Monday, April 4, 2022

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WABUNGE WA EALA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk leo tarehe 4 Aprili 2022 wamekutana na kufanya mazungumzo na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Akizungumza na Wabunge hao Waziri Mulamula amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kupitia chombo hicho muhimu katika Jumuiya, ya kuhakikisha Jumuiya inaendelea kustawi zaidi. Vilevile, Waziri Mulamula ametoa wito kwa wabunge hao kuendele kuwa wamoja katika kutetea, kufuatilia na kulinda maslahi ya Taifa na Jumuiya kwa ujumla. 

Wabunge hao ambao walifanya ziara ya kikazi Wizarani wameeleza kuridhishwa na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha,kupitia Wizara wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwasilisha kwa wakati ada ya unachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Ziara hiyo ililenga kubadilishana mawazo na uzoefu baina yao na Viongozi wa Wizara sambamba na kutoa mrejesho wa maendeleo ya masuala mbalimbali muhimu yanayoendelea katika Jumuiya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akifuatilia mazungumzo na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wannne kushoto) Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (watatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Dr. Abdullah Hasnuu Makame akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wabunge wa EALA, Waziri Mhe. Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Mbarouk yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
 Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Adam Kimbisa akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wabunge wa EALA, Waziri Mhe. Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Mbarouk yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

WAZIRI VICKY FORD AZINDUA MPANGO WA ‘SHULE BORA’ KIBAHA

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford amezindua mpango wa elimu unaojulikana kama ‘Shule Bora’ Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Ford amesema mpango wa ‘Shule Bora’ utasaidia kuboresha elimu nchini Tanzania na utawasaidia zaidi ya watoto milioni nne, ambapo nusu yao watakuwa ni watoto wa kike.

“Elimu ni kipaumbele kwa Rais Samia pamoja na Waziri wa Mkuu wa Serikali ya Uingereza……….ni lengo la Serikali ya Uingereza kuisaidia watoto zaidi ya milioni 15 hapa Tanzania kupata elimu, lakini tumeanza na hawa wachache lakini pia tumezingatia usawa wa kijinsia ambapo nusu ya sehemu ya msaada huu utamnufaisha mtoto wa kike,” amesema Mhe. Ford.

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa msaada wa pound milioni 180 zilizotolewa na Serikali ya Uingereza utasaidi sana kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia mpango wa elimu wa 'Shule Bora'.

Prof. Mkenda amesema pamoja na mambo mengine, kuwa msaada wa Serikali ya Uingereza kupitia mpango huu wa elimu utasaidia sana kuboresha mazingira ya elimu nchini ikiwa ni pamoja nan miundombinu ya shule, vitabu na sheria pamoja na mitaala inayotumika kufundishia.

“………….‘Shule Bora’ itaiwezesha Serikali yetu kufanya mapitio ya Sera ya elimu ya 1978, kuboresha Sheria ya Elimu, kuboresha mitaala ya elimu, kuangalia idadi ya walimu pamoja na wakufunzi na wahadhiri,” amesema Prof. Mkenda

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mhe. David Silinde amemhakikishia Waziri Ford kuwa fedha zote za mpango wa elimu wa ‘Shule Bora’ zitatumika kama ilivyokusudiwa ili kuwawezesha watoto wa kitanzania kunufaika na elimu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford katika viwanja vya shule ya msingi Mkoani ambapo mpango wa elimu wa 'Shule Bora' umezinduliwa 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiangalia baadhi ya vitu vilivyotengenezwa na watoto wa Shule ya Msingi Mkoani kabla ya uzinduzi wa mopango wa elimu wa 'Shule Bora'

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiangalia baadhi ya vitu vilivyotengenezwa na watoto wa Shule ya Msingi Mkoani kabla ya uzinduzi wa mpango wa elimu wa 'Shule Bora'


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford wakizindua mpango wa elimu wa 'Shule Bora' 


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na wageni (hawapo pichani) baada ya uzinduzi wa mpango wa 'Shule Bora'





MKUTANO MAALUM WA 47 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC NGAZI YA WATAALAM UMEFUNGULIWA JIJINI ARUSHA

Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 6 Aprili 2022.

Mkutano huu unafanyika katika mpangilio ufuatao; tarehe 4 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Wataalam, tarehe 5 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu na tarehe 6 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Mawaziri.

Pamoja na mambo mengine Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaandaa taarifa ya masuala ya Fedha na Utawala itakayowasilishwa kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu na baadae kwenye mkutano wa Mawaziri.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Justin Kisoka (kushoto) akichangia hoja katika Mkutano  Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 4 Aprili 2022 jijini Arusha, Tanzania.
Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akifatilia mkutano huo.


