Monday, December 6, 2021

Matukio katika Ufunguzi wa Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali wa Afrika Mashariki

    Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kushoto akiwa katika banda la Serikali ya Tanzania kupata maelezo kuhusu Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali ya Afrika Mashariki. Wengine katika picha kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Mhe. Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wwenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Peter Mathuki.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba 2021.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) na ujumbe wake wakielekea kwenye mabanda ya wajasiliamali wanaoshiriki kwenye Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba 2021. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) 
akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na wajasiliamali kwenye Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba 2021.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akiwa kwenye Banda la Vijana wa CCM mkoa wa Mwanza linalouza bidhaa za CCM kwenye Maonesho ya 21 ya Wajasiliamali ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba 2021. 


Bidhaa mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu zilizobuniwa na wajasiliamali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akiwa katika vazi la utamaduni la Sudan Kusini alilovalishwa baada ya kuwasili kwenye banda la nchi hiyo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akikabidhiwa zawadi ya picha yake ya kuchora katika moja ya mabanda ya Watanzaia.



 

Sunday, December 5, 2021

Wajasiriamali Wahimizwa Kutengeneza Bidhaa zenye Ubora


Na Mwandishi Maalum, Mwanza

Wajasiriamali wametakiwa kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kudhibiti soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hatimaye Afrika nzima, hususan katika kipindi hiki Bara la Afrika limeanzisha Soko Huru la Biashara (CfTA).

Hayo yamesemwa leo tarehe 4 Desemba 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya 21 ya wajasiliamali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemaba 2021.

“Nimetembelea mabanda ya wajasiriamali na kushuhudia bidhaa zenye ubora wa hali ya juu. Hivyo, tuendelee kuboresha bidhaa zetu ili tuingie masoko mengine badala ya kutegemea soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee”, Waziri Mhagama alisema.

Waziri Mhagama alitoa ahadi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Jumuiya, kuimarisha maonesho hayo ili yaweze kupanua soko, kuongeza ajira, kukuza uchumi na hatimaye kuondoa umasikini kwa raia wa nchi wanachama wa EAC.

Maonesho hayo ambayo yatafunguliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2021 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan yanapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo mafunzo kwa wajasiriamali yenye mada tofauti tofauti kama vile; vikwazo visivyo vya kibiashara, wepesi wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya, fursa za biashara katika nchi ya Sudan Kusini, UVIKO-19 na biashara na namna ya kusafirisha bidhaa baina ya nchi za Jumuiya.

Mada hizo zinazowasilishwa na wabobezi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zinazosimamia urasimishaji wa bidhaa, kwa siku ya tarehe 4 Desemba 2021, wajasiliamali wamejifunza falsafa ya Kaizen ambayo inahimiza umuhimu wa mjasiriamali kuboresha utendaji wake kila siku katika maeneo yote kama ya ubunifu, utafutaji wa masoko, vifungashio, utoaji wa huduma kwa mteja n.k.

Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Keneth Bagamuhunda alieleza namna maonesho hayo yanavyondelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kubainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na washiriki wamekuwa wengi zaidi ukilinganisha na miaka mingine.

Wajasiriamali zaidi ya 900 wanashiriki maonesho hayo wakiwemo 420 wa Kitanzania kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Aidha, viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudriki Soragha; Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na Ajira, Mhe. Patrobas Katambi; Waziri wa Jiji la Kampala, Hajatti. Minsa Kabanda; wabunge wanne kutoka Uganda waliungana na Mhe. Mhagama katika Siku ya Tanzania kwenye maoesho hayo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wajasiliamali wanaoshiriki maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa EAC jijini Mwanza.

Baadhi ya wajasiriamali wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akifurahi kufuatia Mkurugenzi wa Ajira katika Wizara yake ambaye pia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya Maonesho ya 21 ya wajasiriamali ya EAC, Bw. Ali Msaki (kulia) kukabidhiwa cheti kutokana na kuratibu vizuri maaandalizi hayo. Anayekabidhi cheti ni Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Sekretarieti ya EAC, Bw. Keneth Bagamuhunda.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Sekretarieti ya EAC, Bw. Keneth Bagamuhunda katika Banda la Sekretarieti ya EAC.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akisaini Kitabu cha Wageni katika Banda la Serikali ya Tanzania. Aliyesimama ni Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Semeni Nandonde.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama pamoja na wajasiriamali wakionesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa EAC.

Bidhaa zina viwango vizuri, hongereni sana wajasiriamali kwa kazi nzuri.

