Saturday, March 6, 2021

PROF. KABUDI ATEMBELEA MIRADI YA KIMKAKATI INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI MKOANI KIGOMA

Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile iliyopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ili kuharakisha maendeleo ya maeneo hayo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi,  alipowaongoza Wajumbe wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mkoa wa  Kigoma.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Eneo  Maalum la Uwekezaji wa Kigoma (Kigoma Special Economic Zone-KiSEZ); Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Bandari Kavu ya Katosho na Bandari ya Kigoma pamoja  na Kituo cha Pamoja cha Kutoa huduma Mpakani (OSBP) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Manyovu mkoani Kigoma.

Akiwa kwenye eneo Maalum la Uwekezaji, Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye eneo hilo na Kampuni ijulikanayo kama Next Gen Solar wa kuzalisha umeme wa jua wa megawati tano ambao utaanza kusambazwa rasmi kwa wakazi wa Kigoma mwezi Aprili 2021. Upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo kiuchumi.

Kadhalika Mhe. Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walipata fursa ya kutembelea kampuni ya Third Man Limited inayozalisha Asali ijulikanayo kama Upendo (Upendo Honey) ambayo nayo imewekeza kwenye eneo hilo maalum la KiSEZ. Katika maelezo yake kwa Mawaziri, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Alex Scovic alisema kuwa Kampuni yake  ambayo inachakata asali inayozalishwa bila kutumia kemikali (organic) inanunua asali hiyo kutoka kwa wafugaji wa nyuki zaidi ya 3,000 waliopo Kigoma na mikoa jirani kama Tabora, Katavi, na Rukwa na baadaye kuiuza asali hiyo nje nchi hususan nchini Marekani.

“Kampuni yetu ni ya kwanza kuwekeza kwenye eneo hili. Tunazalisha Asali safi isiyo na kemikali ambayo ina soko kubwa nje ya nchi hususan nchini Marekani. Biadhaa zetu tunazitangaza kuwa zimetoka Tanzania” alisema.

Pia alijulisha kuwa, Kampuni yake imeajiri zaidi ya vijana 60 wa kitanzania na kwamba mbali na kuchakata asali, kampuni hiyo inazalisha nta ambayo huuzwa nchini Ujerumani ambao huitumia kwa ajili ya kutengeneza vipodozi. Kampuni ya upendo huzalisha zaidi ya tani 4,000 za asali kwa mwaka.

Katika ziara yao kwenye eneo la Bandari Kavu la Kitosho, Mawaziri na Viongozi wengine walijulishwa kuwa eneo hilo limeanzishwa maalum kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo na bidhaa mbalimbali zinazokwenda Burundi kutokea Bandari za Tanzania. Tayari eneo hilo limepata mzabuni atakayeanza ujenzi mwaka huu. Pia Mawaziri hao walitembelea Bandari ya Kigoma na kupata fursa ya kujionea meli kongwe na ya kihistoria ya MV Liemba ambayo ina miaka 108 tangu itengenezwe, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zote zitaanza kufanyiwa ukarabati ili kuziwezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Kigoma na kutoka nchi jirani.

Wakiendelea na ziara ujumbe huo ulitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo ulipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma kuwa, mradi huo unalenga kupanua na kukarabati maeneo mbalimbali ya Uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo awali ilikuwa na urefu wa mita 1800 na sasa mita 1,300 zitaongezwa ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Pia mradi unalenga kujenga jengo la abiria, maegesho ya ndege, usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, maegesho ya magari pamoja na uzio wa usalama.

Mhe. Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro walihitimisha ziara yao kwa kutembelea eneo kitakapojengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu na Mugina kwa upande wa Burundi. Wakiwa Manyovu waliweza kutembelea maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa kwa upande wa Tanzania na upande wa Burundi pamoja na kupokea taarifa ya mradi huo ambapo  walijulishwa kwamba tayari usanifu wa ujenzi wa kituo hicho cha Manyovu ambacho kitakuwa cha aina yake umeanza na utakamilishwa mwishoni mwa mwezi Machi 2021.

Akitoa hotuba kuhitimisha ziara kwenye miradi hiyo, Prof. Kabudi alisema Tanzania inawekeza kwenye miradi hiyo ili kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi mbalimbalii inazopakana nazo ikiwemo Burundi. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shingiro alipongeza jitihada hizo za Tanzania na kuahidi kutumia fursa za miradi hiyo ambayo mingi inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi,Mhe. Balozi Albert Shingiro wakimsikilizaMkurugenzi wa Eneo Maalum la Uwekezaji la Kigoma (KiSEZ), Bw. Omar walipotembelea eneo hilo ili kujionea miradi ya uwekezaji iliyopo. Ziara hiyoilifanyika tarehe 6 Machi 2021 ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha mkuatano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu uliofanyika kati ya Tanzania Burundi Mkoani Kigoma tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Mmoja wa Wataalam  katika kampuni ya kufua umeme wa jua ya ...akitoa maelezo kuhusu mitambo mbalimbali inayotumika kufua umeme huo.

