Tuesday, November 15, 2022

AFRIKA IJIPANGE KUTUMIA FURSA ZAKE KUKIDHI MAHITAJI YA DUNIA


Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo akiwasilisha mada kuhusu fursa za biashara na uwekezaji katika kanda ya Afrika katika mkutano wa mabalozi unaoendelea Zanzibar

 

Mkutano wa mabalozi ukiendelea Zanzibar




Monday, November 14, 2022

RAIS SAMIA KUKUTANA NA MABALOZI ZANZIBAR

 



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika mkutano wa Mabalozi unaoendelea Zanzibar

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiwasilisha hotuba yake kwa mabalozi (hawapo pichani). Mkutano huo umeanza leo Zanzzibar na utamalizika tarehe 21 Novemba, 2022. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akitoa tathmini ya mkutano wa mabalozi unaoendelea Zanzibar 

Sehemu ya mabalozi wakifuatilia kikao

Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakiongozwa na Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu  Balozi Joseph Sokoine (katikati) na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Amani, Balozi Stephen Mbundi wakifuatilia kikao

Thursday, November 10, 2022

MABALOZI WAFANYA ZIARA HOSPITALI YA CCBRT

Mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Palestina, Indonesia na Vietnam hapa nchini wamefanya ziara katika Hospitali ya CCBRT na kujionea utoaji wa huduma za afya na kazi mbalimbali zinazofanywa na Hospitali hiyo pamoja na kuangalia maeneo ya ushirikiano.

Ziara ya mabalozi hao imefanyika leo Jijini Dar es Salaam ambapo mabalozi waliofanya ziara katika hospitaali hiyo ni Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi amesema kuwa ziara ya mabalozi hao imelenga kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotolewa na hospitali hiyo na kwamba CCBRT inaamini kuwa baada ya ziara hiyo mabalozi watapata fursa ya kujionea maeneo ya ushirikiano baina ya nchi zao hospitali hiyo.

“Tunategemea baada ya ziara hii mabalozi wataona maeneo ya ushirikiano, sisi kama CCBRT tuna maeneo matatu ambayo tunapenda kushirikiana nao, eneo la kwanza ni utoaji wa huduma, vifaa na vifaa tiba, na mwisho ni kuwajengea uwezo wataalamu wetu. Maeneo yote haya ni muhimu hasa ukizingatia CCBRT inatoa huduma bobezi na za kibingwa,” amesema Bi. Msangi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza amesema kuwa mabalozi wamefanya ziara katika hospitali hiyo kwa lengo la kujionea utoaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa na CCBRT na kupata fursa kuona maeneo ya ushirikiano baina ya nchi zao na CCBRT.

“Katika ziara ya mabalozi hapa CCBRT, mabalozi wameonesha kuridhishwa na shughuli zinazofanywa na hospitali hii, na baada ya ziara hii watawasiliana na nchi zao na kuona maeneo ya ushirikiano katika kuboresha zaidi sekta ya afya,” amesema Balozi Mgaza.  

Naye Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa na CCBRT katika kuboresha afya za watanzania nchini na kuahidi kuwasiliana na serikali ya Palestina kuona ni jinsi gani serikali yake inaweza kushirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania. 

“Nimekuwa nikipita maeneo haya mara kwa mara lakini sikujua kuwa huduma nzuri zinatolewa hapa CCBRT, nawapongeza kwa jitihada hizi za kuuelimisha umma kuhusu magonjwa mbalimbali na njia za kuyakabili. Naahidi baada ya ziara hii nitawasiliana na Serikali yangu na kuona ni maeneo gani tunaweza kushirikiana katika kuboresha sekta ya afya,” amesema Balozi AbuAli

Kadhalika, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko amesema kazi inayofanywa na hospitali ya CCBRT katika kuwahudumia watanzania hususan akina mama wenye changamoto ya fistula na watu wenye ulemavu wa viungo ni kazi kubwa na inayoigusa jamii.

“Jitihada zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kuboresha vituo vya afya ni nzuri……nimeguswa na jinsi hospitali hii inavyowahudumia wananchi, baada ya ziara hii tutakaa na kuangalia maeneo ya ushirikiano,” amesema Balozi Jatmiko.

Ziara hiyo iliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi akizungumza na Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa CCBRT. 

