Thursday, December 17, 2015

WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE BADO WAPO NYUMA KATIKA MATUMIZI YA TEHAMA

Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa   Tanzania katika Umoja wa Mataifa  akizungumza wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia ya  Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo. Mkutano huo wa siku mbili umefanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
Na  Mwandishi Maalum,  New York

Wanawake na watoto wa kike wanaelezwa kama kundi ambalo bado  halijanufaika ipasavyo na  matumizi ya   Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA)

Na kwa sababu  hiyo, wito umetolewa  kwa nchi Wanahama wa Umoja wa Mataifa, Asasi za Kiraia naTaasisi za Kimataifa   kuhakikisha kwamba panakuwep  na mikakati na mipango ya  ziada yenye lengo la  kupunguza pengo la matumizi ya TEHAMA kati ya wanawake na wanaume.

Hayo yamejiri wakati wa  Mkutano wa siku mbili  wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa   uliokuwa ukitathmini utekelezaji   wa Teknolojia na  Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo, ikiwa ni miaka kumi tangu mchakato wa kuhakisha kuwa  jamii inapata fursa ya  kupata na kutumia TEHAMA ambayo itakuwa   ni jumuishi na yenye gharama nafuu.

Wajumbe wa  mkutano huu walikuwa ni   Mawaziri  wanaohusika na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa  Ban Ki Moon, na Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Monges Lykketofts ni baadhi ya viongozi wakuu waliozungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu.

Ujumbe wa Tanzania  umeongozwa na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba yake mbele ya  wajumbe wa Mkutano, Balozi Manongi,  amesema Serikali inalichukulia kwa  umuhimu wa kipekee  suala   upatikanaji, uboreshaji, usambazaji na  matumizi ya TEHAMA kwa  wananchi wake.

Akasema katika kuhakikisha kuwa TEHAMA  inakwenda na wakati na inawafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu, serikali imekuwa ikishirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje.  

Akasema kama  ilivyo kwa   nchi nyingine zinazoendelea, Tanzania ingependa kuona panakuwapo na ushirikiano zaidi na wenye tija baina ya mataifa yaliyoendelea  na yanayoedelea hususani katika eneo la    uwezeshawaji wa kiteknolojia,raslimali fedha na mafunzo.

Balozi Manongi, na kama  iliyokuwa  kwa wazungumzaji wengine, amesema   ingawa matumizi ya TEHAMA yamekuwa na manufaa makubwa kwa mwanadamu katika Nyanja mbalimbali, lakini pia pamekuwapo na changamoto kadhaa zitokanazo na matumizi mabaya.

Baadhi ya  changamoto hizo ni matumizi  yasiyo sahihi ya mitandao, ukiwamo uhalifu wa  mitandao , ugaidi, uingiliaji wa masuala binafsi ya mtu, ukiukwaji wa maadili,  usambazaji wa matamshi ya chuki na  misimamo mikali.

Akabainisha pia kuwa pamezuka tabia sugu  ( addiction) ya
matumizi ya TEHAMA kiasi  cha kudhoofisha mahusiano miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.


Kama hiyo haitoshi matumizi sugu ya TEHAMA  yamezalisha tatizo jingine la watu kujikuta wakipata magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kwamba
wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye TEHAMA pasipo kuishughulisha   miili yao.


Mwakilishi  huyo wa Tanzania akasema panahitajika juhudi za   pamoja katika kuzikabili  changamoto hizo na nyingine  nyingi.

Wazungumzaji wengi katika  mkutano huo  pamoja na  kubainisha  kuachwa nyuma kwa wanawake na watoto wakike  katiika matumizi ya TEHAMA, walieleza pia kwamba kundi jingine ambalo nalo halijanufaika   na  TEHAMA ni watu wenye ulemavu.

Pia ilielezwa wakati wa mkutano huo kuwa  ingawa asilimia 40 ya  idadi ya watu wote duniani wamepata fursa ya kutumia TEHAMA, bado kuna pengo kubwa baina ya watumiaji kati ya mataifa yanayoendelea na yale yaliyoendelea.

Halikadhalika imebainishwa kwamba kuna pengo  pia miongoni wa watumiaji hao kati ya wale wa mijini na vijijini lakini pia uwezo wa kipato nalo ni tatizo linalosababisha siyo kila mtu anakuwa na uweze wa kumudu gharama za matumizi ya TEHAMA.



Baadhi ya wazungumzaji
wengine walikwenda mbali Zaidi kwa kueleza kwamba TEHAMA ni  muhimu sana kwa utekelezaji wa  ajenda mpya ya maendeleo endelevu lakini pia
ni muundombinu  muhimu ambao hauna
tofauti na miundombinu mingine kama vile barabara. 