Mkutano ukiendelea, kulia ni ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Meza kuu ikiongoza Mkutano.

Mkurugenzi Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta akifatilia majadiliano katika mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukifuatilia majadiliano.

 

WAZIRI FORD ARIDHISHWA NA UTOAJI HUDUMA ‘ENGENDERHEALTH’

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ameonesha kuridhishwa na utoaji wa huduma katika kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Ford ameoneshwa kuridhishwa na utoaji wa huduma jumuishi kwa familia, mama, watoto, vijana na watu wenye ulemavu wakati alipofanya ziara katika kituo cha EngenderHealth Tanzania ambacho kinafadhiliwa na Serikali ya Uingereza.

“Nimeridhika na utoaji wa huduma katika kituo hiki hasa baada ya kuongea na akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti maelezo yao kwangu yanaonesha huduma ni nzuri na zinaridhisha,” amesema Waziri Ford

Pia nimeona mazingira ya kituo hiki pamoja na kuongea madaktari, wauguzi na watoa huduma kwa kweli wamenifariji kazi yao ni nzuri na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa bidi bila kuchoka, ameongeza Waziri Ford

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa EngenderHealth Tanzania, Dkt. Moke Magoma ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili wa baadhi huduma katika kituo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidi na weledi katika kuwahudumia watanzania wanaotumia kituo hicho.

“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wafanyakazi wa kituo hiki tunakushukuru sana kwa ufadhili wa huduma za wahanga wa unyanyasaji na Watoto na watu wenye ulemavu huduma hii imekuwa na msaada mkubwa sana katika jamii, tunakuahidi kufanya kazi kwa bidi na weledi,” amesema Dkt. Magoma

Baadhi ya akina mama waliokuwa katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu na huduma mbalimbali wameomba kuongezewa watumishi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa Pamoja na kujengewa kituo nmumuishi ambacho kitaweza kusaidia upatikanaji wa huduma zote katika eneo moja.

Kituo cha EngenderHealth Tanzania kanafadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika huduma za mama, mtoto, vijana na wenye ulemavu hasa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto. 

Huduma nyingine zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na huduma jumuishi kwa familia, mama, Watoto, vijana na wenye ulemavu.

Waziri Ford yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.    

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na uongozi wa kituo cha Afya cha EngenderHealth mara baada ya kuwasili kituoni hapo Yombo Vituka Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na akina mama waliokuwa katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka wakati wakisubiria huduma za afya  





Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiwa katika kituo cha huduma ya macho, masikio na utengamao kwa mtoto  katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 


Mhe. Zungu akutana na Rais Mwenza wa Bunge la Pamoja la EU na OACPS

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuimarisha ushirikiano miongoni mwao na miongoni mwa wabunge wao. Hayo yameafikiwa tarehe 02 Aprili 2022 kwenye makao makuu ya Bunge la Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu na  Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS), Mhe. Prof. Carlos Zorrinho). 

Mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 41 wa Bunge  la OACPS na EU  ambapo Mhe. Zungu anaongoza ujumbe wa Tanzania, viongozi hao walikubaliana pia kupitia Mabunge yao kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja  wa Ulaya unaimarishwa zaidi.

Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kumwalika Mhe. Zorrinho pamoja na  baadhi ya Wabunge wa Bunge la EU kuitembelea Tanzania na kujionea wenyewe hatua mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya Tanzania. Rais huyo mwenza wa Bunge la Pamoja la Ulaya na ACP alipokea mwaliko huo kwa furaha  na kuahidi kufanya ziara hiyo nchini siku zijazo akiambatana na baadhi wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya na Bunge hilo linafurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania kusimamia ajenda za maendeleo na ustawi wa jamii, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.

Mhe. Zungu alimwomba mwenyeji wake huyo kuwahamasisha wawekezaji wa Ulaya waendelee kuja kuwekeza nchini kwenye masuala ya uchimbaji wa gesi na maeneo mengine, kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.

Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushawishi wa mabunge yao kutoa miongozo itakayoimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Carribean na Pacific pamoja na masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha amani eneo la ukanda wa maziwa makuu hususan nchini Msumbiji. Professa Zorrinho alieleza kuwa EU ina imani kubwa zaidi na Tanznaia katika masuala ya usuluhishi wa migogoro na kukuza amani duniani.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Zungu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na maafisa wengine waandamizi wa Ubalozi na Bunge.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (kushoto) akisalimiana na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (kulia) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili,2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strassbourg.