Mabalozi wakiwa katika kituo cha mabinti cha CCBRT wakati walipofanya zaira hospitalini hapo 

Mabalozi wakiwajulia hali akina mama wanaokabiliwa na changamoto ya Fistula katika hospitali ya CCBRT

Balozi wa Indonesia nchini, Mhe. Triyogo Jatmiko akisalimiana na mtoto anayetumia mguu wa bandia katika karakana ya viungo tiba saidizi na viungo bandia katika hospitali ya CCBRT wakati mabalozi walipofanya ziara hospitalini hapo. Wengine pichani ni Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli, Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Nam Tien, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Bi. Brenda Msangi, (Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Hemed Mgaza pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Ceaser Waitara) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Balozi wa Palestina nchini, Mhe. Hamdi Mansour AbuAli akionesha mabalozi wenzake kitu wakati wa ziara ya mabalozi hao katika hospitali ya CCBRT 

Mabalozi wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT Bi. Brenda Msangi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali hiyo 



Tuesday, November 8, 2022

ZANZIBAR WAPIGWA MSASA KUHUSU UZALISHAJI WA MAZAO BORA YA BAHARI

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame amesema uzalishaji wa matango bahari na uboreshwaji wa zao la mwani unamanufaa makubwa kwa Zanzibar na Nchi za pembezoni mwa ukanda wa Bahari ya Hidi.

Waziri Suleiman Masoud Makame, ameyasema hayo wakati akifungua semina ya siku 5 kuhusu namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani iliyofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar jana tarehe 07 Novemba 2022.

Mhe. Suleiman ameongeza kuwa kufanyika kwa Mkutano huo mjini hapo kutaleta mafanikio kwa kuwa wajumbe watapata nafasi ya kujadiliana juu ya namna bora ya kuzalisha mazao ya baharini ikiwemo vifaranga vya matango bahari.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dkt. Aboud Suleiman Jumbe amesema mkutano huo wa watalamu kutoka katika nchi za IORA utafungua milango kwa watalamu na kuona namna gani Zanzibar ilivyojiandaa katika uchumi wa buluu na uvuvi.

"Nchi za ukanda wa pembezoni mwa bahari ya hindi watajifunza mambo mengi hapa Zanzubar kwa vile kuna wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi" ameeleza

Nae Mkurugenzi wa Uchumi wa Buluu Bi. Rina Setyawati kutoka ukanda wa Bahari ya Hindi Nchi za IORA zimekuwa na usharikiano wa pamoja katika mambo mbalimbali ikiwemo katika suala zima la kujifunza ubora wa kuzalisha vifaranga vya matango bahari na kilimo bora chenye faida kwa Nchi wanachama.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mratibu wa Masuala ya Jumuiya ya Nchi za Mwambao mwa Bahari ya Hindi (IORA) Balozi Agnes Richard Kayola akizungumza katika Mkutano huo ameeleza kuwa IROA inaimani kuwa Mkutano huo utakuwa na tija kubwa kwa wanachama waliotoka nje ya Tanzania kwa vile watapata muda wa kubadilishana uzoefu jinsi ya kufanikiwa katika kilimo cha mwani kwa wananchi.

Aidha, katika kipindi cha siku 5 cha semina hiyo wakulima wa mazao mbalimbali ya bahari watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao sambamba na utaalam wanaoutumia kuzalisha mazao hayo. Hatua hiyo itawapa wakulima hao nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu uchumi wa buluu, sambamba na kujipatia fursa za makoso mapya ya mazao yao.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame akihutubia wakati wa ufunguzi wa semina ya siku 5 kuhusu namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani uliofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar 

Semina ya namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani uliofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar 
Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mratibu wa Masuala ya Jumuiya ya Nchi za Mwambao mwa Bahari ya Hindi (IORA) Balozi Agnes Richard Kayola akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani uliofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dkt. Aboud Suleiman Jumbe akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa semina ya namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani uliofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar 
Picha ya pamoja

Saturday, November 5, 2022

WIZARA KUSHIRIKIANA NA VYUO VIKUU KUONGEZA WIGO WA ELIMU

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeahidi kuendelea kushirikiana na vyuo vikuu nchini ili kupanua wigo wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na wahisani yakiwemo mashirika ya Kikanda, Kimataifa na nchi marafiki.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga alipokutana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Henry James na baadhi ya Viongozi wa Serikali za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.

“Fursa za Masomo Nje ya Nchi na ajira zimekuwa zikitangazwa na kuratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea kupanua wigo wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na Wizara Kikanda na Kimataifa.,” Alisema Balozi Mindi

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bw. Kheri James amepongeza jitihada zinazotekelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha watanzania wanapata fursa mbalimbali za masomo na kazi Nje ya nchi kwani jambo hilo ni la kizalendo.

