Thursday, November 24, 2016

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.  Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo na waandishi wa  habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam. Katika mazungumzo hayo. Mhe. Waziri aliwahabarisha kuhusu ziara ya Rais wa Zambia, Mhe Edgar Lungu anayetarajiwa kuifanya nchini kuanzia tarehe 27 - 29 Novemba 2016.
Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari 


Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma  akielezea jambo kwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo (hawapo pichani), wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo naye akielezea faida zitakazo tokana na ziara nzima ya Rais wa Zambia
Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa katika kikao na Waziri Mahiga.

1.Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu kuzuru Tanzania Novemba 27 - 29, 2016

UTANGULIZI

1.1        Ndugu waandishi, nimewaita leo ili kuwaeleza kuhusu Ziara Rasmi hapa nchini ya Mhe. Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambiainayotarajiwa kufanyika hapa nchini. Najua baadhi yenu mtakuwa mmekwishasikia taarifa za Rais huyokufika nchini hivi karibuni.

1.2        Sasa niwatangazie rasmi kuwa taarifa hiyo ni sahihi na ziara hiyo itafanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2016. Hii ni ziara Rasmi ya kwanza kwa Mhe. Rais Lungu kuifanya nchini tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mwezi Septamba, 2016.

1.3        Ndugu Waandishi, mnafahamu kwamba, mbali na kuwa nchi majirani, mahusiano  kati ya nchi za  Tanzania na Zambia yana historia ndefu, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mzee Kenneth Kaunda wa Zambia.

1.4        Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ya karibu ndipo nchi za Tanzania na Zambia kwa pamoja zilifanya uamuzi wa kihistoria wa kutekeleza mradi mkubwa wa ushirikiano wa ujenzi wa Reli ya TAZARA. Licha ya kwamba mradi huo ni wa kimaendeleo, lakini pia Reli hiyo ya TAZARA ilitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika, wakati ambapo Tanzania na Zambia zikiwa miongoni mwa nchi ziizokuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi (Frontline States).

1.5        Mradi mwingine mkubwa ambao nchi zetu mbili zimeufanya kwa ushirikiano ni mradi wa Bomba la Mafuta la TAZAMA.

Ndugu waandishi, haya, pamoja na mengineyo mengi ambayo nitayaeleza baadaye, yanaufanya ugeni huu kuwa wa muhimu na wa heshima kubwa sana kwetu.

1.6        Mhe. Rais Lungu anafika nchini kufutia mwaliko rasmi kutoka kwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa nchini, pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Magufuli. Mhe. Rais Lungu ataambatana na Maafisa wengine Waandamizi wa Serikali ya Zambia.

2.0       RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI

Ndugu Waandishi, sasa niwaeleze kwa kifupi ratiba ya ziara hiyo.

2.1        Mhe. Rais Lungu anatarajiwa kuwasili nchini siku ya jumapili tarehe 27Novemba 2016saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu ambapo atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo atapigiwa mizinga 21 ya kijeshi kwa heshima yake kumkaribisha nchini.

2.2        Siku inayofuata ya tarehe 28 Novemba 2016 asubuhi, Mhe. Rais Lungu atatembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya TAZARA ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo la ubia baina ya nchi zetu mbili. Baada ya kutoka TAZARA, Mhe. Lungu atazuru pia Shirika la Bomba la Mafuta la TAZAMA, ambapo atatembelea mitambo ya kupampu mafuta, pamoja na matenki ya kuhifadhi mafuta ya TAZAMA vyote vilivyopo eneo la Kigamboni.

2.3        Baada ya ziara hizo za asubuhi, Mhe. Rais Lungu pamoja na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli, pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yatafanyikia Ikulu kuanzia saa 5 kamili? mchana.

2.4        Baada ya mazungumzo rasmi, Mhe. Rais Lungu pamoja na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali minne(4) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniakwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi zetu mbili.

2.5        Jioni ya siku hiyo, Mhe. Rais Lunguatahudhuriadhifa ya kitaifa(State Banquet) itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 12 na nusu jioni. Hilo ndilo litakuwa tukio la mwisho kwa siku ya kwanza hiyo.

2.6        Siku itakayofuata ya tarehe 29 Novemba 2016, Mhe. Rais Lungu atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo atajionea shughuli mbalimbali za upokeaji na upitishwaji wa mizigo bandarini hapo. Baada ya tukio hilo, Mhe. Rais Lungu atafanya ziara fupi kwenye Kampuni ya kusafirisha mizigo inayomilikiwa na Zambia inayojulikana kama Zamcargo.

