Wednesday, October 26, 2011

Viongozi Jumuiya ya Madola Wapewa Changamoto

Na Anna Nkinda – Perth, Australia
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Madola wameombwa kuchukua hatua na kuwasaidia mamilioni ya wasichana wanaoozwa kilazima huku wakiwa na umri mdogo na hivyo kukosa haki zao za msingi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari vilivyohudhuria maandalizi ya mkutano wa Viongozi wa Nchi wanachama wa Jumuia ya Madola (CHOGM) unaotarajia kuanza tarehe 28 hadi 30 mjini Perth nchini Australia inasema kuwa hivi sasa kuna mamilioni ya wasichana wananyanyasika kijinsia kutokana na ndoa za utotoni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo na Plan International na Royal Commonwealth Society inasema kuwa ndoa za lazima na za utotoni ni moja ya vikwazo vikubwa kwa wasichana katika elimu, afya ya uzazi, na uchumi wa mwanamke hivyo basi kuna ulazima kwa jumuia ya madola kuchukua hatua zaidi ili kuzuia wasichana wasilazimishwe kuolewa wakiwa bado au wakiwa tayari kuolewa.
“Jumuia ya madola inatetea haki za binadamu na kaulimbiu yake ya mwaka 2011 ni “Wanawake ni wakala wa mabadiliko” hivyo basi viongozi wa Jumuia hiyo wafanye haraka kuhakikisha kuwa yanapatikana mabadiliko makubwa kwa wanawake na si kubaki kama walivyo”, ilisema taarifa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Plan Internationa nchini Australia Ian Wishart alisema kuwa ndoa za lazima na za utotoni zinamuweka msichana katika umaskini, kutokuwa na afya njema na ukosefu wa elimu.
“Hivi sasa katika Dunia takwimu zinaonyesha kwamba kuna wasichana milioni 10 wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao wanaolewa kila mwaka hii inamaana kuwa kila msichana mmoja anaolewa kila baada ya sekunde tatu”, alisema Wishart.
Aliendelea kusema kuwa wasichana wanaoolewa mapema wanauzoefu wa ukatili wa kijinsia, wanadharauliwa na kulazimishwa kufanya mapenzi hii inawasababishia matatizo ya kijinsia na afya ya uzazi na zaidi wanakosa elimu na hivyo kuwa wajinga..
Wishart alisema, “Ndoa za utotoni na za kulazimishwa ni moja ya vitu vinavyozuia kufika malengo ya milinia ya kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto , upatikanaji wa elimu ya msingi kwa wote, kupunguza umaskini , usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Royal Commonwealth Society Peter Kellner alisema kuwa Jumuia ya madola iko makini kuhusiana na maendeleo ya wanawake na haki za binadamu, na ina mipango kazi ya kuhakikisha kuwa suala la ndoa za lazima na za utotoni linachukuliwa hatua za haraka na linapata ufumbuzi.
“Wanachama wote wa Jumuia ya Madola wamekubaliana kulinda haki za watoto na wanawake kwani nchi 12 kati ya 20 ambazo zilikuwa na kiwango kikubwa cha ndoa za lazima na za utotoni ni nchi za Jumuia ya madola”, alisema Kellner.
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa mamilioni ya wasichana kila mwaka kupitia Jumuia ya madola wanapata nafasi ya kuondokana na matokeo ya ndoa za lazima na za utotoni hii si kwao tu bali katika familia zao, jamaa zao na jumuia ya madola.
Jumla ya viongozi wa nchi 53 ambao ni wanachama wa Jumuia ya Madola wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambao utafunguliwa na Malkia Elizabeth wa pili akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete .
Serikali nchini Tanzania kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ,Taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za Kiserikali zinafanyakazi ya kuelimisha jamii ili kuhakikisha kuwa tatizo la ndoa za lazima na za utotoni linamalizika.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.