Thursday, December 17, 2015

WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE BADO WAPO NYUMA KATIKA MATUMIZI YA TEHAMA

Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa   Tanzania katika Umoja wa Mataifa  akizungumza wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia ya  Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo. Mkutano huo wa siku mbili umefanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
Na  Mwandishi Maalum,  New York

Wanawake na watoto wa kike wanaelezwa kama kundi ambalo bado  halijanufaika ipasavyo na  matumizi ya   Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA)

Na kwa sababu  hiyo, wito umetolewa  kwa nchi Wanahama wa Umoja wa Mataifa, Asasi za Kiraia naTaasisi za Kimataifa   kuhakikisha kwamba panakuwep  na mikakati na mipango ya  ziada yenye lengo la  kupunguza pengo la matumizi ya TEHAMA kati ya wanawake na wanaume.

Hayo yamejiri wakati wa  Mkutano wa siku mbili  wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa   uliokuwa ukitathmini utekelezaji   wa Teknolojia na  Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo, ikiwa ni miaka kumi tangu mchakato wa kuhakisha kuwa  jamii inapata fursa ya  kupata na kutumia TEHAMA ambayo itakuwa   ni jumuishi na yenye gharama nafuu.

Wajumbe wa  mkutano huu walikuwa ni   Mawaziri  wanaohusika na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa  Ban Ki Moon, na Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Monges Lykketofts ni baadhi ya viongozi wakuu waliozungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu.

Ujumbe wa Tanzania  umeongozwa na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba yake mbele ya  wajumbe wa Mkutano, Balozi Manongi,  amesema Serikali inalichukulia kwa  umuhimu wa kipekee  suala   upatikanaji, uboreshaji, usambazaji na  matumizi ya TEHAMA kwa  wananchi wake.

Akasema katika kuhakikisha kuwa TEHAMA  inakwenda na wakati na inawafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu, serikali imekuwa ikishirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje.  

Akasema kama  ilivyo kwa   nchi nyingine zinazoendelea, Tanzania ingependa kuona panakuwapo na ushirikiano zaidi na wenye tija baina ya mataifa yaliyoendelea  na yanayoedelea hususani katika eneo la    uwezeshawaji wa kiteknolojia,raslimali fedha na mafunzo.

Balozi Manongi, na kama  iliyokuwa  kwa wazungumzaji wengine, amesema   ingawa matumizi ya TEHAMA yamekuwa na manufaa makubwa kwa mwanadamu katika Nyanja mbalimbali, lakini pia pamekuwapo na changamoto kadhaa zitokanazo na matumizi mabaya.

Baadhi ya  changamoto hizo ni matumizi  yasiyo sahihi ya mitandao, ukiwamo uhalifu wa  mitandao , ugaidi, uingiliaji wa masuala binafsi ya mtu, ukiukwaji wa maadili,  usambazaji wa matamshi ya chuki na  misimamo mikali.

Akabainisha pia kuwa pamezuka tabia sugu  ( addiction) ya
matumizi ya TEHAMA kiasi  cha kudhoofisha mahusiano miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.


Kama hiyo haitoshi matumizi sugu ya TEHAMA  yamezalisha tatizo jingine la watu kujikuta wakipata magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kwamba
wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye TEHAMA pasipo kuishughulisha   miili yao.


Mwakilishi  huyo wa Tanzania akasema panahitajika juhudi za   pamoja katika kuzikabili  changamoto hizo na nyingine  nyingi.

Wazungumzaji wengi katika  mkutano huo  pamoja na  kubainisha  kuachwa nyuma kwa wanawake na watoto wakike  katiika matumizi ya TEHAMA, walieleza pia kwamba kundi jingine ambalo nalo halijanufaika   na  TEHAMA ni watu wenye ulemavu.

Pia ilielezwa wakati wa mkutano huo kuwa  ingawa asilimia 40 ya  idadi ya watu wote duniani wamepata fursa ya kutumia TEHAMA, bado kuna pengo kubwa baina ya watumiaji kati ya mataifa yanayoendelea na yale yaliyoendelea.

Halikadhalika imebainishwa kwamba kuna pengo  pia miongoni wa watumiaji hao kati ya wale wa mijini na vijijini lakini pia uwezo wa kipato nalo ni tatizo linalosababisha siyo kila mtu anakuwa na uweze wa kumudu gharama za matumizi ya TEHAMA.



Baadhi ya wazungumzaji
wengine walikwenda mbali Zaidi kwa kueleza kwamba TEHAMA ni  muhimu sana kwa utekelezaji wa  ajenda mpya ya maendeleo endelevu lakini pia
ni muundombinu  muhimu ambao hauna
tofauti na miundombinu mingine kama vile barabara. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.