 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama) akichangia katika moja ya kikao cha Bunge la Pamoja la OACPS na EU kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe.Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (katikati kulia) akiwa katika kikao chake na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza (co-President) wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (wa pili kushoto) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strasbourg. Kulia mwa Mhe. Zungu ni Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Ubalozi wa Jamhuri wa Muungano nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya (kulia) na maofisa wengine kutoka Bunge la Tanzania na Bunge la EU.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu,  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Dkt George Pinto Chikoti, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS (kulia) na Mhe Balozi Jestas Abuok Nyamnaga (kushoto) nje ya ukumbi kunakofanyika Mkutano wa 60 wa Bunge la OACPS unaofanyika katika ofisi za Bunge la EU jijini Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 29 Machi, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu  (aliyesimama kulia) akibadilishana mawazo na mmoja wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya wakati wa Mkutano wa 41 wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU uliofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

NCHI WANACHAMA WA SADC ZAPONGEZWA KWA KUJITOLEA KULINDA AMANI YA KANDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor amezipongeza Nchi Wanachama wa SADC zikiwemo zile zinazochangia vikosi nchini Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwenye masuala ya ulinzi wa amani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Msumbiji na kanda ya SADC kwa ujumla.

Mhe. Pandor ametoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Amesema Mkutano huo ni mwendelezo wa majadiliano yanayofanywa na Nchi Wanachama wa SADC kuhusu namna ya kuisadia Msumbiji katika kupambana na vitendo vya ugaidi na ukatili vilivyoripotiwa kwenye maeneo ya Kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.

“Nia ya dhati na msaada unaoendelea kutolewa kwa Msumbiji na Nchi Wanachama ni wa kupongezwa. Hii ni ishara kwamba sote tuna nia moja ya kupambana na ugaidi ambao unatishia jitihada zinazofanywa na jumuiya katika kukuza mtangamano wa SADC na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hata hivyo niwahakikishie kuwa jitihada hizi si za bure zimezaa matunda” alisema Dkt. Pandor.

Kadhalika ameipongeza Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayofanya ya kurejesha hali ya amani na utulivu na kuwawezesha wananchi wa Msumbiji hususan wale wanaoishi Kaskazini mwa nchi hiyo kwenye Jimbo la Cabo Delgado kuendelea na shughuli zao za maendeleo pasipo kuhofia vitendo vya ugaidi. 

"Tumekutana hapa kwa niaba ya wakuu wetu wa Nchi na Serikali, kupokea na kujadili ripoti na mapendekezo kuhusu mwenendo wa Misheni ya SADC nchini Msumbiji. Niwajulishe tu Ripoti inatia moyo kwani mambo mengi mazuri yamefanyika tangu SAMIM ianze kazi nchini Msumbiji na hali ya usalama nchini humo hususan maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado inaendelea kuimarika na wananchi wameanzaa kurejea katika shughuli zao za kawaida”, alisema Mhe. Pandor.

Pia alieleza umuhimu wa kufunguliwa kwa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi ambacho kilizinduliwa rasmi tarehe 28 Februari 2022 jijini Dar Es Salaamkwamba ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama kwenye kanda ya SADC.

“Tumefurahishwa na uzinduzi wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na ugaidi nchini Tanzania tarehe 28 Februari 2022. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usalama wa kanda yetu ambao utafanya kazi kwa kushirikiana na Kituo cha Kanda cha Tahadhari za Mapema” alieleza Dkt. Pandor.

Vilevile alitumia nafasi hiyo kuushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kuchangia kwenye maeneo mbalimbali ya Misheni hiyo na kutoa wito kwa washirika wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia na kuunga mkono jitihada za SADC za kurejesha amani na usalama nchini Msumbiji na maeneo mengine.

Awali akimkaribisha Dkt. Pandor kuzungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi alisema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC ili kuhakikisha lengo lilowekwa la kukomesha kabisa vitendo vya kigaidi nchini Msumbiji linatimia. Pia naye alizipongeza nchi wanachama na Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwa dhati na kueleza kuwa hali ya amani na utulivu imerejea kwa kiasi kikubwa nchini Msumbiji hususan kwenye maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.

Nchi Wanachama kumi (10) za Misheni ya SADC nchini Msumbiji ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na Zambia. 

