDI AKUTANA, KUMUAGA BALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, amekutana na kumuaga Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Paul Sherlock ambaye amemaliza muda wake wa utumishi na amemtakia maisha mema na kumwambia kuwa ni matarajio yake kuwa atakuwa balozi mwema kwa Tanzania nchini Ireland na kwingineko duniani.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amesema kuwa Ireland imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya maendeleo, elimu, kilimo, afya pamoja na biashara na uwekezaji.

“Kupitia uhusiano imara kati ya Tanzania na Ireland hivi karibuni tulivyopatwa na janga la covid 19, Ireland imetoa msaada wa Euro milioni 1.5 ambapo baadhi ya fedha hizo zilipelekwa Shirika la Afya Duniani ofisi ya hapa Tanzania na Shirika la Chakula duniani ofisi ya hapa nchini kwa ajili ya kununua chakula lakini pia kwenda katika mfuko wa Benjamini Mkapa kwa ajili ya kuajiri wafanyakazi na kujenga vituo vya afya ili kutusaidia kupambana na Covid 19,” Amesema Prof. Kabudi.


Waziri Kabudi amemhakikishia Balozi Sherlock, kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ireland utaendelea kuimarika hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara, na kutoa wito kwa Serikali ya Ireland kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za kilimo, viwanda hasa vya nguo pamoja na ujenzi.  

Aidha, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia kwa miaka 40.

" Natumaini kuwa serikali ya Ireland kupitia uhusiano wake na Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo," amesema Balozi Sherlock.

Tanzania na Ireland zimetimiza miaka 40 ya uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Ireland ilipofungua ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1979.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Paul Sherlock wakati alipokuwa akimuaga katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidhi zawadi ya picha ya mlima Kilimanjaro Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock akimuonesha moja ya picha katika kitabu alichompatia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi kama zawadi  



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akimkabidi zawadi ya kitabu cha picha Balozi wa Ireland nchini, Mhe. Sherlock  



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.