Sunday, December 5, 2021

Wajasiriamali Wahimizwa Kutengeneza Bidhaa zenye Ubora


Na Mwandishi Maalum, Mwanza

Wajasiriamali wametakiwa kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kudhibiti soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hatimaye Afrika nzima, hususan katika kipindi hiki Bara la Afrika limeanzisha Soko Huru la Biashara (CfTA).

Hayo yamesemwa leo tarehe 4 Desemba 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya 21 ya wajasiliamali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemaba 2021.

“Nimetembelea mabanda ya wajasiriamali na kushuhudia bidhaa zenye ubora wa hali ya juu. Hivyo, tuendelee kuboresha bidhaa zetu ili tuingie masoko mengine badala ya kutegemea soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee”, Waziri Mhagama alisema.

Waziri Mhagama alitoa ahadi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Jumuiya, kuimarisha maonesho hayo ili yaweze kupanua soko, kuongeza ajira, kukuza uchumi na hatimaye kuondoa umasikini kwa raia wa nchi wanachama wa EAC.

Maonesho hayo ambayo yatafunguliwa rasmi tarehe 5 Desemba 2021 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan yanapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo mafunzo kwa wajasiriamali yenye mada tofauti tofauti kama vile; vikwazo visivyo vya kibiashara, wepesi wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya, fursa za biashara katika nchi ya Sudan Kusini, UVIKO-19 na biashara na namna ya kusafirisha bidhaa baina ya nchi za Jumuiya.

Mada hizo zinazowasilishwa na wabobezi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zinazosimamia urasimishaji wa bidhaa, kwa siku ya tarehe 4 Desemba 2021, wajasiliamali wamejifunza falsafa ya Kaizen ambayo inahimiza umuhimu wa mjasiriamali kuboresha utendaji wake kila siku katika maeneo yote kama ya ubunifu, utafutaji wa masoko, vifungashio, utoaji wa huduma kwa mteja n.k.

Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Keneth Bagamuhunda alieleza namna maonesho hayo yanavyondelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kubainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na washiriki wamekuwa wengi zaidi ukilinganisha na miaka mingine.

Wajasiriamali zaidi ya 900 wanashiriki maonesho hayo wakiwemo 420 wa Kitanzania kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Aidha, viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi. Robert Gabriel Luhumbi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudriki Soragha; Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na Ajira, Mhe. Patrobas Katambi; Waziri wa Jiji la Kampala, Hajatti. Minsa Kabanda; wabunge wanne kutoka Uganda waliungana na Mhe. Mhagama katika Siku ya Tanzania kwenye maoesho hayo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wajasiliamali wanaoshiriki maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa EAC jijini Mwanza.

Baadhi ya wajasiriamali wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akifurahi kufuatia Mkurugenzi wa Ajira katika Wizara yake ambaye pia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya Maonesho ya 21 ya wajasiriamali ya EAC, Bw. Ali Msaki (kulia) kukabidhiwa cheti kutokana na kuratibu vizuri maaandalizi hayo. Anayekabidhi cheti ni Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Sekretarieti ya EAC, Bw. Keneth Bagamuhunda.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Biashara na Forodha wa Sekretarieti ya EAC, Bw. Keneth Bagamuhunda katika Banda la Sekretarieti ya EAC.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akisaini Kitabu cha Wageni katika Banda la Serikali ya Tanzania. Aliyesimama ni Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Semeni Nandonde.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama pamoja na wajasiriamali wakionesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa EAC.

Bidhaa zina viwango vizuri, hongereni sana wajasiriamali kwa kazi nzuri.

Wajasiriamali wanatengeneza hadi vitanda kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa katik hospitali zetu. 

Bidhaa zimefungashwa vizuri

Hongereni wajasiliamali kwa ubunifu wenu, hakika nchi za EAC zinasonga kwa kasi katika biashara na uwekezaji.

Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule (katikati) wakikamilisha jambo na maafisa wa Wizara hiyo, Bw. Hassan Mnondwa na Bi. Semeni Nandonde.

Burdani ni moja ya jambo linalofurahiwa na washiriki pamoja na wale wanaotembelea maonesho ya 21 ya wajasiriamali ya EAC jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.