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Ujumbe huo unamjumuisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (wa pili kulia meza kuu) akifungua  rasmi Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. Wa pili kushoto ni Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,  Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (wa kwanza kulia) akiwa na wajumbe alioongozana nao kutoka Tanzania.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano huo. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo na kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst.) Gaudence Milanzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (wa pili kulia) akifuatilia itifaki za ufunguzi  rasmi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini
tarehe 03 Aprili 2022
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,  Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (wa kwanza kulia) akiwa na wajumbe wa Tanzania na wajumbe wa nchi nyingine za SADC wakishiriki taratibu za ufunguzi rasmi wa mkutano huo uliofanyika  jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Sehemu ya ujumbe wa Malawi ulioshiriki Mkutano huo


Sehemu ya ujumbe wa Lesotho wakati wa ufunguzi wa mkutano






Sunday, April 3, 2022

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WAZIRI WA UINGEREZA JIJINI DODOMA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (kulia) walipokutana kwa ajili ya chakula cha jioni jijini Dodoma wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa pili kushoto) akizungumza na  Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (wa kwanza kulia) walipokutana kwa ajili ya chakula cha jioni jijini Dodoma wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (wa kwanza kulia) akizungumza wakati alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula jijini Dodoma


Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (kushoto) yakiendelea walipokutana na  jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akionesha zawadi y apicha ya michoro ya Tingatinga ambayo alimpatia zawadi Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford walipokutana jijini Dodoma.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akionesha zawadi ya picha ya michoro ya tingatinga ambayo alipewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula walipokutana kwa jijini Dodoma.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akitoa maelezo kuhusiana na michoro ya picha ya tingatinga ambayo alimpatia Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford walipokutana jijini Dodoma


Balozi Liberata Mulamula (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ambaye alifika jijini Dodoma kwa ziara ya kikazi nchini tarehe 03 Aprili 2022.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzai tarehe 3-5 Aprili 2022.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano mzuri ulioko baina ya Tanzania na Uingereza.

Balozi Mulamula amemshukuru Mhe. Ford kwa uamuzi wa kuja kuitembelea Tanzania na kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inafadhiliwa na Uingereza na kumualika kuja tena nchini wakati mwingine.

Naye Mhe. Ford ameelezea kufurahishwa ridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo jambo ambalo amesema inatia moyo kuona fedha zinazotolewa na nchi hiyo zinafanya kazi iliyokusudiwa na hivyo kusaidia harakati za kubadili maisha ya Watanzania.

Waziri Ford aliwasili nchini kupitia uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Kilimanjaro ambako alitembelea miradi ya maendeleo katika mji wa Moshi na baadaye jijini Dodoma ambako alikwenda Ikulu ya Chamwino na kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan .

Tarehe 04 Aprili 2022, Mhe. Ford atatembelea miradi ya kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo, kituo cha kuzuia biashara ya binadamu na ulinzi wa watoto vya Jijini Dar es Salaam na kuzindua mradi wa maendeleo wa elimu bunifu nchini unaoitwa Shule Bora utakaofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Jioni ya tarehe 04 Aprili 2022 Mhe. Ford atakuwa na mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea ziara yake nchini na anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 05, Aprili 2022

WAZIRI UINGEREZA ANAYESHUGHULIKIA MASUALA YA AFRIKA AWASILI DODOMA KWA ZIARA YA KIKAZI

 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Masshariki Balozi Fatma Rajab baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akizungumza na wenyeji wake katika uwanja wa ndege wa Dodoma  baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisaini kitabu cha wageni katika uwanja wa ndege wa Dodoma  baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (katikati) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) kulia ni Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concor akifuatilia mazungumzo hayo.


 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (katikati) huku Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concor (kulia) akifuatilia mazungumzo hayo
 
 
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford amewasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

Waziri huyo amepokelewa katika uwanja wa ndege wa  Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab. 

Baada ya kuwasili jijini Dodoma Waziri Ford alielekea Ikulu ya Chamwino ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznsia Mhe.  Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Katika ziara yake nchini Mhe. Ford pamoja na mambo mengine,  anatarajiwa kuzindua mpango mpya wa Elimu bunifu nchini ambao unafadhiliwa na serikali ya Uingereza. 

katika ziara yake nchni Waziri Ford ataungana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf  Mkenda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa kuzindua mpango huo mpya wa maendeleo wa elimu bunifu nchini unaoitwa Shule Bora utakaofanyika Kibaha mkoani Pwani tarehe 04 Aprili 2022.

Mpango wa Shule Bora utaongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto zaidi ya milioni nne (4) nchini, umelenga kuboresha viwango vya elimu kwa watoto wenye ulemavu, watoto wanaotoka maeneo yenye upungufu wa rasilimali na wasichana.

Kati ya mwaka 2015-2020 Uingereza kupitia ufadhili katika sekta ya elimu imesaidia zaidi ya watoto milioni 15.6 duniani kote kupata elimu, ikiwa ni pamoja na wasichana milioni 8.1.
 
Waziri Ford pia atakuwa na mikutano na ziara mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kazi mbalimbali zinazofanywa nchini katika kuimarisha uhusiano kati ya Uingereza na Tanzania kupitia nyanja za biashara, mabadiliko ya tabianchi na kupambana na uhalifu mkubwa na uliopangwa.