Wajasiriamali wanatengeneza hadi vitanda kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa katik hospitali zetu. 

Bidhaa zimefungashwa vizuri

Hongereni wajasiliamali kwa ubunifu wenu, hakika nchi za EAC zinasonga kwa kasi katika biashara na uwekezaji.

Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule (katikati) wakikamilisha jambo na maafisa wa Wizara hiyo, Bw. Hassan Mnondwa na Bi. Semeni Nandonde.

Burdani ni moja ya jambo linalofurahiwa na washiriki pamoja na wale wanaotembelea maonesho ya 21 ya wajasiriamali ya EAC jijini Mwanza.

Saturday, December 4, 2021

STAMICO, SUNESS LTD ZASAINI MKATABA WA MASHRIKIANO

Na Mwandishi wetu, Roma

Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) limesaini mkataba wa makubaliano ya awali na Kampuni ya Suness Limited ya Italia kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa Shaba katika Mkoa Kilimanjaro. Suness Limited ni kampuni ya Kiitaliano inayojishughulisha na uchimbaji madini na Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kushirikiana na STAMICO katika kuendeleza kwa pamoja mradi wa shaba.

Akiongea mara baada ya kusaini mkataba huo leo Jijini Roma Italia, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa mkataba umesainiwa kupitia jukwaa la biashara na uwekezaji lililofanyika Jijini Roma Italia tarehe 02 – 03 Disemba 2021.

Pamoja na mambo mengine, STAMICO wameweza kuelezea juu ya mradi wa mkubwa wa shaba unaopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo pia mwekezaji  ameonesha nia ya kuingia ubia na STAMICO.

“Shirika lina mradi wake mkubwa wa Shaba mkoani Kilimanjaro wenye kiasi kikubwa cha mashapu ya Shaba na kupitia jukwa la wafanyabiashara na uwekezaji lililofanyika Roma Italia, tumewaeleza juu ya mradi huo na wenzetu wameonesha kuvutiwa na mradi huo na tukakubaliana kusaini makubaliano ya awali na baadae watakuja Tanzania ili kwa pamoja twende kwenye eneo la mradi husika na mwishowe tuingie katika makubaliano ya pamoja ya kuendeleza mradi huo,” Amesema Dkt. Mwasse

Naye Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo amesema kuwa amefurahishwa na utiaji saini wa awali wa mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza kwa pamoja mradi wa Shaba

“Nimefurahia kuanza kwa makubaliano haya mapya ambayo yataleja matokeo chanya kati ya nchi ya Tanzania na Italia na naahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili katika sekta hii ya madini,” amesema Bw. Calo.

Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudiwa  na Naibu Waziri, Wizara ya Madini Mhe. Prof. Shukrani Manya, Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo, Mkurugenzi Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Zanzibar Classic Safaris, Bw. Yussuf Salim Njama.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse pamoja na Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo wakisaini mkataba wa makubaliano ya awali kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa Shaba katika Mkoa Kilimanjaro. Utiaji saini wa mkataba huo umeshuhudiwa  na Naibu Waziri, Wizara ya Madini Mhe. Prof. Shukrani Manya, Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo pamoja Mkurugenzi Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka Jijini Roma, Italia. 


Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse akibadilishana mkataba wa makubaliano ya awali kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa Shaba katika Mkoa Kilimanjaro na Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo mara baada ya kusainiwa wakisaini kwa mkataba huo leo Jijini Roma, Italia 


Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse pamoja na Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo wakionesha mkataba wa makubaliano ya awali kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa Shaba katika Mkoa Kilimanjaro na mara baada ya kusainiwa leo Jijini Roma, Italia 



Friday, December 3, 2021

JUKWAA LA KWANZA LA BIASHARA NA UWEKEZAJI LAFANYIKA ITALIA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Na Mwandishi wetu, Roma

Jukwaa la kwanza la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Jijini Roma kwa mafanikio makubwa, Italia na kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili hasa katika kipindi hiki cha Uviko 19.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Italia ambapo limendaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya ambapo Prof. Manya amewaeleza wawekezaji na wfanyabiashara kutoka Italia kuwa Tanzania kwa sasa imejikita kuwekeza katika miundombinu wezeshi ya uwekezaji, na kwamba hilo ndilo jambo ambalo Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Rais  Samia ameliweka suala la uwekezaji kama kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi wanawekeza fedha na mitaji yao ili kukuza biashara na ajira kwa watanzania na kuwezesha uchumi wa Tanzania kusonga mbele

“Tanzania inathamini uwekezaji na sasa inapiga hatua kwa kuweka miundombinu wezeshi pia Tanzania kama nchi tunamshukuru Mungu kwamba lengo la njozi yetu na maono yetu ya Tanzania Development Vision (2020-2025) imeweza kufikia malengo yake miaka mitano kabla muda uliokuwa umepangwa. Ambapo lengo kubwa lilikuwa ni kuifanya Tanzania kwenda katika viwango vikubwa vya kiuchumi na mwaka 2020 Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia kuingia katika Uchumi wa kati,” amesema Prof. Manya.

