Tuesday, June 23, 2020

MKUTANO WA DHARURA WA BARAZA LA MAWAZIRI WA SADC WAANZA DAR ES SALAAM


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifungua kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa waandamizi/ Makatibu Wakuu wa SADC kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongoza Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa waandamizi/ Makatibu Wakuu wa SADC katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe (katikati) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nziku (kulia) na Naibu Katibu Mkuu (Fedha za Nje) Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban, katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa waandamizi/ Makatibu Wakuu wa SADC kinachofanyika jijini Dar es Salaam

Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa waandamizi/ Makatibu Wakuu wa SADC wakifuatilia kikao hicho.



Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya Mtandao (Video Conferencing) unafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam  tarehe 23 Juni, 2020.

Mkutano huo umeanza kwa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa Waandamizi/ Makatibu Wakuu chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
  
Mkutano wa Baraza la Mawaziri utajadili utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Mawaziri dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa COVID 19, kupokea taarifa ya Mkutano wa Kamati ya Wataalamu ya SADC ya kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC uliofanyika tarehe 05 Juni 2020 na upendeleo utakaotolewa na India kwa nchi za SADC zitakaponunua dawa, vifaa kinga na vifaa tiba kwa ajili ya COVID 19.

Mkutano pia utapitia na kujadili Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji wa shughuli za usafirishaji ndani ya SADC pamoja na masuala ya uratibu, usimamizi na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia, ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la CORONA ili kunusuru uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi na unakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya kutoka nchi 16 wanachamawa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.