Monday, December 21, 2015

Tanzania yaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kukabiliana na magonjwa ya mlipuko


Bw. Noel Kaganda, Afisa Mwandamizi, Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza kwa niaba ya Tanzania wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokutana mwishoni mwa wiki kujadili suala la Afya na Sera ya Mambo ya Nje

  ===============================
JUMUIYA YA KIMATAIFA IJIZATITI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO - TANZANIA


Mwishoni mwa wiki, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilijadili ajenda ya Afya na Sera ya Mambo ya Nje ambapo pamoja na mambo mengine lilipitisha azimio linalotathmini utayari wa nchi wanachama kukabiliana na magonjwa ya milipuko na dharura nyingine za kiafya.

Katika mjadala huo, wazungumzaji wengi walisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo ya afya, hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati zisizo na uwezo wa kutosha wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Aidha, walieleza umuhimu wa kung’amua mafunzo muhimu ya janga la ugonjwa wa Ebola uliosababisha maafa makubwa katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Akichangia katika mjadala huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Bw. Noel Kaganda, Afisa Mwandamizi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa alibainisha kuwa pamoja na jitihada zilizolenga kuimarisha sekta ya afya katika kipindi kilichomalizika cha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile upungufu wa madaktari na wauguzi; vifaa finyu na vichakavu; na mazingira yasiyo salama.

Alisisitiza kuwa, jitihada za kuboresha afya ya binadamu, hususan ya akina mama na watoto, lazima ziendelezwe kwa ufanisi zaidi katika muktadha wa Agenda ya Maendeleo Endelevu  hadi kufikia mwaka 2030.

Aliongeza kuwa pamoja na kuzuia vifo vya watoto wachanga, ambavyo idadi yake ulimwenguni kwa mwaka 2015 imefikia milioni 6, sawa na vifo 16,000, jumuiya ya kimataifa haina budi kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile Ebola na mengineyo, ambayo yanaweza kuathiri jamii nyingi duniani kufuatia kushamiri kwa utandawazi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na binadamu.

Pamoja na kusisitiza kuwa wananchi wote wapatiwe huduma bora za afya, Tanzania iliunga mkono mapendekezo ya ripoti ya wa Shirika la Afya Duniani kuhusu ulinzi na ustawi wa watumishi katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watumishi wengi wa sekta ya afya wanazalilishwa na kushambuliwa wakiwa kazini na wanaathirika na majanga mengine kama vile Tsunami na matetemeko ya ardhi. Tanzania ilisema kuwa vitendo hivyo vinachangia katika kuzorota kwa sekta ya afya, hivyo ilitaka vikomeshwe mara moja. Pia ilipendekeza wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Vilevile ilitaka watumishi wa sekta ya afya wapatiwe mafunzo na zana za kujilinda na maambukizi, ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kadhalika ilisisitiza umuhimu wa mashirikiano baina ya nchi wanachama na wadau wengine wa afya, kama vile Shirika la Afya Duniani, yenye lengo la kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imekuja siku chache kabla ya jopo la Ngazi ya Juu lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupendekeza namna bora ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko duniani. Jopo hilo linaloongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, linatarajia kuwasilisha taarifa yake mwezi Januari 2016.

Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeazimia kufanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu “antimicrobial resistance - AMR” kwa lengo la kubaini kiini cha magonjwa sugu kama kama ilivyo kwa baadhi ya jamii za ugonjwa wa Kifua Kikuu.

=Mwisho=

 


WAZIRI WA MAMBO YA NJE AKAGUA UJENZI WA MAHAKAMA YA UMOJA WA MATAIFA JIJINI ARUSHA

Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akipata maelekezo ya ziada kuhusu ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Lakilaki Jijini Arusha. Aneyetoa maelezo ni Afisa Mambo ya Nje na Mwansheria Bw. Elisha Suku. Kushoto kwa Waziri Mahiga ni Nd. Hamdouny Mansour, Katibu Tawala Msaidizi upande wa miundombinu. 



Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na ujumbe wake wakiangalia eneo la eka 16 ambapo majengo manne ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa yanajengwa. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Mwezi Aprili mwaka 2016.
 Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha Mhe. Wilson Nkhambaku baada ya kukagua eneo hilo na kuridhika na kasi ya ujenzi uliozingatia viwango vya kimataifa na vile vya Umoja we Mataifa. 

Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na ujumbe wake baada ya kumaliza ukaguzi wa ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa jijini Arusha. 




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  
Serikali imeridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Masalia ya kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT) katika eneo la Lakilaki jijini Arusha, uliozinduliwa rasmi Julai mosi mwaka huu.