Kadhalika, Prof. Manya ameongeza kuwa katika miaka mitano inayokuja Tanzania inapoelekea kumaliza njozi yake, inatamani kuendelea kukuza uchumi na ikiwezekana ihame katika uchumi wa kati na kuhamia uchumi wa juu……na ndiyo maana imejikita kuwekeza katika miundombinu ya reli ya kati itakayotumika kusafirisha mizigo kwa umeme, ujenzi wa bwawa kubwa linaloweza kuzalisha umeme wa kutosha pamoja na barabara za kusafiri kutoka mashariki kwenda magharibi na kaskazini kwenda kusini.

Ameongeza kuwa Tanzania inajivunia kuwa na hali ya amani na utulivu na katika nchi za ukanda wa maziwa makuu Tanzania inajivunia kuwa na siasa safi yenye utulivu na amani ndani yake.

“Mfano tumeona mwekezaji aliyewekeza katika kilimo cha Pareto ameshuhudia kwa kusema kuwa Tanzania ni nchi ya amani na utlivu na kuwasihi Waitaliano kuja kuwekeza Tanzania,” ameongeza Prof. Manya.

Kupitia jukwaa hili, tunaamini kuwa litachagiza chachu ya uwekezaji zaidi nchini Tanzania na kukuza biashara kati ya Tanzania na Italia.

Mwitikio ni mkubwa na wameonesha utayari wa kuja kuwekeza zaidi Tanzania pamoja na kukuza biashara miongoni mwetu na tumewahahakikishia kuwa Tanzania ni sehemu salama na yenye mazingira mazuri ya Uwekezaji na wameahidi kuwekeza zaidi Tanzania.

Nae Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa Jukwaa la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania ili kukuza uchumi wa pande zote mbili.

“Mwitikio ni mkubwa sana na tumeitikiwa na Serikali ya Italia vizuri sana pamoja na jumuiya za Italia za kibishara na pia kwa upande wa Tanzania pia mwitikio ni mkubwa pia,” amesema Balozi Kombo.

Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji wa Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza, ni nchi ya amani, tulivu kwa uwekezaji, karibuni sana kuwekeza Tanzania,” amesema Bw. Rosso

Katika Jukwaa hilo, Kampuni mbalimbali za Kiitaliano zimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania ambazo ni pamoja na Kampuni ya utengenezaji Magari Ferari ambayo imeonesha utayari wa kuwekeza katika Gereji nchini Tanzania na Shirikisho la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu kutoka Italia pia limeonesha nia ya kuwekeza Tanzania.

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia Jijini Roma. Jukwa hilo limefanyika tarehe 2 na 3 Disema 2021 

 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma 


Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  







Thursday, December 2, 2021

WAWEKEZAJI ZAIDI YA 140 KUTOKA ITALIA WAWEKEZA TANZANIA

 Na Mwandishi wetu, Roma

Wawekezaji zaidi ya 140 kutoka Italia wamewekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania

Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Waziri Wizara ya Madini, Prof. Shukrani Manya alipokuwa akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma, Italia.

Prof. Manya amasema kuwa miradi hiyo inathamani ya Shilingi bilioni 5 inayotoa ajira kwa watanzania zaidi ya 4000.

“Jukwa hili tunataka liendelee kuwa sababu ya kuchagiza uwekezaji mwingine kutoka Italia kwa kutumia teknolojia waliyonayo, kwa kutumia utalaamu walionao wa 'designing'…….na sasa waone kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na Tanzania inaendelea kuweka mazingia wezeshe ya kukuza sekta ya uwekezaji na biashara,” Amesema Prof. Manya

Ameongeza kuwa kupitia jukwaa la biashara na uwekezaji biashara na uwekezaji utaendelea kuongezeka na kuongeza zaidi na hasa katika maeneo ambayo tumawaeleza hapa kupitia jukwaa hili.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa kongamano hili la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania.

