Monday, June 18, 2012

Taarifa Waziri Membe kwa Waandishi wa Habari

Tanzania imefaidika kwa kiasi kikubwa katika masuala ya kuboresha miundombinu kupitia ushirikiano wa Afrika na Marekani katika uwekezaji na biashara yaani AGOA.

Hayo yalisemwa jana na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alipozongumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu mkutano wa AGOA uliofanyika hivi karibuni mjini California, Washington DC, Marekani.

Mhe. Membe alisema kuwa hadi sasa Tanzania imekwishanufaika na mpango huo kwa kupatiwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 700 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara za Namtumbo-Songea na Mbinga-Mbamba Bay. Aidha, miradi mingine inayonufaika chini ya mpango huo ni ile ya kupambana na malaria na UKIMWI kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Aliongeza kuwa, mkutano huo ambao ulibeba kaulimbiu isemayo “Umuhimu wa Miundombinu katika Kuleta maendeleo Barani Afrika” ulielezea pia faida kwa bara hili kuimarisha miundombinu kuwa ni pamoja na kuhamasisha na kukuza biashara, kuimarisha muungano wa kikanda yaani nchi na nchi na kuimarisha biashara ya ndani ya Bara la Afrika.

Aidha, Mhe. Membe alitumia fursa hiyo pia kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu Wizara ambayo yamekuwa yakiandikwa na kutangazwa na vyombo vya habari isivyo. Masuala hayo ni pamoja na taarifa kuhusu uwasilishwaji wa Ripoti ya Tanzania kuhusu Mpango wa Nchi za Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Katika suala hili Mhe. Membe alitoa ufafanuzi kuwa, ni kweli Mhe. Rais hatoweza kuwasilisha ripoti ya tathmini ya Tanzania katika Mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kufanyika mjini Addis Ababa mwezi Julai, 2012 kwa kuwa Timu ya Umoja wa Afrika chini ya APRM inayopitia ripoti hiyo ya Tanzania haijakamilisha kazi hiyo. Hivyo Tanzania itawasilisha ripoti yake Januari 2013 baada ya timu hiyo kuipitia na si kwa sababu Tanzania inadaiwa Dola za Marekani laki nane (800,000) kama mchango wake kwa mpango huo.

“APRM ni chombo kilichoanzishwa na Serikali za Afrika na kwa hapa Tanzania kinaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje, ni chombo cha hiari kwa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe kiutawala bora, si kweli kuwa Rais atashindwa kuwasilisha Ripoti ya Tanzania AU kwa sababu hatujalipa deni, bali ni kwa sababu timu inayopitia ripoti hiyo ya Tanzania haijakamilisha kazi yake hivyo tunatarajia kuwasilisha ripoti yetu mwezi Januari 2013 wakati wa kikao kingine cha Wakuu wa nchi wa AU,” alisema Mhe. Membe.

Kuhusu suala la fedha zilizotoweka Wizarani, Mhe. Membe alieleza kuwa hakuna fedha zilizopotea isipokuwa Wizara imewasimamisha kazi Watumishi watano waliofanya mchakato wa kuhamisha kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kutoka Hazina kuja Wizarani kwa ajili ya ziara za Mhe. Rais za Addis Ababa, Geneva, Brazil na Arusha bila kibali cha Afisa Masuuli yaani Katibu Mkuu ambaye hakuwepo wakati mchakato huo unafanyika.

Aliongeza kuwa, Watumishi hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi unaofanywa na kamati iliyoundwa ili kujiridhisha kama taratibu za kifedha zilifuatwa au kukiukwa katika mchakato huo mzima.

“Tarehe 1 Machi, 2012 wakati mimi sipo Wizarani wala Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mhasibu Mkuu kuna mchakato wa kuhamisha fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.5 ulifanywa kutoka Hazina kuja Wizarani kwa ajili ya safari za Mhe. Rais za Geneva, Addis Ababa, Brazil na Arusha bila kibali cha Afisa Masuuli. Timu inayojumuisha watu kutoka TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Wizara na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali imeundwa ili kuchunguza suala hilo ili kujua kama taratibu za kifedha zilifuatwa au kukiukwa na uchunguzi ukikamilika tutaweka hadharani hakuna cha kuficha,” alisema Mhe. Membe.

Vile vile, Mhe. Membe alipinga uvumi unaoenezwa kuwa amekitabiria ushindi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kwa kusema kuwa yeye si mtabiri na kwamba yeye ni mwanachama halisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa maneno na kwa matendo. Mhe. Membe aliongeza kuwa alichokifanya ni ukarimu kwa kuwakaribisha Vijana wa CHADEMA jimboni kwake Mtama mkoani Lindi na kushiriki nao chakula nyumbani kwake.

“Ukarimu hauna udini, rangi wala itikadi, vijana wa CHADEMA walikuja nikawakaribisha kwa chakula nyumbani, na leo nataka niwape somo kidogo, upinzani sio uadui, nchi inayoona upinzani ni uadui haiko salama wala haitaendelea,”alisisitiza Mhe. Membe.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.