Sunday, June 10, 2012

Ujerumani yaingia makubaliano na Tanzania


Serikali ya Tanzania na ya Ujerumani zimeweka saini Mkataba ambao utaruhusu wenza na wategemezi wa wafanyakazi katika Balozi kuweza kufanya kazi wakiwa katika nchi hizo.
 
Mkataba huo ulisainiwa jijini Dar es Salaam tarehe 8 Juni, 2012 kati ya Bw. John M. Haule, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mhe. Klause Peter Brandes, Balozi wa Ujerumani  hapa nchini kwa niaba ya ya Serikali yake.
 
Katika maelezo yake baada ya kusaini mkataba huo, Bw. Haule alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo kutatoa fursa kwa wenza na wategemezi wa wanadiplomasia kufanya kazi wakiwa katika nchi hizo na kuwasaidia kuendeleza taaluma zao na kuongeza kipato katika familia zao.
 
“Dhumuni kubwa la kusaini mkataba huu leo ni kutoa fursa kwa wenza na wategemezi wa wanadiplomasia wetu katika Balozi kuweza kufanyakazi katika nchi hizi mbili na kwa mantiki hiyo wataweza kuendeleza taaluma zao na pia kuongeza kipato kwa familia zao” alisema Bw. Haule.
 
Aidha, aliongeza kuwa, Tanzania inakuwa nchi ya pili kwa Afrika kupata fursa hii ya kusaini mkataba na Ujerumani ambapo nchi nyingine ni Zambia. Vile vile, Tanzania imekwisha saini mkataba kama huu na nchi za Marekani na Canada.
 
Kwa upande wake Balozi Brandes alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huu ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani na kwamba ni moja ya mafanikio makubwa ya ushirikiano huo.
 

 
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.