2.7        Baada ya hapo Mhe. Rais Lungu ataelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere ambapo ataagwa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli kurejea nchini Zambia.

3.0       MANUFAA YA ZIARA HIYO

3.1        Ndugu Waandishi, kama nilivyoeleza awali, mahusiano yetu na Zambia ni ya kidugu na yana historia ndefu. Kupitia uhusiano huo, Tanzania na Zambiazimeendelea kufanya kazi kwa kuaminiana na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Hivyo, ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, itatoa fursa ya kuimarisha zaidi mahusiano hayo kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa Tanzania na Zambia.

3.2         Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi, ziara hiyo inatarajiwa kuzidisha zaidi uhusiano katika maeneo bayana kama ifuatavyo:

a).  Kukuza ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa Reli ya TAZARA:
·        Kama nilivyoeleza hapo awali, Reli ya TAZARAni mhimili na kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na Zambia, lakini pia na kwa nchi nyingine majirani za ukanda wa kusini na kati mwa Afrika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Malawi n.k. Reli hiyo inatoa huduma ya usafirishaji wa mizigo, rasilimali ghafi pamoja na abiria katika nchi hizo.

·        Hata hivyo, kama ambavyo wengi wenu mtakuwa mnafahamu, ufanisi wa Reli ya TAZARA umekuwa chini ya matarajio ya wadau wa sekta hiyo ya usafiri. Serikali za Tanzania na Zambia kama wamiliki wa Reli hiyo kwa ubia sawa wa 50% kwa 50% zimeendeleakuchukua hatua mbalimbali kuisaidia TAZARA, hususan kwa kushirikiana na marafiki zetu Serikali ya China.

·        Napenda kuwataarifu kuwa, katika ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala hili la TAZARA litajadiliwa kwa kina baina ya viongozi hao wawili ili Shirika hilo liweze kuongeza ufanisi na kujiendesha kwa tija kibiashara.

b). Kukuza Ushirikiano katika Matumizi ya Bomba la TAZAMA.
·        Ndugu waandishi, bomba la TAZAMA lilijengwa mwaka 1968 kwa lengo la kutoa njia nafuu ya Kusafirisha mafuta ghafi kwenda nchini Zambia na hivyo kuiepusha nchi hiyo na athari za kupanda kwa bei ya mafuta. Hata sasa umuhimu wa bomba hilo bado upo.

·        Nchi zetu mbili zinamiliki bomba hilo kwa ubia ambapo Zambia ina mtaji wa mbili ya tatu na Tanzania inamiliki bomba hilo kwa mtaji wa moja ya tatu. Bomba hilo limekuwa likijiendesha kibiashara kwa faida na limeendelea kuziingizia kipato nchi zetu mbili.

·        Wakati wa ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala la TAZAMA linatarajiwa pia kujadiliwa, hususan namna ya kulifanya bomba hilo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya nchi zetu mbili.

c).  Ushirikiano katika Matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam:
·        Ndugu Waandishi, kama mnavyofahamu kuwa nchi ya Zambia haina bahari (land locked country), na kwa muda mrefu imekuwa ikitumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake. Kwa sababu za kiuchumi na za kihistoria, nchi hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa katika matumizi ya bandari hiyo.
·        Tunatarajia pia wakati wa ziara hiyo, Viongozi wetu wawili watapata fursa ya kujadiliana kuhusu suala hilo.

3.3         Ndugu waandishi, yapo masuala mengine ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili yatakayojadiliwa wakati wa ziara hiyo na taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.

4.0       HITIMISHO

5.1    Ndugu waandishi, kwa mara nyingine tena tunatarajia kumpokea kiongozi wa kitaifa kutoka nje ya nchi. Huu ni mwendeleze wa utekelezaji mzuri wa Sera ya Mambo ya Nje inayosimamiwa vizuri na Serikali ya Awamu ya Tano ambapo tunanuia kuimarisha mahusiano yetu, hususan ya kiuchumi, na nchi zote majirani na nyinginezo barani Afrika na  kote duniani. 

5.2    Hivyo basi, kupitia kwenu, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Mhe. Rais Lungu atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere mpaka Hoteli ya Hyatt Regency/Kilimanjaro atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Julius K. Nyerere/Pugu.

Asanteni!