Akikagua ujenzi huo na kupokea taarifa kutoka kwa wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa majengo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, amesisitiza kuwa ujenzi huo uzingatie viwango vya kimataifa ili kuhakikisha usalama wa nyaraka na ushahidi utakaohifadhiwa kwenye majengo hayo.

Alieleza kuwa ahadi ya Serikali iko palepale kushirikiana na Umoja wa Mataifa na kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme na maji vinapatikana kwenye eneo hilo ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi ya kuridhisha.

“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi huu kwani hii ilikua kazi yangu ya mwisho nilipokuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kule Umoja wa Mataifa, kutetea mahakama hii ijengwe hapa Arusha.

Akifafanua miundombinu iliyowekwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala Msaidizi upande wa miundombinu Nd. Hamdouny Mansour alisema kuwa kwa upande wa upatikanaji wa maji, mkoa umefanikisha upatikanaji wa bomba maalum linaloleta maji kwenye eneo la ujenzi mojakwamoja bila kuathiri upatikanaji wa maji maeneo mengine pembezoni ili kutimiza azma hiyo ya Serikali.

Ujenzi huo wa Mahakama unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwa na majengo makuu manne; jengo la mahakama, jengo la uhifadhi wa nyaraka, jengo la ulinzi na jengo la ofisi za Umoja wa Mataifa. Msimamizi wa ujenzi wa Umoja wa Mataifa alielezea teknolojia ya kisasa itakayotumika kujenga jengo la kuhifanyia nyaraka haitahitaji kutumia viyoyozi ili kuhifadhi uhasilia wa nyaraka.

Kwa upande wa wakandarasi wanaojenga ambao ni kampuni kutoka India walielezea changamoto iliyopo kwenye ujenzi huo ni kutekeleza mpango wa kupanda mti aina ya mshita-acacia, utakaomaanisha haki ambayo kihistoria na jadi za kiafrika ilipatikana kwa mazungumzo kwenye mabaraza ya kijiji. Mti huo wa mshita au Tree of Justice utapandwa ndani katikati ya majengo hayo manne.

Serikali kupitia Hazina ilinunua eneo hilo la Lakilaki lenye ekari 431 na kukabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje ambapo limetengwa mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa taasisi mbalimbali za kimataifa. Taasisi nyingine zinazotarajiwa kujengwa kwenye eneo hilo ni African Union Advisory Board on Corruption (AUABC), African Institute of International Law (AIIL) na African Court on Human and Peoples' Rights (ACHPR).

Ujenzi wa majengo haya ya awali kwenye eneo la Lakilaki unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwakani. Ujenzi huo ulizinduliwa rasmi Julai mwaka huu wa 2015 na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

20 Desemba, 2015

Friday, December 18, 2015

Dkt. Mahiga afanya mahojiano maalum na BBC kuhusu Burundi

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akijibu maswali kuhusu hali ya kisiasa nchini Burundi wakati wa mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari kutoka Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Bw. Leonard Mubali. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga akinukuu mahojiano hayo. Mahojiano hayo yatarushwa  tarehe 18 Desemba, 2015 saa 3:00 usiku kupitia kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na  Kituo cha Star TV
Mahojiano yakiendelea.
Mhe.Dkt. Mahiga akiagana na Bw. Mubali  baada ya kumaliza  mahojiano hayo.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHE. DKT. AUGUSTINE MAHIGA
 MKOANI ARUSHA
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Arusha kuanzia kesho Jumamosi tarehe 19 Desemba 2015.

Atakapokuwa mkoani Arusha, Balozi Mahiga atafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Richard Sezibera. Mazungumzo yao yatahusu namna ya kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.

Aidha, Mhe. Waziri atatembelea eneo la Lakilaki ambalo limetengwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za taasisi za kimataifa. Ujenzi unaoendelea hivi sasa kwenye eneo hilo ni jengo la ofisi la taasisi ya Mechanism for Crime Tribunals (MICT) inayorithi shughuli za Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ambayo itakamilisha shughuli zake tarehe 31 Desemba 2015.

Mhe. Waziri pia atatembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kuonana na uongozi wa Kituo hicho  kwa madhumuni ya kufahamiana. AICC ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Mhe. Waziri atarejea jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili tarehe 20 Desemba 2015.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
18 Desemba, 2015

Balozi Mulamula akutana kwa mazungumzo na Balozi wa India nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (kulia), akizungumza na Balozi wa India hapa nchini, Mhe. Sandeep Arya katika mazungumza yao yalijikita katika kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na India katika sekta mbalimbali za kiuchumi, biashara, afya na elimu. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 18 Desemba, 2015.
Balozi Arya naye akizungumza na Balozi Mulamula
Mazungumzo yakiendelea

Picha na Reginald Philip