Mtaalam wa umeme wa jua akitoa maelezo kwa Mhe. Prof. Kabudi  walipotembelea eneo maalum la uwekezaji ili kujionea mradi huo ambao ukikamilika utazalisha megawati 5 zitakazosambazwa kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Generali Wibert Ibuge akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye wakati waliposhiriki ziara ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kwenye maeneo mbalimbali.

Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho wakimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Asali ya Third Man Limited inayozalisha ijulikanayo kama Upendo, Bw. Alex Scovic  akifafanua kuhusu Kampuni yake ambayo imewekeza kwenye Eneo Maalum la Uwekezaji la Kigoma,

Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia Asali inayozalishwa na Kampuni ya Upendo

Mhe. Pfof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia mapipa ambayo hutumika kusafirisha Asali nje

Mhe. Prof. Kabudi akiangalia nta iliyokuwepo kwenye Kampuni ya Asali ya Upendo

Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakimsikiliza Mkurugenzi wa TANROAD-Kigoma, Mhandisi  Narcis Choma alipokuwa akitoa taarifa fupi kuhus ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma

Mhe. Prof. Kabudi akionesha eneo ambalo  mita 1300 za barabara ya kurushia na kutua ndege zitaongezwa 



Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja  na Mhe Balozi Shingiro wakiwasili kwenye eneo la Kitosho mjini Kigoma itakapojengwa Bandari Kavu kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha shehena mbalimbali zinazokwenda nchini Burundi kutokea Tanzania

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mhandisi Deusdedit Kakoko akitoa maelezo kuhusu Bandari Kavu hiyo 

Mawaziri wakimsikiliza Mhandisi Kakoko walipowasili kwenye Bandari ya Kigoma

Mhe. Dkt. Chamuriho naye akizungumza kuhusu masuala ya uchukuzi bandarini hapo

Mhe. Prof. Kabudi akisaini kitabu ca wageni mara baada ya kutembelea Meli Kongwe ya Mv Liemba. Meli hiyo ambayo ina historia ya muda mrefu ilitengenezwa mwaka 1913. Serikali inao mpango wa kuikarabati meli hiyo ili iendelee kutoa huduma kwenye Ziwa Taznganyika. Kulia ni Mhe. Dkt. Chamuriho na kushoto ni Nahodha wa Meli hiyo , Bw. Titus Mnyanyi

Nahodha Mnyanyi akitoa maelezo kuhus meli ya MV Liemba

Balozi Ibuge nae akisaini kitabi cha wageni kwenye Meli ya MV Liemba

Mhe. Prof.Kabudi akiwa kwenye chumba cha nahodha huku akionesha namna meli hiyo inavyoendeshwa

Mhe. Balozi Shingiro nae akijaribu usukani wa meli hiyo kongwe nchini

Waheshimiwa viongozi wakifurahia kuwa ndani ya meli hiyo yenye historia kubwa

Mhe. Prof. Kabudi akiwa ameongozana na Mhe. Balozi Shingiro wakiteremka kutoka kwenye Meli ya MV Liemba baada ya kutembelea meli hiyo

Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakisaini kitabu cha wageni walipowasili kwenye Ofisi za Forodha za Tanzaniazilizopo  katika eneo la Mpaka wa Manyovu. Mhe. Prof. Kabudi alifika eneo hilo kwa ajili ya kukagua mahali kitakapojengwa Kituo cha Pamoja cha Kutoa Huduma Mpakani /(OSBP)

Makatibu Wakuu wakiwa kwenye Ofisi za Forodha za Tanzania mpakani Manyovu

Mhe. Prof. Kabudi akionesha eneo ambalo Kituo cha OSBP kitajengwa

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Frank Mwega wakati wa ziara huko Manyovu

Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro wakivuka mpaka kuelekea Burundi kwa ajili ya kujionea eneo ambalo limetengwa na Serikali ya Burundi kwa ajili ya ujenzi wa OSBP

Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia jiwe ambalo ni mpaka kati ya Tanzania na Burundi

Hotuba

Picha ya pamoja ya viongozi wakionesha upande wa Tanzania

Picha ya viongozi wakiwa mpakani

Picha ya pamoja



 

Friday, March 5, 2021

TANZANIA NA BURUNDI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Tanzania na Burundi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya nchi hizo ulimalizika mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021.

Makubaliano yaliyofikiwa yamejikita kwenye maeneo kuimarisha sekta za siasa na mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama, maendeleo ya miundombinu, ushirikiano katika sekta ya uchumi na kijamii.

 Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wa watu wake kupitia jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine ikiwemo Burundi.

Ameongeza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza  mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi na kuinua maisha ya watanzania. Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeendelea kuwekeza na kuboresha sekta mbalimbali pamoja na kujenga miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219.