Friday, November 18, 2016

Waziri Mahiga asaini Mkataba na Serikali ya China


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China  nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Lu Youqing wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya uwekwaji wa samani katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Tukio hili limefanyika mapema leo Wizarani Jijini Dar es Salaam


Mazungumzo yakiendelea kabla ya kusaini mkataba

Mhe. Waziri Mahiga akifafanua jambo kwa Balozi wa China nchini Tanzania Balozi Dkt. Youqing walipokutana Wizarani Jijini Dar es Salaam

Thursday, November 17, 2016

WAZIRI MAHIGA AKUTANA NA MABALOZI



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
 

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 



            20 KIVUKONI FRONT,
            P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb), amepokea Nakala za Hati za Utambulisho za Waheshimiwa Mabalozi Wateule wa Nchi za Yemen na Saudi Arabia na baadaye kufanya mazungumzo na Waheshimiwa Mabalozi wa  Malawi na Japan leo ofisini kwake.

Wakati wa mazungumzo na Balozi Mteule wa Saudi Arabia, Mhe. Mohammed Mansour Al-Malik viongozi hao walisisitiza umuhimu wa Tanzania na Saudi Arabia kuimarisha uhusiano na ushirikiano hususan katika nyanja za biashara na uchumi. Dkt. Mahiga  alimweleza Balozi Mteule kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alifurahishwa na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mhe. Adel Al Jubair  aliyoifanya nchini mwezi Machi 2016. 

Wakati wa ziara hiyo, Rais Magufuli aliomba Serikali ya Saudi Arabia kupitia Mfuko wa Serikali (Saudi Fund) kufadhili ukamilishwaji wa miradi mbalimbali ya barabara hapa nchini. Ombi hilo liliafikiwa na ujumbe kutoka Saudi Arabia ulifanya ziara nchini hivi karibuni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo kumualika Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo  kutembelea Hifadhi za Taifa zilizopo hapa nchini. Mhe. Waziri alikubali isipokuwa alisema atakuja wakati mwingine na mwanae wa kiume ambaye anapenda sana kuona paka wakubwa akimaanisha wanyama wakubwa kama simba, chui, tembo na faru.

Kwa upande wake, Balozi Mteule wa Saudi Arabia aliahidi kusimamia utekelezaji wa yote yaliyoafikiwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake na masuala mengine yenye maslahi ya pande zote mbili.

Wakati wa mazungumzo na Balozi Mteule wa Yemen, Mhe.  Fikri Taleb Abubaker Al-Sakaf, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo pia kuwaalika wafanyabiashara wakubwa kutoka Yemen kuja kuwekeza Tanzania. Alisema kuna wafanyabiashara wengi wenye asili ya Yemen wamefanikiwa kibiashara hapa nchini.

Aliongeza kuwa historia inaonesha kwamba watu kutoka Yemen ndio walikuwa wa kwanza kufanya biashara za maduka ya bidhaa muhimu nchini ambao walikuwa na utaratibu wa kukopesha bidhaa na kulipa baadaye. Alisema watu hao kutoka Yemen pia ndio walikuwa na utaratibu wa kupeleka bidhaa hadi vijijini na kukopesha wateja wao ambao leo unatumiwa na wafanyabiashara wa Tanzania kwa jina maarufu wamachinga.

Kwa upande wake, Balozi Mteule wa Yemen aliahidi kuwa atafanya kila awezalo kushawishi makampuni makubwa kutoka Yemen kuja kuwekeza nchini. Alisema kama watu wa Yemen walikuwa wanafanya biashara ndogo ndogo huko nyuma hapa nchini, kuna haja sasa ya kupanua wigo na kuingia katika biashara kubwa.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Malawi, Mhe. Hawa Ndilowe, wawili hao walisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Aidha, Mhe. Ndilowe alimweleza Waziri Mahiga kuwa Malawi imejipanga kuandaa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi (JPC) mwezi Desemba 2016. Alieleza mara ya mwisho kufanyika mkutano huo ilikuwa mwaka 2003 nchini Tanzania, hivyo kuna umuhimu wa kuitisha mkutano huo ili kutoa fursa kwa wadau kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano pamoja na kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zinazotukabili.

Waziri Mahiga alikaribisha uamuzi huo kwa furaha kwa kusema kuwa wakati wa mkutano huo itakuwa fursa nzuri ya kufafanua masuala mbalimbali ambayo yamefanyiwa mabadikiko na Serikali ya Awamu ya Tano, hususan katika sekta ya usafirishaji katika Bandari ya Dar es Salaam, mifuno ya ulipaji kodi, uhamiaji na biashara za mipakani.

Aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Malawi zinatakiwa kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama, hususan katika kukabiliana na mauaji ya watu wenye ualbino ambayo yameikumba nchi zao.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Japan hapa nchini, Mhe. Masaharu Yoshida, Waziri Mahiga alipongeza ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao umejikita katika kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu hapa nchini kwa ajili ya maendeleo.

Aidha, akitoa maoni yake kuhusu Mkutano wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (TICAD VI)  uliofanyika kwa  mara ya kwanza Afrika, Jijini Nairobi mwezi Agosti, 2016, Waziri Mahiga alisema mikutano hiyo ni jukwaa muhimu linalotoa fursa kwa nchi za Afrika na Japan kujadili maendeleo. Pia alipongeza agenda zilizojadiliwa kwenye mkutano wa TICAD VI ikiwemo kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uendelezaji wa viwanda; Kuboresha sekta ya Afya kwa maisha bora na kusaidia jitihada za kudumisha amani na utulivu katika jamii kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 17 Novemba, 2016.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi Mteule wa Yemen nchini Mhe.Fikri Taleb Abubaker Al Sakaf mara baada ya kuwasili Wizarani kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akionesha Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Yemeni nchi Tanzania Mhe.Fikri Taleb Abubaker Al Sakaf mara baada ya kukabidhiwa 

aziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi Mteule wa  Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Mohammed Bin Mansoor Al Malyk alipowasili Wizarani Jijini Dar es Salaam  kukabidhi Nakala za Hati za Utambulisho
Balozi Mteule wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Mohammed Bin Mansoor Al Malyk  akikabidhi Nakala za Hati za Utambulisho kwa Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga Wizarani Jijini Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Hawa Ndolowe alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam
Mzungumzo yakiendelea, Kushoto ni Balozi Msaidizi wa Malawi nchini Tanzania Bw.Sai Kaphale na Kulia ni maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo yalikuwa yakiendelea.



Wakiwa katika picha ya pamoja

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe.Masaharu Yoshida alipomtembelea kwa mazungumzo yaliyofanyika Wizarani Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo yakiendelea. Kushoto ni Maafisa kutoka Ubalozi wa Japan nchini Tanzania na kulia ni Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea

Tuesday, November 15, 2016

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Algeria nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza Balozi wa Algeria nchini Tanzania Mhe. Saad Belabed katika mazungumzo yaliyofanyika Wizarani Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifanunua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Algeria nchini Tanzania Mhe. Saad Belabed. Kulia ni Afisa wa Wizara akifuatilia mazungumzo

Waziri Mahiga azungumza na Wadau wa Maendeleo kutoka nchi za Nordic na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo kwenye Mkutano na Wadau wa Maendeleo kutoka nchi za Nordic uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Nchi za Nordic zinatoa mchango mkubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini ikiwemo kilimo na miradi ya maji. Nordic inaundwa na Nchi tano ambazo ni Norway, Finland, Iceland,Sweden na Denmark. 

Mkutano ukiendelea

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Bw.Alvaro Rodrigues  akizungumza wakati wa mkutano

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway Bi. Sive Cathrine Moe akizigumza wakati wa mkutano

Baadhi ya Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakifuatilia Mkutano.

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland, Mhe. Kai Mykkanen alipomtembelea kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Wawili hao wamezungumzia masuala mbalimbali kuhusu masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya huduma za kijamii nchini. Mhe. Kai katika mazungumzo hayo ameahidi kupitia Wizara yake ataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za maendeleo sambamba na kuendelea kushawishi sekta binafsi za Finland kuja kuwekeza nchini.

Mhe. Waziri, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland  Mhe. Kai Mykkanen

Mazungumzo yakiendelea

Mhe. Waziri, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza  Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Finland  Mhe. Kai Mykkanen walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam

Monday, November 14, 2016

Waziri Mahiga apokea hati ya utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman, Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs alipowasili Wizarani Jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi hati ya utambulisho 

Mhe. Wiziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Ubalozi mdogo wa Oman, Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs
Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na  Konseli Mkuu wa Ubalozi wa mdogo wa Oman Zanzibar Mhe. Ahmed Hamood Al Habs mara baada ya kukabidhi hati ya utambulisho

Mazungumzo yakiendelea 

Wakiwa katika picha ya pamoja