“Wizara ina fursa ya ziada ya kuviunganisha vyuo vikuu nchini na Vyuo Vikuu Nje ya nchi kwa ufadhili wa masomo, mahusiano kati ya vyuo vya Tanzania na vya Nje na kubadilishana wanafunzi katika taaluma mbalimbali ili kuwajengea uwezo na ufanisi katika masomo,”Alisema Bw. James.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Spencer Minja na Rais wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Bw. Mark Makaranga ambapo pamoja na mambo mengine wanafunzi hao wameipongeza na kuiomba Wizara kuandaa Kongamano la wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhusu Mtangamano wa Jumuiya ya Kikanda na Kimataifa. 

Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo ina vyuo vitano ambavyo ni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Shule Kuu ya Sheria, Chuo cha Maji na Chuo cha Mtakatifu Joseph.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akieleza jambo wakati wa kikao na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Henry James na baadhi ya Viongozi wa Serikali za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Henry James akimsikiliza Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga wakati wa kikao na baadhi ya Viongozi wa Serikali za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akifafanua jambo wakati wa kikao na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Henry James na baadhi ya Viongozi wa Serikali za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo

Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Bw. Mark Makaranga akieleza jambo wakati wa kikao

Kikao kikiendelea 

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Henry James katika pichaa ya pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga, Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kulia), Bw. Spencer Minja na Rais wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Bw. Mark Makaranga (kushoto)


Saturday, October 29, 2022

TANZANIA, MALAWI KUSHIRIKIANA KATIKA MUSUALA YA ULINZI NA USALAMA

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi zimesaini hati mbili za makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission for Cooperation - JPCC) kati ya nchi hizo mbili uliofikia tamati jana tarehe 28 Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam.

Hati hizo za makubaliano zilizosainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) na Mhe. Titus Mvalo Waziri wa Sheria wa nchini Malawi zinahusu ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi la Malawi na Jeshi la Polisi la Tanzania, na ushirikiano baina ya Taasisi za Uhamiaji za pande zote mbili. 

Akizungumza muda mfupi baada ya kusaini hati hizo, Waziri Ndumbaro na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, ambaye pia alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameeleza kuwa Mkutano huo umewezesha pande hizo mbili kukubaliana katika masuala mbalimbali ya msingi huku msisitizo mkubwa ukielekezwa katika sekta ya Biashara, Uwekezaji, Ulinzi na Usalama, Miundombinu, Masuala ya Mambo ya Nje na Kijamii 

“Katika Mkutano huu wa Tano wa JPCC pamoja na masuala mengine nchi zetu mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya kutatua changamoto zinazokabili sekta binafsi ili kuwezesha na kurahisisha biashara, vilevile tumekubalia kutumia fursa ya uwepo wa Ziwa Nyasa katika kurahisisha uendeshaji wa shuguli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu kwa maendeleo ya wananchi wetu” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Mdumbaro aliongeza kutaja fursa na faida mbalimbali zilizotokana na Mkutano huo ikiwemo, nia na dhamira ya Nchi ya Malawi ya kutumia barabara ya Mtwara hadi Bandari Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma katika kusafirisha bidhaa na huduma kwenda nchini humo. Fursa nyingine ni nia ya Malawi kushirikiana na Tanzania katika suala la elimu na mfunzo kupitia Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaa, ambapo alieleza kuwa hati ya makubaliano kuhusiana na suala hilo inatarajiwa kusainiwa siku za usoni. 

Dkt. Ndumbaro aliendelea kufanunua kuwa licha ushirikiano na uhusiano mzuri wa Kidiplomasia uliopo baina ya pande hizo mbili, Malawi imeonesha nia ya kutumia Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay kutokana na ukweli kuwa njia hiyo ni fupi zaidi ikilinganishwa na njia zote wanazozitumia hivi sasa kutoka Bandari mbalimbali kuingiza bidhaa nchini humo. 

Mbali na kuzungumzia fursa za kiuchumi Dkt. Ndumbaro, alitoa rai kwa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kuthamini lugha ya Kiswahili sambamba na kuhimiza matumizi ya lugha hiyo nchini humo. Vilevile aligusia umuhimu wa Serikali ya Jamhuri ya Malawi kuendelea kufundisha somo la Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu nchini humo.