Alisisitiza mbali na jitihada hizo, upo umuhimu mkubwa wa Tanzania kushirikiana na nchi nyingine ikiwemo Burundi ili mafanikio haya yawe na tija zaidi kwa wananchi. “Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Magufuli imeendelea kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ili kukuza uchumi wa wananchi wake. itihada hizi haziwezi kufanikiwa kama Tanzania haitashirikiana na nchi nyingine na kama Tanzania haitawahimiza wananchi wake kuvuka mipaka na kufanya biashara na wenzao wan chi nyingine. Ni kwa msingi huo Mkutano huu wa Tume ya Pamoja ya kudumu una umuhimu mkubwa kwa nchi zetu mbili hususan kuingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali” alisisitiza.

Kadhalika alisema kuwa maeneo ya ushirikiano yaliyokubalika kwenye mkutano huo ni sehemu tu ya maeneo mengi muhimu ambayo Tanzania na Burundi zitaendelea kuyaibua kadri ushirikiano huo unavyoendelea.

“Kuna maeneo mengi sana ambayo nchi zetu zinaweza kushirikiana, ni dhahiri mpaka sasa hatujaweza kuzitumia fursa zote zilizopo. Tumeanza na sekta za ulinzi na usalama; biashara na uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi inayounganisha nchi hizi pamoja na masuala ya kijamii na tutaendelea kuvumbua maeneo mengine mapya ya ushirikiano kadri tunavyoimarisha ushirikiano huu” alisema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kuzihimiza sekta zinazohusika na usimamizi wa miradi ya kikanda ya miundombinu  inayotekelezwa na Serikali za Tanzania na Burundi chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiwemo  mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (260km) na Barabara ya Rumonge-Gitaza (45km)  na ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu/Mugina kutekeleza kikamilifu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Tanzania na Burundi.

Pia alitoa rai kwa watendaji wa Tanzania na Burundi kusimamia kikamilifu utelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ili mikutano ya tume iwe yenye tija.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu, Mhe. Balozi Albert Shingiro alisema nchi yake imedhamiria kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa na kutaja mkutano wa sita kama mwanzo mzuri wa kuendeleza ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Burundi.

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi umehitimishwa kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo matano ambayo ni Ushirikiano wa Kidiplomasia; Ulinzi na Usalama; Uendelezaji Miundombinu ya Usafirishaji; Elimu na Utamaduni na Biashara na Uwekezaji. Kadhalika Mkutano huo umeshuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chemba za Biashara za Tanzania na Burundi ukiwa na lengo la kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili.

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ambao umefanyika mjini Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021 umehudhuriwa na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na viongozi wengine waandamizi kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza kama Mwenyekiti wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya Mawaziri mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021. Wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje Burundi na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo Mhe. Balozi Albert Shingiro ( wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (wa pili kutoka kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Gen. Wilbert Ibuge (kulia)  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba (kushoto). Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam ulifanyika tarehe 3 na 4 Machi 2021.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro akizungumza wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika kwa ngazi ya mawaziri mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021

Balozi Ibuge nae akizungumza wakati wa mkutano sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya Mawaziri 

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akiwakaribisha Mkoani Kigoma Viongozi na Wajumbe walioshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ulifanyika kwa ngazi ya mawaziri 

Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakisaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo kadhaa yaliyojadiliwa na kukubalika wakati wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tannzania na Burundi

Mawaziri wakibadilishana Hati hizo baada ya kusaini

Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCA), Bw. Paul Koyi kwa pamoja na Kaimu Rais wa Chama cha Wafanyabiasha cha Burundi, Bw. Tharcisse Havyarimana (kushoto) wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kwenya masuala ya Biashara na Uwekezaji.

Sehemu ya Mawaziri na Makatibu wakuu na Viongozi wengine kutoka Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi uliofanyika kwa ngazi ya mawaziri tarehe 5 Machi 2021.

Sehemu nyingine ya Makatibu Wakuu wakifuatilia matukio mbalimbali ya mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Ujumbe wa Tanazania wakati wa mkutano
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Buhohela akitoa ratiba ya masuala mbalimbali yanayoendelea wakati wa mkutano wa sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Ujumbe wa Burundi

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Frank Mwega (kulia)  akiwa na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi

Mhe. Prof. Kabudi akimpatia Mhe. Balozi Shingiro zawadi ya picha ya michoro maarufu  ya Tingatinga zinazopatikana hapa nchini

Mhe. Prof. Kabudi akimbidhi Mhe. Balozi Shingiro Kamusi ya Kiswahili ili kumwezesha kuendelea kuongeza msamiati wa Kiswahili ikiwa ni Lugha iliyokubalika kufundishwa nchini Burundi.

Mhe. Balozi Shingiro akimkabidhi Mhe. Prof. Kabudi zawadi ya kikapu  kinachotambulisha utamaduni wa Burundi 

Makatibu Wakuu  nao wakipeana zawadi ambapo Balozi Ibuge anaonekana akimkabidhi Mhe. Ntirampeba zawazi ya Kamuzi ya Kiswahili

Mhe. Ntirampeba nae akikabidhi zawadi kwa Balozi Ibuge

Viongozi wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja

Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jillyy Maleko ( wa tatu kushoto waliosimama)

Meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi

Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja naMhe. Balozi Shingiro wakifurahia kikundi cha ngoma maarufu kama Mapigo Tisa cha mkoani Kigoma kilichotumbuiza wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi