Wednesday, December 8, 2021

TANZANIA YANADI BIDHAA ZA KILIMO NCHINI MAREKANI

Na Mwandishi Wetu,

Katika kusheherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 60 ya uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wake nchini Marekani imefanya Kongamano kwa njia ya Mtandao kuhusu biashara ya bidhaa za Kilimo za Tanzania.

Mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Taasisi za Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Sister Cities International na Thunderbird School of Global Management. Lengo la Kongamano hilo lilikua ni kuimarisha mauzo ya bidhaa za kilimo za Tanzania nchini Marekani.

Kongamano hilo lilishirikisha wajumbe kutoka Serikali za Tanzania na Marekani, Wafanyabishara na wadau wa kilimo wa nchi hizo mbili na Taasisi za Fedha, ambapo Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), ameshiriki kwenye Kongamano hilo, kadhalika, Meya wa Jiji la   Helena-West, Arkansas, Mstahiki Kevin Smith naye pia ameshiriki.

Wakati wa Kongamano hilo, fursa mbalimbali za biashara ya mazao kati ya Tanzania na Marekani zilijadiliwa. Mazao hayo ni pamoja na maparachichi, ufuta, samaki, asali, kokoa, mchele, mvinyo, pareto, na mazao ya bahari.

Akizungumza kwenye Mkutano huo, pamoja na kueleza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo na kuongeza mauzo ya nje, Mhe. Waziri Prof. Mkenda ameeleza pia changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo pamoja na fursa za uwekezaji pamoja na kuwasihi wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, Meya Kevin Smith ameeleza kwamba Jiji lake la Helena-West linalima mchele kwa wingi na lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika biashara ya zao hilo.

Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza, ameeleza kuwa Kongamano hilo ni mwanzo wa makongamano mengine mengi ya namna hiyo, kwa sababu Ubalozi umejizatiti kuimarisha mauzo ya bidhaa mbalimbali za Tanzania nchini Marekani, hasa bidhaa za kilimo. Pamoja na mambo mengine, Balozi Kanza ameahidi Ubalozi utaendelea kushirikiana na mwekezaji au mfanyabiashara yeyote mwenye lengo la kuwekeza Tanzania.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), akiwasilisha hotuba yake kwenye Kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao 


Balozi wa Tanzani nchini Marekani Dkt. Elsie Kanza akiwa pamoja na wajumbe wa Ubalozi wakishiriki kwenye Kongamano hilo 


Sehemu ya Wajumbe walioshiriki katika Kongamano   


Balozi Kanza akizungumza wakati wa kongamano  


Meya Kevin Smith wa Jimbo la Helena-West Arkansas, nchini Marekani akizungumza wakati wa Kongamano



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.