“mwitukio ni mkubwa na tumeitikiwa na jumuiya za kibiashara na wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili wameshiriki katika kongamano hili,” amesema Balozi Kombo

Balozi Kombo ameongeza kuwa, Wafanyabiashara kutoka italia ni wabobezi katika sekta ya madini lakini pia katika utalii hivyo ni matumanini yake kuwa mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Italia wataongezeka zaidi Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza…..nawahakikishia mimi nimewekeza Tanzania na ninaona ni sehemu salama ya kuwekeza karibuni sana kuwekeza kwa maendeleo ya Tanzania na Italia,” amesema Bw. Rosso

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki katika jukwaa hilo kuwa CRDB ipo tayari kutoa mikopo kwa watakao kuwa tayari kuwekeza Tanzania.

“Nawahakikishia kuwa Benki ya CRDB itawawezesha mikopo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu mitaji ya kuwekeza ipo karibuni sana tuijenge Tanzania,” Amesema Bw. Nsekela.

Jukwa hilo la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji takribani 250 kutoka nchi zote mbili. Wafanyabiashara na wawekezaji hao ni wa sekta za utalii, kilimo, madini, na ujenzi.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


 

Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya akihutubia wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kushiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma 


Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara (hawapo pichani) walioshiriki Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Sekta ya Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso akiongea na Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mmoja wa Wafanyabiashara kutoka Italia akiongea na Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  


Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma  



Wednesday, December 1, 2021

KIKAO CHA FOCAC DAKAR KIMEKUWA CHA MAFANIKIO - BALOZI MULAMULA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza baada ya kumalzika kwa mkutano wa nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)

 


Na Mwandishi wetu, Dakar

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefanyika kwa mafanikio makubwa.

Balozi Mulamula ametoa kauli hiyo jijini Dakr nchini Senegal baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika Novemba 29 na 30 2021 nchini humo.

Amesema kikao hicho kimekuwa cha mafanikio kwani kimepitisha maazimio makubwa na mpango kazi ambao umejikita katika kutekeleza maeneo ya kimkakati ambayo yakisimamiwa kikamilifu yatazinufaisha nchi za Afrika .

Balozi Mulamula amesema kauli ya China ya kuzihakikishia nchi za Afrika kuwa itasaidia kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo za COVID 19 pamoja na dawa nyingine ni ya kujivunia na ya kupongezwa.

"Tanzania imefurahishwa na ahadi hiyo kwani jambo hilo litazifanya nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kuzalisha chanjo na dawa nyingine kwa ajili ya kuwalinda watu wake na kuacha kutegemea msaada., kauli ya Rais Jinping ni ya kujivunia na ya lupongezwa,"amesema Balozi Mulamula.

Amesema kikao kimekuwa na mafanikio zaidi kwani mbali na kuangalia maeneo ya siku zote ya kuendeleza miundombinu na viwanda, kwa mara ya kwanza umeangalia jinsi ya kusaidia na kuendeleza wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Amesema uamuzi wa China kwa kutoa kipaumbele katika eneo la kujenga viwanda vya kuzalisha dawa na chanjo na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ni wa kupongezwa mno kwani mambo hayo ndiyo ambayo Tanzania ilitilia mkazo katika taarifa yake na kuongeza kuwa wamefarijika kwamba Rais Jinping ameahidi kusaidia katika eneo hilo.

“Jambo hili ni zuri na kubwa sana, ni miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania iliyasemea, eneo hilo ndiko watu wengi walikopata ajira hasa akina mama na vijana tunaishukuru na kuipongeza China  kwa kutoa kipaumbeele katika eneo hilo”, alisema Mhe. Waziri.

Amesema kikao hicho pia kimeangalia maeneo ya kujengea uwezo wananchi wa Afrika katika eneo la ufadhili wa masomo ambalo kwa wakati huu limekwama kutokana na mlipuko wa virusi vya Covid 19 lakini wameahidi kuendelea nalo pale hali itakapotengemaa.

Ameongeza kuwa kikao pia kimeangalia suala la kuendeleza kilimo ili kuwa na kilimo cha kisasa na kuendeleza miundombinu ya kidijitali hasa nyakati hizi ambazo ni lazima kujiunganisha kidigitali ili kujikwamua  kiuchumi.

Amesema China imesisitiza na kuweka mkazo katika eneo la kundeleza kilimo ili kuziwezesha nchi za Afrika kujikwamua na umasikini na wameahidi kutoa fedha na kuleta wataalamu kwa ajili ya kuendeleza kilimo.

Mkutano huo wa siku mbili ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China uliangalia jinsi China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya miradi ya kimkakati na ukuzaji wa wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.