Wednesday, December 16, 2015

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa SADC na Balozi wa Marekani nchini

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akimkaribisha Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipofika Wizarani kwa ajili ya kumpongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa huo na pia kumpatia taarifa fupi kuhusu muundo, majukumu na utendandaji wa Jumuiya ya SADC.Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Desemba, 2015.
Mhe. Dkt. Mahiga akimweleza jambo Dkt. Tax wakati wa mazungumzo yao.
Wajumbe waliofutana na Mhe. Dkt. Tax wakinukuu mazungumzo ya viongozi hao ambao hawaonekani pichani.
Mhe. Dkt. Tax akifafanua jambo kwa Mhe. Dkt. Mahiga.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Innocent Shiyo akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga pamoja na Bw. Thobias Makoba, Msaidizi wa Waziri.
Mazungumzo yakiendelea

..........Mkutano na Balozi wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akimkaribisha  Balozi wa Marekani hapa nchini, Mhe. Mark Childress alipofika Wizarani kwa lengo la kumpongeza  kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kwenye wadhifa huo na pia kuzungumzia masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani.
Mhe. Dkt. Mahiga akizungumza na Balozi Childress ambapo alimhakikishia ushirikiano Balozi huyo.
Balozi Childress nae akizungumza.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali pamoja na Msaidizi wa Waziri, Bw. Thobias Makoba nao wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Mahiga na Balozi Childress (hawapo pichani).
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea
Picha na Reginald Philip

Wafanyabiashara wa Qatar wahimizwa kuwekeza Tanzania


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kutoka Qatar kutumia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini. 


Balozi Mulamula aliyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Qatar iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regence, Kilimanjaro jijini Dar es Salaam jana.


“Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, madini, uchukuzi, elimu, afya, nishati, wanyamapori, mafuta na gesi, hivyo natoa wito kwa ndugu zetu wa Qatar watumie fursa ya uhusiano mzuri tulionao kuja kuwekeza nchini”, Balozi Mulamula alisema.  


Balozi Mulamula aliendelea kusema kuwa Serikali inaelekea katika uchumi wa gesi na ina matumani makubwa ya kufaidika na uzoefu wa mshirika wake Qatar ambayo ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa gesi duniani. 


Suala lingine ambalo Katibu Mkuu aliligusia ni umuhimu wa Tanzania na Qatar kuunganisha nguvu ili kutumia rasilimali fedha na ardhi zilizopo kuimarisha sekta ya kilimo kwa madhumuni ya kuodoa changamoto za usalama wa chakula kati ya nchi hizi mbili.


Kwa upande wake, Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdulla Jassim Al Maadadi pamoja na mambo mengine, aliongelea suala la Qatar kuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu wa Kombe la Dunia kwa mwaka 2022. Alisema miradi mingi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2020.  Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara, mtandao wa reli, viwanja vya mpira, viwanja vya ndege na nyumba za makazi.


Alisema miradi hiyo ni mikubwa hivyo inahitaji wafanyakazi wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani na aliahidi kuwa watu watakaokwenda kufanya kazi nchini humo, haki zao zitalindwa.



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Liberata Mulamula akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha ya Siku ya Taifa la Qatar kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Augustine Mahiga. Katika maadhimisho hayo, Balozi Mulamula alisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar hususan katika sekta za kiuchumi na biashara.
Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani)
Balozi Mulamula akiendelea kuzungumza
Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdallah Jassim Al-Maadadi naye akizungumza katika maadhimisho hayo.
Sehemu nyingine ya Mabalozi waliohdhuria hafla hiyo.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Hangi Mgaka (wa kwanza kulia), na Bw. Batholomeo Jungu (wa pili kutoka kulia) nao wakimsikiliza Balozi Al-Maadadi (hayupo), katika maadhimisho hayo.
Balozi Mulamula (wa pili kutoka kulia), Balozi wa Qatar nchini (wa tatu kutoka kulia), Balozi wa Demokrasia ya Kongo, Mhe. Juma Mpango (wa nne kutoka kushoto), Balozi wa Oman nchini, Mhe. Soud Ali Bin Mohamed Al Rugaishi (wa kwanza kushoto), Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Al suwaidi (wa pili kutoka kushoto) wakishiriki tendo la kukata Keki ya maadhimisho ya Siku ya Taifa la Qatar.
Balozi Mulamula akizungumza na Balozi Al - Maadadi.
Balozi Mulamula akimtangaza mshindi wa bahati nasibu iliyochezeshwa hapo jana, mshindi huyo (hayupo pichani) alijishindia tiketi ya Ndege ya kuelekea Doha.
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Al-Maadadi
Katibu Mkuu Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi waliohudhuria maadhimisho hayo.