Kwa upande wake Mhe. Titus Mvalo, Waziri wa Sheria wa Malawi na Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi ambaye pia alikuwa anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo amebainisha kuwa, masuala yote katika Mkutano huo yamehafikiwa katika wakati sahihi ambapo Viongozi Wakuu wa Serikali za pande zote mbili wanania ya dhati kuona ushirikiano wa Tanzania na Malawi unaleta tija ya kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili. 

Waziri Mvalo aliendelea kuelezea namna Serikali ya Malawi inaweka jitihada katika kukuza lugha ya Kiswahili nchini humo ikiwemo kuongeza somo la kiswahili kwenye mtaala wa elimu nchini humo.

“Moja ya sifa kubwa ya lugha ya Kiswahili ni ile ya kutokuwa na mizizi ya ukabila, siyo rahisi hata hapa nchini Tanzania kusikia kabila moja wapo miongoni mwa makabila zaidi ya 120 yaliyopo likijinasibu kuwa lugha ya kiswahili ya kwake. Tunajivunia lugha hii hadhimu ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha ya asili ya Afrika inayounganisha watu wengi barani hapa” alisema Waziri Mvalo 

Akihitimisha hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Tano wa JPCC Waziri Mvalo ametoa rai kwa sekta zote kuhakisha wanakutana mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa masuala yote yaliyohafikiwa katika Mkutano huo. 

Mkutano wa Tano wa JPCC ambao umehitimishwa katika ngazi ya Mawaziri umefanyika kwa kipindi cha siku tatu kuanzia terehe 26 - 28 Oktoba 2022. Mbali na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kwa upande wa Tanzania Mkutano pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa. Wengine waliohudhuria ni Watendaji kutoka Wizara, Idara, na Taasisi mbalimbali za Serikali. 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akisalimiana na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo kwenye wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akifungua Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo wakibadilishana nyaraka kwenye Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Waziri wa Sheria wa nchini Malawi Mhe. Titus Mvalo wakisaini Hati za Makubaliano kwenye Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Azizi akitoa neno la ukaribisho wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Dar es Salaam
Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole akifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea
Sehemu ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally S. Gugu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Bw. Kheri Abdul Mahimbali wakibadilishana mawazo wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam
Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ukiendelea

Thursday, October 27, 2022

DIASPORA WAHIMIZWA KUTUMIA HUDUMA ZA FEDHA ZA KIDIGITALI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewasisitiza Diaspora wote Duniani kutumia huduma za kifedha kupitia kwa watoa huduma waliosajiliwa ili kuendelea kuchangia uchumi wa Tanzania.

Dkt. Tax ametoa wito huo jijini Dar es Salaam aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa.

Amesema, upo umuhimu mkubwa kwa Diaspora kutumia huduma za kifedha zilizosajiliwa ili kuhakikisha usalama wa fedha zao na kuweka kumbukumbu sawa. Amesema kwa mujubu wa Takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 30 mwaka 2019 na mwaka 2021 Diaspora walichangia uchumi wa Taifa kwa Dola za Kimarekani milioni 569 sawa na kuchangia asilimia 0.8 ya pato la Taifa.

Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuwekeza katika ubunifu na kuboresha huduma zao wakati wote ili kuendana na mahitaji ya wananchi kulingana na mabadiliko ya Teknolojia. 

Amesema anaipongeza Kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunganisha Afrika kupitia huduma zao ambapo kwa sasa wamepanua wigo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuongeza ukanda wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jambo ambalo litawawezesha Diaspora kwenye maeneo hayo kutuma na kupokea fedha pasipo kikwazo chochote.

“Sekta ya fedha ni sekta muhimu katika nchi yoyote, Serikali inaona jambo hili ni kubwa kwa sababu ya umuhimu wa sekta ya fedha lakini kwa kutambua kwa sasa dunia ipo katika uchumi wa kidigitali. Uchumi wa kidigitali unafanya kazi kidigitali hivyo nawasihi Diaspora kutumia huduma hii ili kuweza kuchangia maendeleo ya taifa kwa kuwa benki na taasisi nyingine zinazotoa huduma za kifedha zimerahisisha biashara na uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa ujumla,” alisema Dkt. Tax.

Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa miongozo mbalimbali inayowawezesha watoa huduma za fedha nchini kuandaa huduma zenye manufaa kwa wanannchi na kuahidi Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutimiza lengo la kuwainua wananchi kiuchumi kupitia huduma mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni amesema kuzinduliwa kwa huduma ya M-Pesa katika ukanda wa SADC kumetoa fursa ya kuongeza wigo wa kutuma na kupokea pesa katika nchi nyingi zaidi barani Afrika hususan nchi za SADC.  

“Wateja wetu wanaweza kupokea na kutuma fedha katika ukanda wa Sadc, sasa tumeiunganisha Afrika na M-Pesa, jambo hili litachangia ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” amesema Bw. Mbeteni

Bw. Mbeteni ameongeza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo utarahisisha ufanyaji wa biashara na huduma nyingine za kijamii. Uzinduzi wa huduma hiyo uliongozwa na kauli mbiu ya “Dunia Kijiji, Afrika ni M-Pesa”.  Katika uzinduzi huo, Dkt. Tax aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwasilisha hotuba ya ufunguzi aliposhiriki uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyoanzishwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kupitia huduma ya kutuma fedha ya M-Pesa  

Mkurugenzi wa Vodacom M-pesa, Bw. Epimack Mbeteni akiongea na washiriki wakati wa uzinduzi wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Washiriki wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa baadhi ya nchi za SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwin Gondwe na wafanyakazi wa Kampuni ya simu ya Vodacom



Wednesday, October 26, 2022

TANZANA-MALAWI WAKUTANA KUJADILI MASUALA YA USHIRIKIANO


Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission For Cooperation - JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi umeanza leo tarehe 26 Oktoba 2022 jijini Dar es Salam. 

Mkutano huu wa siku tatu, kuanzia tarehe 26 – 28 Oktoba 2022, utafanyika katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 26 Oktoba 2022, Makatibu Wakuu tarehe 27 Oktoba 2022, na kuhitimishwa na Mawaziri tarehe 28 Oktoba 2022. 

Agenda za mkutano huu zinaangazia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, afya, ulinzi na usalama, usafirishaji, sekta ya mafuta, maliasili, masuala ya utafiti na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Vilevile Mkutano huu utajadili namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya forodha ili kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya mataifa haya mawili. 

Akifungua Mkutano huo katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi, Balozi Joseph Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ameeleza mkutano huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali za pande zote mbili zinaendelea kutambua na kuthamini umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na karibu zaidi ili kuchochea maendeleo ya shughuli mbalimbali za kijamii na uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Aidha Balozi Sokoine ametoa rai kwa wataalamu waandamizi wa pande zote mbili kuhakikisha kuwa wanatumia mkutano huo kujadili na kuweka mikakati madhubuti ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa mataifa hayo mawili yenye utajiri wa fursa na rasilimali, kuweza kuchochea kasi ya maendeleo siyo tu kwa faida ya mataifa hayo mawili bali kwa faida ya kikanda na kimataifa kwa ujumla

“Sote tunatambua kuwa mataifa yetu yameendelea kufarahia ushirikiano mzuri uliopo baina yetu ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na mifumo mizuri ya kisheria inayotuwezesha kukutana na kujadili masuala yanayotuhusu mara kwa mara. Natoa rai kwenu kutumia mkutano huu vyema katika kujadili kwa kina kuhusu masuala muhimu kwa maslahi na maendeleo ya pande zote mbili” alisema Balozi Sokoine. 

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendelea kuendesha programu na kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi sambamba na kudumisha Uhusiano wa Kidiplomasia na Mataifa mbalimba duniani. 

Kwa upande wa Malawi, Ubalozi wa Tanzania nchini humo chini ya Mhe. Balozi Humphrey Polepole sambamba na kuendelea dumisha Uhusiano wa Kidiplomasia umekuwa ukiendelea na utekelezaji wa mikakati inayoliwezesha Taifa kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini humo. 

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), biashara kati ya Tanzania na Malawi imeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 138.12 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 186.1 mwaka 2019. Kutokana na janga la UVIKO-19 mwaka 2020, biashara ilipungua na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 159.4. Hata hivyo mwaka 2021 biashara iliongezeka tena hadi kufikia shilingi milioni 198.3.

Ujumbe wa Malawi katika Mkutano huo umeongozwa na Bw. William Kantayeni ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchini humo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi unaofayika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Azizi akichangia jambo kwenye Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja

Sehemu ya ujumbe wa Malawi wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Malawi Bw. William Kantayeni akichangia jambo kwenye Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Balozi Humphrey Polepole akifuatilia mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.

Meza kuu wakifuatilia Mkutano wa Tano (5) wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi katika ngazi ya Maafisa Waandamizi uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kamataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam