Monday, August 31, 2020

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NJE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA KENYA NCHINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 31 Agosti 2020 kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye nyanja za diplomasia, biashara na uwekezaji. Pia Balozi Kazungu alitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya uchumi wa kati pamoja na kuongoza kwa mafanikio Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kadhalika aliitakia Tanzania uchaguzi wa amani na mafanikio hapo mwezi Oktoba 2020. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Generali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu

Sehemu ya ujumbe uliofuatana na Balozi Ibuge ukifuatilia mazungumzo. Kushoto ni Bw. Hangi Mgaka, Katibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Bw. Isaac Isanzu, Afisa Mambo ya Nje.

Balozi Dan Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha zinazowaonesha waasisi wa mataifa ya Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta na Uganda, Hayati Mzee Milton Obote. Balozi Ibuge alizipokea picha hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye aliahidiwa picha hizo na Serikali ya Kenya wakati wa ziara yake nchini humo mwezi Novemba 2019.

Mhe. Balozi Kazungu akimkabidhi Balozi Ibuge zawadi ya picha inayowaonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta. Picha hiyo ilipigwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Rais Kenyatta aliyoifanya hapa nchini mwezi Julai 2019.








 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.