Picha na Reginald Philip

Tuesday, December 15, 2015

Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Seiji Kihara yaliyofanyika katika Ofisi ya Wizara hiyo leo.

Walioshuhudia mazungumzo hayo kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mbelwa Kairuki, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi, Mindi Kasiga na Katibu wa Waziri, Bw. Thobias Makoba.
Katikati ni Balozi wa Japani Mhe. Masahau Yoshinda nchini akiwa na Maofisa kutoka Serikali ya Japan.
Mazungumzo yanaendelea.
Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akikabidhi zawadi ya picha kwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan.
Balozi Mahiga akiagana na Mgeni wake Mhe. Kihara.


TAARIFA FUPI YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA KUHUSU UHUSIANO KATI YA JAPAN NA TANZANIA TAREHE 15 DESEMBA 2015


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo leo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Seiji Kihara ambaye aliwasili nchini jana kama Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Japan Mhe.  Shinzo Abe ambapo kesho tarehe 16 Desemba 2015 anatarajiwa kuwasilisha Ujumbe wa Waziri Mkuu wa Japan kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.   Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Pamoja  na kuwasilisha ujumbe kwa Mheshimiwa Rais, mgeni huyo anatarajiwa kuhudhuria hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mkopo wa dola za kimarekani milioni 96 utakaotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wa Kenya na Tanzania wenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka Singida na Manyara kupitia Babati na Arusha mpaka Namanga.


          MAHUSIANO KATI YA TANZANIA NA JAPAN
Tanzania na Japan zimekuwa katika uhusiano na ushirikiano wa karibu mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru wake. Mahusiano hayo yamekuwa yakikua na kuimarika miaka hadi miaka katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, nishati, Kilimo, biashara, viwanda, usafirishaji na uwekezaji.  Kufanyika kwa ziara hii ya Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan ni muendelezo wa kukuza ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.


            MIRADI MIPYA ITAKAYOFADHILIWA NA SERIKALI YA JAPAN



Serikali imeingia makubaliano na Serikali ya Japan kutekeleza miradi mitatu ya ujenzi wa barabara yenye lengo la kupunguza tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam linaloathiri uchumi wa nchi yetu. Miradi hiyo ni pamoja na:



    Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Juu katika eneo la TAZARA (TAZARA flyover):

Mkataba wa ujenzi wa Barabara hiyo tayari ulikwishasainiwa tangu tarehe 15 Oktoba 2015 na ujenzi unategemewa kuanza mapema mwakani.



              Mradi ya Ujenzi wa Barabara ya Morocco – Mwenge

Serikali ya Japan itafadhili upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco ili kuweza kupunguza msongamano wa magari.  Upanuzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.  Tayari Serikali imekwishaanza hatua za mwanzo za ujenzi wa barabara hiyo kufuatia uamuzi wa Mhe. Rais kuelekeza fedha zilizokuwa zigharamie sherehe za uhuru zitumike kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo.


            Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Gerezani mpaka bendera tatu

Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa fedha za msaada kutoka Serikali ya Japan. Ujenzi wa barabara hii nao unatarajiwa kuanza mwakani.



Mbali na miradi ya ujenzi wa barabara, Serikali ya Japan imeingia makubaliano na Serikali ya Tanzania kutekeleza miradi ya umeme kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa matumizi ya wananchi na viwandani kama ilivyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM.    Miradi itakayotekelezwa kwa ufadhili kutoka Japan ni pamoja na:



 Mradi ya Ujenzi wa Njia ya Kusafirishia Umeme Kenya – Tanzania Power Interconnection Project


Mradi huu una lengo la kuimarisha usambazaji kwa kuuza na  kununua umeme katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Kenya. Ni ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wenye KV400 na urefu wa kilomita 414.5 kutoka Singida na Namanga kupitia Babati na Arusha.

Mkataba wa mradi huu unatarajiwa kutiwa saini baadaye leo Wizara ya Fedha na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi wa  Mambo ya Nje wa Japan.



    Ujenzi wa mradi wa Mtambo wa kuzalisha umeme katika eneo la Kinyerezi (Kinyerezi II power plant project).



Mkataba wa ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 300 huko Kinyerezi ulisainiwa  tarehe 27 Machi 2015 kati ya Serikali na Benki ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Japan (Japan Bank for International Cooperation – JBIC).  Utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa kuanza mapema mwakani.